SIMBA inajiandaa kushuka uwanjani jioni ya leo kuvaana na Kilimanjaro Wonders katika mechi ya kiporo cha Kombe la Shirikisho, lakini mapema wakati kikosi hicho kikijiweka tayari, mabosi wa Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini walikuwa wakipitia faili la beki wa Wekundu hao kwa lengo la kutaka kumsajili.
Ndiyo, klabu hiyo inayonolewa na kocha wa zamani wa Yanga na FAR Rabat ya Morocco, Nasreddine Nabi imedaiwa inatafuta beki wa kushoto na tayari majina mawili yalikuwa mezani mwa vigogo wa timu hiyo, likiwamo la Ernest Luzolo anayekipiga TP Mazembe ya DR Congo.
Inaelezwa, Nabi amewasisitiza mabosi wa klabu huyo, atafurahi kama ataletewa Tshabalala kutokana na ukweli anaujua uwezo wake na kama itashindikana kabisa, basi hata Luzolo kwake itakuwa shega kwani lengo ni kuona upande wa kushoto wa ukuta wa timu hiyo unaimarishwa zaidi.
Kaizer ambayo usiku wa leo itakuwa uwanja wa nyumbani kuvaana na Free Agents katika mechi ya raundi ya 32 Bora ya Kombe la Nedbank kabla ya Jumamosi ijayo kuvaana na Orlando Pirates ugenini katika pambano la Dabi ya Soweto, inasaka beki wa kushoto ili kuimarisha kikosi hicho cha Nabi.
Kocha huyo inadaiwa ameutaka uongozi kupambana na kuhakikisha inampata Tshabalala, japo inajua inaweza kuwa ngumu na kuliweka jina la Luzolo kama chaguo la pili.
Nabi anahisi huenda Simba ikatia ngumu kwa sasa kumuachia Tshabalala anayeelekea kumaliza mkataba alionao na klabu hiyo kutokana na ushiriki wake wa michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ikitinga robo fainali baada ya kuongoza Kundi A la michuano hiyo mbele ya CS Constantine ya Algeria.
Mkataba wa Tshabalala na Simba utamalizika mwishoni wa msimu huu na Kaizer inapiga hesabu kama itamkosa kwa sasa basi itasubiri beki huyo hadi mwisho wa msimu ili impate kiulaini na kama vipi imkomalie Luzolo, ambaye ameonyesha nia ya kununua mkataba alionao Mazembe akitaka kutimka.
Taarifa kutoka kwa mtu wa karibu wa Nabi, amelidokeza Mwanaspoti kocha huyo amewataka mabosi wa klabu hiyo kuweka mkazo kwa Tshabalala anayeamini nidhamu na ubora alionao utambeba ndani ya kikosi hicho, huku akitaka kukwepa kuwajaza Wakongomani katika timu hiyo kwani kwa sasa ipo hatua ya mwisho ya kumalizana na kiungo mshambuliaji Makabi Lilepo.
Taarifa ambazo Mwanaspoti ilizonazo ni Tshabalala bado hajaongeza mkataba mpya, licha ya awali kuanza kwa mazungumzo, lakini pande mbili hazijaafikiana kuhusu ishu ya maslahi mapya na beki huyo aliwahi kunukuliwa na gazeti hili akisema ana ndoto ya kwenda kupata changamoto mpya nje ya nchi.
“Tayari nimeshacheza misimu zaidi ya 13 katika ligi ya hapa nyumbani na bado nina ndoto za kucheza nje ya Bongo ili kuendelea kujiimarisha zaidi na kutengeneza uzoefu mkubwa katika kazi yangu ya soka,” alikaririwa Tshabalala aliyeanza kuitumikia Simba tangu msimu wa 2024-2014 akiwa nyota wa kikosi cha kwanza licha ya kubadilishwa mabeki wa kumshughulisha kikosini.
Katika msimu huu beki huyo amecheza mechi zote za kimataifa na kufunga bao moja, huku katika Ligi Kuu Bara akifunga bao moja na kuasisti mara tatu.