Dar es Salaam. Kufuatia kuanza kwa mkutano wa nishati Afrika unaowakutanisha marais na viongozi mbalimbali wa Afrika kuanzia kesho, taasisi ya Afya ya Aga Khan imejipanga kuwahudumia kiafya wageni hao.
Utayari huo unakuja baada ya ukaguzi uliofanywa hospitalini hapo baada ya kuchaguliwa na Serikali kuwa miongoni mwa taasisi zitakazotoa huduma ya afya kwa wageni hao, ambao wameanza kumiminika nchini tangu jana usiku.
Mkutano huo utakaofanyika kuanzia Januari 27 hadi Januari 28, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNICC), unatarajiwa kuhudhuriwa na zaidi ya marais 25 na mawaziri 60 kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
Akizungumza hii leo Januari 26, 2025 na waandishi wa habari baada ya ukaguzi wa hospitali hiyo, Waziri wa Afya, Jenista Mhagama amesema lazima sekta ya afya ijipange kutokana na ugeni huo.
“Ili kuufanya mkutano huu uendelee kuwa salama ni kuzitayarisha taasisi zetu ambazo zimebobea kwenye utoaji wa tiba za kibingwa na kibobezi kuanza kujiandaa na kuchukua tahadhari ya kutoa matibabu ya namna yeyote na kwa jambo lolote litakalotokea katika kipindi hiki cha mkutano.”
‘Kama waziri mwenye dhamana ya afya pamoja na maandalizi ya muda mrefu leo nimekagua eneo la dharura kila kinachotakiwa kipo, eneo la wagonjwa mahututi (ICU), mahali viongozi au wageni watakaotaka huduma za kimataifa, eneo la vifaa tiba vifaa vya kiuchunguzi kwa kweli niseme taasisi hii wako tayari,” amebainisha.
Kwa upande, wake Mganga Mkuu wa Taasisi ya Afya ya Aga Khan Tanzania, Dk Harrison Chuwa amesema wako tayari kwa chochote kitakachotokea kwa wageni.
“Kama taasisi tumepata heshima kutambuliwa kuhudumia viongozi hawa kama watapata dharura yeyote na tuko tayari,” amesema Dk Chuwa.