Wanne wakutwa na kipindupindu Mbeya, hatua zachukuliwa

Mbeya. Wakati Kata ya Isyesye jijini Mbeya ikitaja watu wanne kugundulika kuwa na kipindupindu, serikali ya kata hiyo imesema itawachukulia hatua kali wazazi na walezi watakaokaidi kulipia chakula cha wanafunzi shuleni ifikapo Januari 30 mwaka huu ili kuepusha kuenea kwa ugonjwa huo.

Pia imekataza aina yoyote ya mikusanyiko na vyakula pale inapotokea msiba wa aina yoyote mtaani humo ikieleza kuwa Serikali itasimamia mazishi na atakayekaidi maelekezo atachukuliwa hatua.

Akizungumza wakati wa mkutano wa hadhara, Afisa Mtendaji wa Kata hiyo, Peter Mapinda amesema Serikali imezuia aina yoyote ya mikusanyiko na vyakula inapotokea msiba badala yake uongozi utahusika wenyewe katika  mazishi.

Amesema baada ya kata hiyo kubainika kuwa na idadi ya watu wanne waliokumbwa na mlipuko wa kipindupindu, Serikali imezuia wanafunzi kununua vyakula vinavyouzwa maeneo ya shule badala yake chakula kitatolewa shuleni hapo.

“Nitumie mkutano huu kuwakumbusha, ikifika Januari 31 kwa wale wazazi na walezi ambao watakuwa hawajalipia chakula shuleni, nitakuwa msitari wa mbele kuongozana nao mahakamani, hatuwezi kuvumiliana katika hili”

“Serikali ilizuia vyakula vya aina yoyote kuuzwa shuleni, lakini pia imepiga marufuku mikusanyiko na mapishi ya chakula kwenye msiba, lakini wapo baadhi ya watu wanakaidi, sheria itachukua mkondo wake” amesema Mapinda.

Mapinda amewataka wananchi kuendelea kushiriki mikutano ya hadhara ili kujadili maendeleo ya kata hiyo na kuchangia kwa wakati gharama za taka ili kurahisisha shughuli za uzoaji taka ili kulinda na kutunza mazingira.

Mmoja wa wananchi, Mussa Juma amesema ili kuendana na kasi ya kupambana na mlipuko wa ugonjwa huo, mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira,  itoe huduma ya maji walau siku mbili kwa wiki.

“Tukijadili suala la ugonjwa huu niombe uongozi uwasiliane na mamlaka ya maji itupe huduma hii japo kwa siku mbili kwa wiki ili tuendane na kasi hii, vinginevyo haitawezekana” amesema Juma.

Maria Sendawa amesema wananchi wanapaswa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutokomeza ugonjwa huo, akieleza kuwa hatua zozote zitakazochukuliwa ni sahihi ili kuwalinda watoto.

“Binafsi nakubaliana na mkakati wa Serikali, wanaoathirika ni watoto wetu, kila mzazi na mlezi ajitahidi kutimiza wajibu wake na siyo kulaumu kwa kila jambo” amesema Mariam.

Related Posts