Wanawake wenye vyeo, Madaraka hawafai kuolewa? – Global Publishers


Mwaka huu ulipanga kufanya nini na mwenzi wako? Nini ambacho hakijakamilika? Kwa sababu gani hamjakamilisha? Mkishajua wapi mmekwama, basi ni suala la msingi sana ili kuweza kufikia ndoto zenu ambazo mlizianza siku za nyuma.

Muhimu ni kwamba, hakuna kukata tamaa, hata kama mmepitia kwenye changamoto kubwa ya aina gani, aminini bado mnayo nafasi ya kusimama na kutimiza malengo yenu. Muhimu ni kuwa na afya njema, zielekeeni ndoto zenu kwa nguvu zote.

Bila kupoteza wakati, twende kwenye mada ya leo kama inavyojieleza hapo juu. Kumekuwa na hii kasumba ambayo naweza kusema kwa sasa, tayari imeshajengeka kwenye vichwa vya watu wengi hususan wanaume.

Wanaamini kwamba, wanawake wakishakuwa na pesa au cheo fulani huwa ni vigumu sana kuolewa. Kwamba hawawezi kudhibitiwa na wanaume wao kwani nao wanajiona kwamba wana mamlaka kamili, hawawezi kutikiswa na wanaume.

Mwanamke ana kazi nzuri, ana mshahara wake mzuri pengine kupita hata wa mwanaume, utamwambia nini? Anataka na yeye anyenyekewe na mume au mwanaume wake kama ambavyo vijana wa kiume wanavyomnyenyekea anapokuwa kazini au kwenye biashara yake.

Yes, yeye ni bosi kwenye ofisi yake, hivyo si vijana wa kiume tu wanaomnyenyekea bali hata wa kike. Wapo hadi wazee wanaomwamkia ofisini kwake, si kwa sababu amewazidi umri, bali wanafanya hivyo kutokana na nafasi aliyonayo.

Waswahili wanakwambia; ‘mtumikie kafiri’ ili mambo yako yaende. Watu wazima kabisa wenye familia zao nyumbani, wanamnyenyekea binti mdogo ambaye wanaweza hata kumzaa. Jamani haya mambo yapo na tunayaona!

Sasa unategemea nini kwa mwanamke wa aina hii pindi anaporudi nyumbani halafu mumewe ajifanye analeta ‘kibesi’ au amri ya kumwambia amuwekee maji ya kuoga kama hataambiwa akaweke mwenyewe.

Ndugu zangu, hapa ndipo kwenye kiini cha hoja yangu. Ni vizuri sana kujifunza kwa undani ni nini hasa kinachosababisha haya? Ni hulka tu ya mtu ambayo wakati mwingine inaletwa na madaraka au pesa kama nilivyosema.

Tabia zinazoletwa na pesa au madaraka, huwa ni vigumu sana kuzidhibiti, si wanawake tu hata wanaume wapo wanaoshindwa kujizuia. Wakipata vyeo au madaraka, hujikuta wamebadilika sana. Wanafanya mambo ya hovyo ambayo awali walikuwa hawayafanyi.

Hivyo basi, hili suala ni mtambuka. Muhimu hapa kujifunza tu kwamba, binadamu tunapaswa kuishi kama binadamu. Uwe na madaraka au hauna, utu uwe ndiyo kila kitu. Kiburi cha pesa au madaraka ni cha muda tu na kinaweza kutoweka muda wowote.

Muhimu sana ni kuishi kwenye misingi ya kibinadamu. Kujiheshimu na kuheshimu wengine. Kujua nini wajibu wa mke au mwanamke kwa mwanaume wake. Pesa na madaraka visikutoe akili ukafanya ya kijinga. Vitu vyote hivyo vinakuja, vinatafutwa na vinaweza kutoweka, lakini heshima na utu wako utabakia.

Kwa msingi huo, wanawake wenye vyeo na madaraka wanaweza kuolewa na kuishi kwa nidhamu ya kike kama tu watazingatia haya niliyoyasema. Kama tu hawataamua kujitoa ufahamu au kupofushwa na vyeo au madaraka.

Asanteni kwa kunisoma, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri.

Related Posts