Rukwa. Miili ya wavuvi tisa kutoka kata za Mtowisa na Nankanga, wilayani Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa waliopoteza maisha kutokana na dhoruba katika Bonde la Ziwa Rukwa usiku wa Januari 23, 2025, imeopolewa leo Jumamosi.
Ajali hiyo ilisababishwa na upepo mkali uliovuma kwenye ziwa hilo, ambapo taarifa zinaeleza kuwa wavuvi 540 waliokolewa, huku wengine 10 wakiripotiwa kutoonekana baada ya dhoruba hiyo.
Awali akizungumza leo Jumamosi Januari 25, 2025 mkoani Rukwa, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa amesema miili tisa imepatikana katika operesheni ya uokoaji inayoendelea kwenye ziwa hilo.
Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji mkoani humo, Chacha Mchaka
ameiambia Mwananchi jioni hii kuwa miili iliyoopolewa imefikia tisa na kazi ya uokozi kwa leo imesitishwa mpaka kesho watakapoendelea kuutafuta mwili mmoja uliosalia.
Waziri Bashungwa akiwa ameambatana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Ashatu Kijaji, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Edwin Mhede, ametoa pole kwa wananchi wa Kijiji cha Nankanga.
“Kwa taarifa tulizozipata sasa, pamoja na jitihada nzuri za mafanikio ya kuokoa ndugu zetu 540 ambao tumewaokoa kutoka ziwani kwa takwimu za jana (juzi), bahati mbaya taarifa nilizo nazo sasa kutoka kwa wanaoendelea na ukoaji ziwani tumewapoteza ndugu zetu saba hadi saa sita mchana,” amesema waziri huyo.
Amesema shughuli ya ukoaji inaendelea ikiongozwa na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji (CGF), John Masunga ambaye anatumia helkopta kuwasiliana vikosi maalumu vya uokoaji ambavyo vinashirikiana na wananchi.
Amesema vikosi hivyo vina jumla ya vyombo 19 vya uokoaji katika operesheni hiyo.
Bashungwa ametoa wito kwa wananchi kufuatilia na kuzingatia taarifa zinatolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) kwa sababu Serikali imeiwezesha mamlaka hiyo kuwa na vifaa vya kisasa vinavyotoa taarifa za uhakika kwa wakati.
Aidha, Bashungwa amesema Serikali inaendelea kuimarisha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili kuteleleza majukumu yake kwa ufanisi.
Amesema Serikali imeliwezesha jeshi hilo kununua helikopta moja ya kuokoa na kuzima moto, magari 150 ya kuzima moto, magari 40 ya kubebea wagonjwa na boti 23 za kuzima moto na uokoaji.
Kamishna Jenerali Masunga amesema oparesheni ya ukoaji inaendelea vizuri kwa kuhakikisha wavuvi wote waliokuwa ziwani wanapatikana wakiwa hai au kupata miili yao.
Amesema kikosi maalumu cha askari cha uokoaji kutoka Dar es salaam kitafika kijijini hapo kuongeza nguvu ya uokozi kwa kushirikiana na askari wenzao pamoja na wananchi wanaoendelea na shughuli hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Sumbwanga, Nyakia Chirukile amesema shughuli ya wananchi kuitambua miili ya ndugu zao inafanyika katika zahanati ya kijiji Nankanga ili kuwezesha taratibu za mazishi kufanyika.
Diwani wa Kata ya Nankanga, Anyisile Kayuni ametoa shukurani kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa faraja na upendo mkubwa kwa wananchi kwa kuwaagiza mawaziri kuja na vikosi maalum kuweka kambi na kuhakikisha ukoaji unafanyika pamoja na shughuli nyingine.
Awali, Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, Chacha Mchaka, aliwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari pindi wanapoona dalili mbaya ya hali ya hewa kama hakuna ulazima wa kuingia ziwani au shambani ili kuepuka madhara yatokanayo na hali hiyo.
Meneja wa TMA Mkoa wa Rukwa, Felix Kibona amesema wameendelea kutoa tahadhari ya kujikinga na hali mbaya ya hewa na kusema kuwa mara nyingi mgandamizo wa hewa ukipungua upepo unakuwa na uwezo wa kutembea kutoka sehemu moja kwenda nyingine kutokana na utofauti wa mgandamizo wa hewa.
Pia, amewataka wananchi kufatilia utabiri wa hali ya hewa pindi wanapotangaza ambapo siku chache zilizopita walitangaza upepo unaofikia kilomita 40 kwa saa na mawimbi yanafikia zaidi ya mita mbili hivyo kinachotokea Ziwa Tanganyika ndicho ambacho kinatokea ziwa Rukwa na kusema ni hali ya hewa ya kawaida.
Amesisitiza wananchi waendelee kuchukua tahadhari kabla ya kuingia ziwani wawe na taarifa sahihi za utabiri wa hali ya hewa ambazo huwa zinaonyesha hali kulingana na mazingira.
Baadhi ya wananchi akiwamo Annacreta Exavery mkazi wa Kata ya Mtowisa amelipongeza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kazi kubwa waliofanya na kulitaka kuongeza kasi na juhudi za kutafuta miili ya wavuvi waliosalia katika ziwa hilo.
Ikumbukwe Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitangaza kuwepo na mvua za chini ya wastani hadi juu ya wastani zitakazotarajiwa kuwa na matukio ya hali mbaya ya hewa, kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.
TMA ilisema vipindi vya mvua kubwa vinatarajiwa kujitokeza na kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi, yanayoweza kusababisha uharibifu wa miundombinu, mazingira, mlipuko wa magonjwa pamoja na upotevu wa mali na maisha.
Mvua hizo zinatarajia kunyesha msimu wa masika Machi- Mei 2025 za chini ya wastani hadi wastani ni maeneo ya mikoa ya Pwani, Kigoma, Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Morogoro, Tanga, Dar es Salaam na visiwa vya Unguja na Pemba.
Hata hivyo, mikoa inayopata mvua za wastani hadi juu ya wastani ni mashariki mwa mikoa ya Simiyu na Mara.