WAKATI mashabiki wa Yanga wakiwa na hamu kubwa ya kumuona nyota mpya wa kikosi hicho, Jonathan Ikangalombo ‘Ikanga Speed’ katika mchezo wa Kombe la Shirikisho la (FA), dhidi ya Copco FC, mambo yamekuwa ni tofauti baada ya kukosekana baada ya kocha Sead Ramovic kumchomoa kikosini.
Nyota huyo aliyesajiliwa katika dirisha dogo la Januari akitokea AS Vita Club ya kwao DR Congo ni miongoni mwa wachezaji wawili waliosajiliwa na kikosi hicho cha Jangwani, akiungana pia na beki wa kulia, Israel Mwenda aliyetoka Singida Black Stars.
Katika kikosi cha Yanga kinachocheza mchezo huo wa hatua ya 64 bora, Ikanga amekosekana hata benchi huku walioanza ni Aboutwalib Mshery, Israel Mwenda, Nickson Kibabage, Bakari Mwamnyeto, Jonas Mkude na Salum Aboubakar ‘Sure Boy’ na Farid Mussa.
Wengine ni Prince Dube, Duke Abuya, Stephane Aziz Ki na Shekhan Khamis ambao wanapambana kurejesha furaha kwa mashabiki wa timu hiyo, baada ya kutupwa nje katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, kufuatia kuishia hatua ya makundi.
Yanga inapambana kutetea taji la michuano hilo ambalo ililichukua msimu uliopita, wakati ilipoifunga Azam FC kwa mikwaju ya penalti 6-5, baada ya timu hizo kutoka suluhu dakika 120, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Amaan visiwani Zanzibar.