Simba kuibomoa Yanga, yaanza mkakati

MABOSI wa Simba wameonyesha hawatanii. Baada ya kumvutia waya kiungo kutoka Guinea anayeichezea CS Sfaxien ya Tunisia, safari hii imeigeukia Yanga, ikipiga hesabu ya kuibomoa.

Simba inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara na kutinga robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, ikiwa wawakilishi pekee wa Tanzania waliosalia hadi sasa baada ya Yanga kutolewa makundi ya Ligi ya Mabingwa, imedaiwa imeibipu Yanga.

SIMBA imeibipu Yanga baada ya kudaiwa imebisha hodi kwa menejimenti ya kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Maxi Nzengeli kwa nia ya kutaka kumsajili kwa ajili ya msimu ujao wa mashindano.

Maxi aliyeanza kurejea uwanjani kutoka kuwa majeruhi, inaelezwa mkataba alionao na Yanga unamalizika mwisho mwa msimu huu na jambo hilo limewafanya mabosi wa Simba kuamua kutesti zali la kuanza kumfuatulia kupitia menejimenti inayomsimamia ili kujua pa kuanzia ili kutekeleza pendekezo ya kocha.

Inadaiwa kocha Fadlu Davids amemfuatilia Maxi aliyesajiliwa na Yanga msimu uliopita kwa kusaini mkataba wa miaka miwili unaomalizika baada ya duru la pili la msimu huu kuisha na kupendekeza kama inawezekana avutwe Msimbazi fasta akaliamshe goma, licha ya kuelezwa tayari Yanga nayo imeanza mazungumzo.

Kiungo huyo anayecheza kikosi cha kwanza cha Yanga tangu enzi za kocha Migueal Gamondi na sasa Sead Ramovic amekuwa na kiwango kizuri tangu atue katika klabu hiyo akitokea AS Union Maniema ya DR Congo.

Mkongomani huyo (24) msimu uliopita alimaliza akiwa na mabao 11 na asisti mbili katika mechi 23 ilizocheza Yanga, huku kwa msimu huu kabla ya kuumia alifunga mara tatu katika Ligi Kuu inayorejea Februari Mosi.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imezinasa zinasema kuwa, vigogo wa Simba wamemfuata bosi anayemmiliki kiungo huyo, Jenerali Amissi Kumba kutaka kujua mkataba alionao na Yanga ili wamsajili haraka.

Kumba ndiye mmiliki wa klabu ya AS Maniema iliyoshiriki hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu na kushindwa kupenya kwenda robo fainali kama ilivyokuwa kwa Yanga, ambapo kigogo huyo ndiye mkuu wa jeshi la nchini humo.

Bosi mmoja wa juu wa Maniema alilidokeza Mwanaspoti kuwa, Simba imemfuata Kumba ikitaka kujua mkataba halisi wa kiungo huyo na Yanga ili wafanye uamuzi wa kumsajili mapema kwa ajili ya msimu ujao.

Ingawa bado pande hizo mbili hazijakubaliana, bosi huyo amefichua kwamba Kumba amewaomba Simba wampe muda kabla ya kuwarudishia majibu.

Maxi bado hajaongeza mkataba na Yanga, ingawa Mwanaspoti linafahamu kwamba mazungumzo ya mkataba mpya yamefanyika na kilichobaki ni pande hizo mbili kukubaliana kwa hatua ya mwisho ya kusaini.

“Simba wanamtaka Maxi, wanasema ni mchezaji wanayemuona atafanya vizuri katika kikosi chao, walishampigia simu Jenerali (Kumba) ila waliambiwa wasubiri,” alisema bosi huyo mkubwa ndani ya Maniema na kuongeza;

“Yanga haijamuongezea mkataba bado, ingawa walishampigia Jenerali kumjulisha kwamba wanaendelea na mazungumzo na Maxi, sijajua watakubaliana lini ila najua mchezaji huyo hawezi kusaini hadi kwanza azungumze na Jenerali Kumba.”

Maxi amekosekana kwa muda sasa ndani ya kikosi cha Yanga, baada ya kuwa majeruhi ambapo juzi alionekana akijifua na kikosi cha timu hicho kwenye Uwanja wa KMC Complex, wakati timu hiyo ikijiandaa na mchezo wa Kombe la Azam Shirikisho unaopigwa leo jioni dhidi ya Copco FC ya Mwanza.

Related Posts