Adebayor apiga mkwara Singida | Mwanaspoti

MSHAMBULIAJI wa Singida Black Stars, Victorien Adebayor amepiga mkwara mapema kabla ya ngwe ya lala salama ya Ligi Kuu Bara kuanza wikiendi hii, kwa sasa amepata muda mzuri wa kufanya mazoezi na timu, hivyo anarudi na moto.

Adebayor aliyesajiliwa dirisha kubwa alianza kutumika katika mechi tatu za Ligi Kuu ikiwamo ile ya kwanza dhidi ya Tanzania Prisons iliyopigwa Desemba 16, mwaka jana jijini Mbeya na Singida kushinda mabao 2-0 kisha kuifunga KenGold mjini Singida kabla ya kupoteza 1-0 nyumbani mbele ya Simba.

Baada ya mechi hiyo ligi ilisimama kuanzia Desemba 29 kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi 2025 na fainali za CHAN 2024 zilizoahirishwa kutoka Februari hadi Agosti mwaka huu na sasa inatarajiwa kurudi kwa kuchezwa michezo miwili ya viporo vya Simba na Yanga Febaruri Mosi na Pili.

Kutokana na kurejea kwa ligi hiyo, Adebayor amesema anachukulia duru la pili la Ligi Kuu kuwa ni nafasi ya kuonyesha uwezo alionao baada ya kushindwa kufanya maajabu katika mechi chache alizocheza akiwa na kikosi cha Singida.

Adebayor ambaye ni raia wa Niger, alisema anatambua ushindani wa namba ni muhimu unaomfanya mchezaji kuongeza bidii na kwa mechi tatu za awali za Ligi Kuu alizocheza tangu ajiunge na timu hiyo zilimpa muda mzuri wa kuwasoma anaocheza nafasi moja uwanjani na kukaza buti katika mazoezi.

“Kipindi ligi ilivyosimama kilikuwa kizuri kwangu, tulipata muda mwingi wa mazoezi kujua washindani wako wa namba wapoje na kocha anataka kitu gani. Napenda kuona ushindani wa namba katika nafasi ninayocheza, inanifanya niwe makini muda mwingi kuliko kuridhika nakuona hakuna wa kukusumbua pia ni afya kwa timu kufanya vizuri dhidi ya wapinzani,” alisema mshambuliaji huyo wa zamani wa RS Berkane ya Morocco ASGNN ya Niger na AmaZulu ya Afrika Kuisni. 

Kuhusu Ligi kwa ujumla ya Tanzania, Adebayor alisema ni ngumu inayohitaji nguvu na akili, akisisitiza bila mazoezi ya ufiti inakuwa ngumu kuonyesha kiwango.

“Ndoto zangu nasisitiza nikuacha rekodi ya heshima ya kutambulika nilipita katika ligi ya Tanzania, kama ilivyo kwa wachezaji wengine ambao walifanya makubwa, haijalishi nimeuanzaje msimu,” alisema.

Related Posts