Serikali yaeleza sababu za kukatika umeme

Dar es Salaam. Wakati kukiwa na malalamiko ya kukatika mara kwa mara kwa umeme, Serikali imesema kwa sasa nchi inazalisha umeme kuliko uwezo wa mahitaji ya nishati hiyo,  baada ya kukamilika kwa ujenzi wa  bwawa la kufua umeme la Mwalimu. Nyerere.

Hayo yamesemwa leo Jumamosi Januari 25, 2025 na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, katika mkutano wake na waandishi wa habari, uliofanyika Hifadhi ya Mikumi mkoani Morogoro.

Pamoja na kugusia mambo mbalimbali ya nchi, Msigwa aligusia suala la upatikanaji umeme nchini na kueleza kuwa ni moja ya  sababu kubwa ya Tanzania kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa mkutano mkubwa wa nishati Afrika unaotarajiwa kufanyika Januari 27 hadi 28 jijini Dar es Salaam ambapo washiriki wataweza kujifunza kutoka nchini.

 “Uwezo wetu kwenye gridi ya Taifa ni megawati 3410 ni kiasi kikubwa cha umeme tunachozalisha ukilinganisha na mahitaji yetu ambayo ni megawati 1888. Tuna umeme mwingi kwenye gridi ya Taifa na sasa tunajenga miundombinu ya kusafirisha umeme tuutoe kwenye bwawa letu la umeme tupeleke kwenye nchi jirani za Kenya na Zambia,” amesema Msigwa.

Hata hivyo, Msigwa amesema pamoja na kuongeza uzalishaji, kazi kubwa inaendelea kufanywa ya kuimarisha miundombinu ya kusambaza umeme ambayo sio tu kwa kupeleka nchi jirani bali kuhakikisha na usambazaji ndani ya nchi unakuwa imara.

“Tunao mradi unaitwa gridi imara, ambao huu mradi kazi yake kubwa ni kuhakikisha tunaimarisha njia za kupeleka umeme kwenye majumba ya watu kutoka wilaya hadi wilaya, kutoka mkoa hadi mkoa. Lakini pia kujenga vituo vya kupoozea umeme sababu haya ndio maeneo makubwa ya kitaalamu,” amesema Msigwa.

Aidha, amesema ukisikia sasa hivi Watanzania wanasema umeme unakatika, haukatiki kwa sababu kuna upungufu wa umeme gridi ya Taifa bali ni kwa sababu ya changamoto za kimiundombinu.

Amesema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kupitia Tanesco kwenye uzalishaji umeme na sasa wanaendelea kwenye miundombinu ili kuhakikisha nishati hiyo inawafikia Watanzania bila kukatika.

“Hivi ninavyozungumza na nyinyi tumeshafikisha asilimia 99 kwa maeneo ya mijini watu wanapata umeme na tuna asilimia 60.6 katika maeneo ya vijijini,” amesema Msigwa.

Related Posts