Kibaha. Ilikuwa siku tisa za mateso. Hivi ndivyo inavyoweza kuelezewa kwa kilichotokea kwa familia ya Melkizedeck Mrema na mkewe Johana Bung’ombe ambao mtoto wao wa miezi saba Merysiana alichukuliwa na watu wasiojulikana, waliovamia nyumbani kwao asubuhi ya Januari 15.
Kwa siku tisa familia ya Melkizedeck Mrema ilipitia maumivu makali ikihangaika huku na kule kumtafuta mtoto wao huku wakijuliza nia ya watu waliomchukua akiwa na umri wa miezi saba, huku wakijaribu kuwaua wazazi wake.
Hata hivyo, jitihada zilizofanywa na Jeshi la Polisi mkoa wa Pwani ziliwezesha kukamatwa kwa watu watatu wakiwa na mtoto huyo katika pori la Kimara Misare lililopo Mlandizi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase alisema baada ya kufanyika msako, Januari 24 saa tisa usiku walifanikiwa kuwakamata watu hao na mtoto huyo na alipelekwa hospitali ya Tumbi kwa ajili ya uchunguzi, uliobaini ni mzima wa afya.
Mwananchi ilifika katika kijiji cha Kumba, umbali wa kilomita sita kutoka Kibaha kwa Mfipa mkoani Pwani, kwa ajili ya mahojiano na wanandoa hao, siku moja baada ya kumpata mtoto huyo aliyepotea kwa siku tisa.
Sehemu kubwa ya kijiji hicho imezungukwa na mashamba na mapori kukiwa na nyumba chache za makazi ya watu, ikiwemo hiyo anayoishi Melkizedeck na familia yake, ambayo inaonekana kuwa ya kisasa zaidi katika eneo hilo.
Licha ya kulazimisha kutabasamu, uso wa Johana haukuficha uchovu alionao kutokana na kile alichopitia katika siku tisa zilizopita, tofauti na alivyoonekana mume wake ambaye muda wote alikuwa akitabasamu na kucheza na mtoto wao.
Katika mahojiano hayo, Johana anasema hadi sasa hafahamu watu hao walikuwa na lengo gani hadi kuwasababisha maumivu makali kiasi hicho, kwa kuwatenganisha na mtoto wao wa pekee kwa siku tisa, bila kueleza chochote.
Hata hivyo, mama huyu anasema ndani ya moyo wake alikuwa anaamini kwamba mtoto yuko hai, ila hofu kubwa ilikuwa maisha anayoishi mikononi mwa watu hao ambao walionekana dhahiri kuwa na nia ovu dhidi ya familia hiyo.
“Siku ambayo tukio limetokea, walitutesa kwa kutupiga, kutujeruhi na kututumbukiza kwenye mashimo ya choo kwa nia ya kutuua, hata hivyo hayo hayakuwa mateso kama niliyopitia katika siku zote tisa ambazo mtoto hakuwa kwenye mikono yangu.
“Ilikuwa ni maumivu makali kwangu, kila nilipofikiria hali ya mtoto wangu huko aliko, ilipofika muda wa kula nilifikiria hivi mwanangu amekula na anapewa chakula gani. Kilichokuwa kinaniumiza kichwa zaidi ni je, watazingatia muda wa kumpa chakula kama ninavyofanya mimi,” anasema Johana na kuongeza.
“Nilikuwa nahofia mtoto wangu anapenda kula na akikosa chakula Analia, sasa nikawa nawaza asije akawalilia mwisho wakaamua kumpa chochote ale ili anyamaze, kingine kilichokuwa kinaniumiza kichwa, mwanangu huwa anaamka alfajiri kunyonya je, hao watu watampa nini muda huo? Kingine nilichokuwa nafikiria mtoto wangu ana mzio wa ngozi hapaki kila mafuta, sasa nikawa nawaza ikiotokea wakampaka mafuta itakuwaje?” amesema.
Mbali ya mahitaji ya kibinadamu, Johana anasema hofu nyingine aliyokuwa nayo ni watu hao kumfanyia vitendo vya ukatili wa kijinsia mtoto huyo kama ambavyo imekuwa ikiripotiwa kuwepo na ongezeko la matukio ya ukatili dhidi ya watoto.
Anasema kuna wakati uvumilivu ulikuwa unamshinda, hivyo kujikuta akibubujikwa na machozi akiwaza hatima ya mwanaye, hata hivyo faraja aliyokuwa anaipata kutoka kwa watu mbalimbali ilimtia nguvu.
“Sikujua kama Watanzania wana upendo kiasi hiki, katika siku hizi tisa tumetembelewa na watu wengi tusiowafahamu wakitupa pole na kutufariji, viongozi wa dini, makundi ya wanawake walikuwa hawakauki hapa nyumbani, hapo bado ndugu, jamaa na marafiki.
“Kwa kifupi nimepitia kipindi kigumu mno kwenye maisha yangu na kila kitu kilisimama. Nashukuru watu waliokuwa wanakuja kunifariji na kuniombea, wengi wao waliniambia mtoto yupo salama tuendelee kumuombea Mungu amlinde na hilo tulilifanya kwa uaminifu mkubwa mimi na mume wangu, hatimaye jana maombi yetu yakajibiwa,” amesimulia mama huyo.
Alivyokutanishwa na mwawawe
Johana anasema mchana wa Januari 24, mume wake alipokea simu kutoka kwa mmoja wa ndugu zao aliyewapongeza kwa kupatikana mtoto, akiwaeleza kuwa ameona taarifa hizo kwenye mitandao ya kijamii.
“Hatukuelewa ujumbe ule kwa sababu hatukuwa na taarifa zozote hadi muda huo kutoka polisi, hivyo mume wangu akafunga safari kwenda polisi kujua kinachoendelea. Alipofika kwenye kituo cha polisi akaambiwa ni kweli mtoto amepatikana akiwa salama kabisa, lakini taarifa rasmi tutapewa na kamanda wa polisi wa mkoa.
Mume wangu baada ya kupewa majibu yale alinipigia simu kunipa habari hiyo njema iliyotufanya tupige kelele za furaha na kumshukuru Mungu. Hakika ilikuwa kipindi cha kupima uvumilivu wetu na imani yetu kwake,”
Anasema baada ya taratibu hizo kukamilika yeye na mumewe waliitwa kwenye ofisi ya kamanda wa polisi walihojiwa na hatimaye wakakabidhiwa mtoto wao ambaye hata hivyo kwa mara ya kwanza walishindwa kutambua kwamba ni yeye.
“Tulipofika kwenye eneo la makabidhiano tulimuona mtoto akiwa na mwanamke ambaye baadaye tulikuja kujua ni wa ustawi wa jamii. Kwa haraka haraka tulishindwa kumtambua mtoto wetu kwa sababu alikuwa amebadilika mno, amepungua na ngozi yake imefubaa, tofauti na alivyokuwa awali.
“Baada ya kumuangalia kwa makini tukagundua ni yeye, kiukweli nilitokwa na machozi ya furaha, hata hivyo furaha hiyo iliambatana na maumivu makali pale nilipotaka kumchukua akanikataa, akawa anamlilia yule mama wa ustawi wa jamii. Baadaye nilikuja kuelewa huenda ilikuwa hivyo kwa sababu katika muda mfupi aliokaa naye tayari alishamzoea,” amesema.
Anasema hali hiyo iliendelea kwa dakika kadhaa kabla ya mtoto kumtambua na kumkubali na uhusiano wao ukaanza upya.
Johana anasema, “yule mtu wa ustawi wa jamii aliniambia niwe namkumbusha mtoto vitu vya zamani na vile alivyokuwa anavipenda, ikiwemo michezo ili iwe rahisi kwake kututambua kwa sababu kuwa mbali na sisi kwa kipindi chote hicho huenda imemuathiri kisaikolojia.
“Nilikubaliana na hilo kwa sababu baada ya kunitambua na kunikubali alibadilika akawa anamkubali kila anayeonyesha nia ya kumbeba. Kwa kawaida mtoto wangu hayuko hivyo, ndiyo maana nakubali hoja ya kwamba inawezekana ameathirika kisaikolojia, lakini hakuna athari nyingine yoyote ya kimwili amepata, hata daktari amethibitisha.”
Anasema baada ya kukamilisha taratibu zote hatimaye walikabidhiwa mtoto na kurudi naye nyumbani na kidogo kidogo akaanza kuwazoea wanafamilia.
“Alianza kwa kushangaa shangaa, taratibu akatuzoea na maisha yamerejea kama zamani, ingawa hapa nyumbani kuna watu wengi ambao wamekuja baada ya tukio hili, sitamani atoke mbele ya macho yangu. Kuna muda natamani angekuwa na uwezo wa kuzungumza atusumulie kilichomtokea katika kipindi chote hiki.
“Kwa kuwa anapenda kula kwa sasa naweka nguvu kwenye kuhakikisha anapata lishe ya kutosha, ili kumrudisha kwenye afya yake kama ilivyokuwa awali. Sijui hawa watu walikuwa wanaishi naye wapi na kumpa chakula gani, maana amedhoofika na hata ule ung’avu wa ngozi haupo tena.”
Johana anasema licha ya kuwasamehe watu hao kama Mungu anavyoelekeza umuhimu wa binadamu kusameheana, shauku yake ni kuona sheria inachukua mkondo wake na wanapewa adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine.
“Ndani ya moyo wangu nimewasamehe kwa sababu Mungu anatufundisha kusamehe saba mara sabini, ila kwa mamlaka zinazohusika kwa sababu wametuhakikishia hawa watu wamewakamata, basi hatua kali zichukuliwe dhidi yao ili iwe funzo kwa vijana wengine wanaofikiri wanaweza kufanya upuuzi wa aina hii kwenye familia za watu.
“Sitamani maumivu niliyopitia mimi na familia yangu wayapitie wengine, kwa sababu hawa watu wangekuwa na nia ya kuiba vitu wangefanya hivyo na kuondoka, maana tuliwapa kila walichotaka ila wakaona haitoshi watuachie maumivu ya kuondoka na mtoto wetu,” anasema Johana.
Itaendelea kwa kuangazia ilivyokuwa siku ya uvamizi, walivyookolewa kwenye mashimo ya nyumba tofauti ya vyoo, jinsi wasiojulikana walivyomchukua mtoto.