Mwambusi ana deni Coastal Union

KOCHA Mkuu wa Coastal Union, Juma Mwambusi amesema kazi imebaki kwake na wachezaji kuhakikisha kupambana ili kufikia malengo ya kucheza tena Ligi Kuu Bara msimu ujao baada ya uongozi kufanyia kazi usajili dirisha dogo.

Coastal Union ambayo ipo nafasi ya 11 baada ya kukusanya pointi 18 kwenye mechi 16 ilizocheza imeongeza wachezaji tisa dirisha dogo la usajili lililofungwa Januari 15.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwambusi alisema usajili umezingatia mahitaji na ana imani na wachezaji walioongezwa kilichobaki ni mipango imara kuhakikisha wanafanya vizuri mzunguko wa pili.

“Naamini maingizo mapya na wachezaji waliopambana mzunguko wa kwanza licha ya kutokuwa vyema wakiungana wataisaidia Coastal Union kurejesha makali na kuwa timu ambayo itacheza tena msimu ujao japo haitakuwa rahisi bila mipango imara,” alisema.

“Tuna mechi tano mwezi ujao ambao ndio ligi inarejea baada ya maboresho ya ratiba kati ya hizo nyumbani tutakuwa na michezo miwili – hiyo ni lazima tuhakikishe tunapata pointi zote sita na mingine mitatu ugenini.”

Mwambusi alisema maandalizi kwa ajili ya mechi za mzunguko wa pili yanakwenda vizuri na wachezaji wake wapo kwenye hali nzuri ya kiushindani huku akidai kuwa ameanza kwa kufanyia kazi upungufu uliojitokeza katika mzunguklo wa kwanza na kuwajenga wachezaji wake kisaikolojia ili waweze kurudi vyema katika ushindani. Msimu uliopita timu hiyo ilimaliza ligi ikiwa nafasi ya nne katika msimamo.

Related Posts