Bagamoyo. Watu wanne wamefariki dunia na 20 wakijeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyotokea jioni ya jana Jumamosi, Januari 25, 2025 eneo la Msolwa, Chalinze Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.
Ajali hiyo imetolea kati ya saa 10 na 11 jioni imehusisha lori na basi dogo la abiria aina ya Coaster iliyokuwa inasafirisha msiba kutoka jijini Dar es Salaam kwenda Bukoba, Mkoa wa Kagera.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Chalinze, Allen Mlekwa akizungumza na Mwananchi amesema kati ya waliofariki dunia wanaume ni watatu na mwanamke mmoja. Majeruhi ni 20 kati yao 15 walipewa rufaa kwenda Hospitali ya Tumbi Kibaha.
Amesema miili ya waliofariki ajalini pamoja na mwili uliokuwa ukisafirishwa imehifadhiwa hospitalini hapo, huku majeruhi hao wakiendelea kutibiwa kwenye Hospitali ya Msoga wilayani Bagamoyo.
Hilo ni tukio la pili ndani ya kipindi kisichozidi mwezi mmoja, mapema Januari 2025 gari aina ya Coaster ilipata ajali maeneo ya Mazizi wilayani humo na kusababisha kifo cha mtu mmoja na majeruhi kadhaa.
Jitihada za kumtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani zinaendelea ili kueleza zaidi undani wa ajali hiyo.
Kwa taarifa zaidi endelea kufuatilia Mwananchi