Watuhumiwa wizi wa majafafa Tabora wafikia 20

Tabora. Idadi ya watu waliokamatwa kwa kosa la wizi wa magunia ya kubebea tumbaku (majafafa) yenye thamani ya Sh1.4 bilioni imeongezeka kutoka watu 15 hadi kufikia watu 20.

Desemba 2024, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alitoa taarifa ya kukamatwa kwa watu 15 wakituhumiwa kwa wizi wa magunia hayo ambapo alitoa maelekezo kwa vyombo vya ulinzi na usalama mkoa wa Tabora, kuendeleza operesheni ili kudhibiti vitendo hivyo na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria.

“Hakikisheni watu wote wanaohusika na wizi huu wanakamatwa  na uchunguzi wa kina ufanyike na hatua zichukuliwe kwa mujibu wa sheria” alisema Bashe.

Akitoa taarifa ya utendaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Tabora,  Mkuu wa taasisi hiyo, Abnery Mganga amesema jumla ya watu waliokamatwa katika sakata hilo wamefika 20.

Abnery amesema watu saba  kati ya hao 20 wamefikishwa mahakamani na kukiri makosa yao ambapo wamekubali kurudisha magunia hayo kwa wakulima bure kama ilivyo utaratibu kufanya hivyo.

“Tumewafikisha mahakamani na watu saba wamekiri kufanya wizi huo na wanarudisha magunia hayo wakulima bure,” amesema.

Kuhusu watuhumiwa wengine, Abnery amesema taratibu za kisheria zinaendelea dhidi yao.

Katika hatua nyingine,  Takukuru Mkoa wa Tabora imefanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo 11 yenye thamani ya Sh28.9 bilioni, huku akidokeza kuwa miradi yenye Sh27.7 bilioni ilikutwa na upungufu wa aina  mbalimbali.

“Tumetoa maelekezo miradi yote yenye upungufu, wahusika waifanyie maboresho kulingana na ushauri tuliotoa ili kuleta thamani halisi,” amesema.

Aidha, amebainisha kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi hivyo wananchi wajiepushe na vitendo vya rushwa,  kwani itasababisha kuwachagua viongozi wasiostahili.

Wakazi wa mkoani hapa, Saidi Issa na Michael Joseph wamefurahishwa na hatua zilizochukuliwa na Takukuru,  huku wakisema wabadhirifu wanakwamisha maendeleo ya watu wengine.

Wameongeza kuwa kwa sasa taasisi hiyo imeongeza ufuatiliaji kwa kasi na utunzaji wa siri za watoa taarifa za matukio ya rushwa hivyo wakiendelea hivyo watapata taarifa nyingi muhimu kutoka kwa wananchi.

“kwa kweli kwa sasa Takukuru inatufanya tuwe na imani na kujiamini kutoa taarifa kwani usiri umekua mkubwa na kukamatwa kwa watu hao kutaondoa hasara kwa wakulima,” amesema Issa.

Related Posts