Dar es Salaam. Wakati Benki ya Azania ikiweka historia ya kukusanya Sh63.3 bilioni ndani ya siku 32, asilimia 97 ya waliowekeza kwenye hati fungani hiyo ni wawekezaji mmoja mmoja.
Mauzo hayo ni mara mbili zaidi ya kiwango kilichokuwa kimekusudiwa cha kukusanya Sh30 bilioni na nyongeza ya Sh15 bilioni mpaka kufika tamati ya mauzo Desemba 6, 2024 ikiwa ni baada ya kufunguliwa Novemba 4, 2024.
Matokeo haya ya hatifungani ya kwanza tangu kuanzishwa kwa benki hii yalitangazwa rasmi wakati wa hafla ya kuiorodhesha hatifungani ya ‘Bondi Yangu’ katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) jijini hapa.
Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo ya hatifungani hiyo na kuiorodhesha DSE, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Azania, Dk Esther Mang’enya amesema takwimu zetu zinaonyesha kuwa, asilimia 97 ya waliowekeza kwenye hatifungani hiyo ni wawekezaji mmoja mmoja.
“Hii inaonesha kwamba watu binafsi wengi wanaiamini Benki ya Azania. Tunawashukuru sana wawekezaji wote kwa kutuamini na kusimama pamoja nasi katika kuleta mabadiliko chanya kwenye nchi yetu,” amesema.
Benki hiyo ilikusudia kukusanya kiasi hicho cha fedha na kuzielekeza katika utekelezaji wa malengo ya kimkakati ikiwamo utoaji wa mikopo nafuu kwa ajili ya makundi maalum kama vile kinamama, Vijana, Walemavu.
Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba mbali na kupongeza mafaniko hayo alisema Serikali itaendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji hasa kwenye masoko ya mitaji kwani ni uwekezaji wenye tija.
Alitumia nafasi hiyo kuzitaka taasisi nyingine kuiga mfano wa Benki ya Azania ili kufikia mafanikio hayo huku akisema rekodi hiyo ya mauzo inaweza kushangaza taasisi nyingine.
“Nimeambiwa pia kuwa takwimu zinaonesha asilimia 97 walikuwa wawekezaji mmoja mmoja na asilimia 3 tu ndio walikuwa wanunuzi kutoka mashirika, hii imenipa faraja sana kwani na mimi ni mmoja wa walionunua hatifungani hii kama mnunuzi wa mmoja mmoja,” amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Masoko na Dhamana (CMSA), Nicodemus Mkama amesema mafanikio yaliyopatikana ni ishara ya kuimarika kwa juhudi katika elimu ya masuala ya fedha.
“Sasa Watanzania wengi wanaelewa umuhimu wa kuwekeza kwenye hatifungani na dhamana za fedha ni hatua kubwa katika juhudi zetu za ushirikishwaji wa kifedha,” amesema.
Kiasi cha chini cha ununuzi wa hatifungani hiyo kilikuwa ni Sh500,000 huku riba ilikuwa ni asilimia 12.5 kwa kipindi cha uwekezaji wa miaka minne, riba hiyo italipwa kila miezi mitatu.