Dar es Saalam. Shirika la Reli Tanzania (TRC) limewaomba abiria wanaofanya safari zao kati ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma kupanga vizuri namna ya kufika mapema vituo vya stesheni wanavyotarajia kupandia treni hususani kituo cha Magufuli jijini Dar es Salaam na cha Samia jijini Dodoma.
Kutokana na taarifa iliyotolewa leo Januari 26, 2025 na shirika hilo kufika mapema kwa abiria hao itaepusha usumbufu unaoweza kujitokeza kutokana na baadhi ya barabara kufungwa kupisha mkutano wa kimataifa wa Nishati unaoanza kesho Jumatatu.
Awali, taarifa ya Polisi iliyotolewa jana Jumamosi Januari 25, 2025 na Kamanda Kanda Maalumu ya Polisi Dar es Salaam, Jumanne Mulir, imesema kutokana na ugeni wa viongozi watakaokuja kwenye mkutano huo, barabara zitafungwa kwa muda kuanzia leo.
Amezitaja barabara zitakazofungwa kwa muda kuwa ni Nyerere kutokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwenda katikati ya Jiji.
Nyingine ni Barabara ya Sokoine, Kivukoni na Lithuli kuanzia taa za Gerezani kwenda Hoteli ya Johari Rotana, Hyatt Regency hadi Ikulu.
Pia ipo Barabara ya Ohio kutokea Kivukoni kwenda Hoteli ya Serena na ile ya Ghana kutokea barabara ya Ohio kwenda Hoteli ya Onomo.
Vilevile Barabara ya Bibi Titi kutokea makutano ya Barabara za Ohio na Ally Hassan Mwinyi kwenda Hoteli ya Crowne na Barabara ya Azikiwe kwenda Hoteli ya Four Points, Hoteli ya Golden Tulip City Center na Hoteli ya Holiday Inn.
Pia, ipo Barabara ya Morogoro kutokea Sokoine kwenda Hoteli ya Tiffany No. 1 na ile ya Makunganya kutokea Azikiwe kwenda Hoteli ya Tiffany No. 2.
Aidha Barabara ya Garden kutokea Barabara ya Lithuli kwenda Hoteli ya Southern Sun pamoja na Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa JNICC nayo itafungwa kutokana na ugeni huo.
“Katika hatua nyingine kufuatia kufungwa kwa muda barabara hizo na Jeshi la Polisi Tanzania, TRC inapenda kuuarifu umma na abiria wanaotarajia kusafiri kati ya Dar es Salaaam na Dodoma Januari 27 na 28, 2025 kuwa treni zote ikiwemo ya Express, zitasimama kupakia na kushusha abiria katika kituo cha Pugu na kwamba utaratibu huu utahusu pia abiria wa kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam,” imefafanua.
Hata hivyo hatua mbalimbali zimeshachukuliwa kutokana na umuhimu wa mkutano huo ikiwemo wafanyakazi wa umma kufanyia kazi nyumbani, huku wanafunzi wa shule na vyuo kupumzika siku mbili.