Dar es Salaam. Baada ya watumishi wa umma jijini Dar es Salaam kutangaziwa kufanyia kazi nyumbani isipokuwa wale ambao mazingira yao ya kazi yanawataka kuwepo vituoni, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia imetangaza kuzifunga shule zote na vyuo kwa siku mbili kuanzia kesho Januari 27 hadi 28, 2025 wanafunzi nao wametakiwa kusomea nyumbani kwa siku mbili wakati wa mkutano wa kimataifa wa nishati unaoanza kesho Januari 27 na 28, 2025.
Taarifa iliyotolewa usiku wa leo Jumapili Januari 26, 2025 na Kamishina wa Elimu, Dk Lyabwene Mtahabwa shule zilizofungwa ni za umma na binafsi sanjari na vyuo. Amesema hatua hiyo na kuepuka changamoto ya usafiri kutokana na kuanza kwa mkutano huo.
Dk Mtahabwa ametoa taarifa hio saa chache tangu Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa alivyotumia mtandao wa X kueleza wanafunzi wa shule na vyuo pia wanapaswa kusomea nyumbani.
“Kufuatia taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi kuwa Januari 27 na 28, 2025 watumishi wa umma wa Mkoa wa Dar es Salaam wafanyie kazi nyumbani kutokana na barabara nyingi kufungwa ili kupisha mkutano wa nishati wa wakuu wa nchi barani Afrika, mnajulishwa kuwa wanafunzi wa shule na vyuo pia mnapaswa kusomea nyumbani kwa siku hizo mbili,”imeeleza taarifa hiyo ya Msigwa.
Awali, Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka alisema watumishi wa umma wa jijini hapa wameelekezwa kufanyia kazi nyumbani isipokuwa wale ambao mazingira yao ya kazi yanawataka kuwepo katika vituo vya kazi.
Kauli na hayua za viongozi hao zimekuja ikiwa ni siku moja kabla ya kuanza kwa mkutano wa kimataifa wa nishati utakaofanyika, katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) ambapo jumla ya washiriki 2,600 wa ndani na nje ya Tanzania wamejisajili kushiriki mkutano huo jambo ambalo litafanya baadhi ya barabara muhimu tisa za Jiji la Dar es Salaam kufungwa kama ilivyotangazwa na Jeshi la Polisi.
Aidha, waajiri wa sekta binafsi wameshauriwa kuruhusu watumishi wao katika jijini humo kufanyia kazi nyumbani au kuweka utaratibu ambao hautasababisha changamoto ya usafiri kutokana na kufungwa kwa barabara tisa kufuatia mkutano huo.
Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi ilifafanua kuwa miongoni mwa wanaotakiwa kuwa kazini ni watumishi wa vyombo vya ulinzi na usalama, sekta ya afya na sekta ya usafiri na usafirishaji. Vilevile, benki hazitafungwa na biashara katika Soko la Kariakoo zitaendelea kufanyika. Hoteli na migahawa nayo haitafungwa.
Tanzania imepata fursa ya kuwa mwenyeji wa mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika kuhusu nishati (Africa Energy Summit) utakaofanyika jijini Dar es Salaam ambao umeandaliwa kwa pamoja baina ya Serikali ya Tanzania, Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika.
Mkutano huo utajumuisha marais wa nchi za Afrika 25 wakiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, wawakilishi wa wakuu wa nchi na Serikali za Afrika 21.
Wengine ni wakuu wa taasisi za kimataifa sita akiwemo rais wa Benki ya Dunia, rais wa benki ya Afrika na Rais wa Taasisi ya Rockefeller na washirika wa maendeleo watano.
Taarifa ya Polisi iliyotolewa Jumamosi Januari 25, 2025 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, ilisema kutokana na ugeni huo, barabara hizo zitafungwa kuanzia leo.