Wasomi watakiwa kutafiti usafirishaji haramu wa binadamu

Dar es Salaam. Wanafunzi wa vyuo vikuu wametakiwa kufanya utafiti na kuandika maandiko ya kisomi, kuhusu usafirishaji haramu wa binadamu ili kuibua na kupaza sauti dhidi ya ukatili huo.

Mkurugenzi wa Program wa Mtandao wa Kitaifa wa Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu, Jones John amesema hayo leo Januari 25, 2025 wakati alipokuwa wakitoa elimu  kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Tumaini kuhusu usafirishaji haramu wa binadamu.

John amesema wanafunzi wanaosomea Shahada ya Uzamivu (PhD) na elimu ya juu ngazi ya stashahada ya uzamili, wanaweza kufanya utafiti, kuandika maandiko ya usafirishaji haramu wa binadamu na kuyachapisha ili kutoa uelewa kwa jamii mapambano ya ukatili huo.

“Tunaangalia namna  kutengeneza programu ambayo itaunganisha katika kufanya utafiti ili kuhakikisha suala la usafirishaji haramu wa binadamu, linapata maelezo na kueleweka pamoja na kutambuliwa kwenye jamii husika,” amesema na kuongeza:

“Tunapoenda vyuoni kuna utajiri wa mawazo tunawashirikisha kwenye hii kampeni ya kuandika maandiko ya kitaaluma juu ya tatizo hili kulieleza na kulielewa katika mtazamo wa kimasomo,  ndiyo maana tunakishirikisha Chuo Kikuu cha Tumaini na tunatarajia kwenda katika vyuo vingine nchini,” amesema John.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Nyumba Salama (Courage Worldwide), Suzana Shoo amesema wametoa elimu hiyo kwa wanafunzi hao,  kwa kuwa matukio hayo yanatokea kwenye jamii inayowazunguuka hivyo watu wanajua  ukatili huo unatokea nje ya nchi pekee.

“Tumetoa elimu hii kwa wanafunzi hawa lengo letu kuzifikia jamii zote ili wajue tatizo linapotokea jukumu lao ni kupinga ukatili huu na kupaza sauti, kwa kuwa wanaoathirika zaidi ni watoto na wanawake, ambapo wahalifu wanawawinda tunataka wajulikane Ili sheria ifuate mkondo wake,” amesema Suzana.

Mmoja wa wanafunzi anayesomea sheria, Julieth Samweli amesema mafunzo hayo yatawasaidia wanapokutana na matukio hayo atatoa taarifa sehemu husika ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

Amesema wanakutana na matukio hao likiwemo watoto wadogo chini ya miaka 18 wanaosafirishwa kutoka sehemu wanakoishi na kuletwa mijini kwa ajili ya kufanyishwa kazi za ndani.

Related Posts