Dar es Salaam. Wataalamu wa sheria wamesema kitendo cha mwimbaji wa muziki wa injili, Goodluck Gozbert kuchoma moto gari aliyopewa kama zawadi ni kinyume na uvunjaji wa sheria ikiwemo ya mazingira na sheria ya kanuni ya adhabu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ( The Pinal Code).
Kwa mujibu wa moja ya sheria hizi adhabu yake inaweza kuwa ni kifungo cha miaka 14 au kifungu cha miaka saba ikiwa atakutwa na hatia katika vifungu tofauti.
Hayo yanasemwa ikiwa ni siku moja tangu msanii huyo kuchapisha video akichoma gari aliyopewa na Mchungaji wa Kanisa la Ngurumo ya Upako, Nabii Geor Davie wa Kasongo jijini Arusha
Wakati hilo likifanyika, mchungaji huyo amedai kuwa kitendo cha gari alilotoa kama zawadi kuchomwa moto kimemfanya ajue ni kwa kiasi gani watu wanampenda kutokana na jumbe mbalimbali alizotumiwa hadi na watu ambao hakuwadhania.
Kipande cha video ya kuchomwa gari hiyo kilichosambaa Januari 25, 2025 kiliambatana na chapisho la mahojiano aliyoyaweka katika akaunti yake ya mtandao wa youtube akisimulia vitu mbalimbali alivyokutana navyo kabla ya kufikia uamuzi huu.
Akielezea namna alivyopewa gari, Gozbert amesema hakuwahi kufahamiana na mtumishi huyo wala kuwa na mazungumzo naye hadi siku aliyompa gari, na uwepo wake katika kanisa hilo ilikuwa ni mwaliko kama waimbaji wengine wanavyoitwa kuhudumu sehemu tofauti.
“Sikuwahi kumfahamu kabla, nilikuwa nimeenda na ilikuwa ni ‘surprise’ ya gari palepale, kupewa gari ilikuwa ni kitu ambacho kiliwashtua wengi, mimi pia ila sikuwa naona kama ina ubaya kwani hata Yesu alipozaliwa Mamajusi walimpelekea zawadi,” amesema Gozbert.
Amesema baada ya kupewa gari hiyo aina ya Mercedes Benz, alibadilisha rangi kutoka ‘silver’ (shaba) kuwa nyeusi, akabadilisha mwonekano wa mbele huku akifafanua kuwa mchungaji huyo pia alimuunganisha na watu ambao wangeweza kumsaidia kubadilisha umiliki na alifanya hivyo.
“Niliibadili umiliki na ilikuwa yangu kabisa, niliiendesha sana kiasi ambacho niliichoka, mimi si mpenzi wa kuendesha gari, ila hiyo gari niliendesha hadi nikachoka kuiendesha, ikabaki uendeshaji wa kawaida, leo nitatoka na gari hii kesho nitatoka na hii,” amesema Gozbert.
Amesema baada ya muda kupita akiwa katika maombi alidai kuwa Mungu alimsemesha na kumuambia asiendeshe gari hiyo, lakini alikuwa akipuuza kwa kuendesha ndipo sauti hiyo aliisikia tena akikatazwa.
Hali hiyo ilimfanya yeye kuigesha gari hiyo kwa muda na siku moja rafiki yake ambaye hakumtaja jina alikuwa na harusi alipoombwa gari alimpatia na aliporudisha kwa mujibu wake alisikia tena sauti ya Mungu ikimuambia, maelekezo ya kutoendesha gari hiyo si yake pekee bali hata kumpa mtu mwingine aendeshe haitakiwi.
“Baada ya maelekezo hayo nilisema Mungu hiki ndiyo ulichokisema nitatii,” amesema Gozbert na kuongeza “Lakini pamoja na katazo hili nilikuwa nikiiwasha gari na kuzima ili kutunza injini isife huku nikiamini kuwa huenda Mungu atakuja kunipa maelekezo mengine, vipi akiniambia niendeshe na injini iwe imekufa itanigharimu hela nyingi kuitengeneza.
Amesema baada ya kukatazwa kuendesha gari hiyo ilianza kutangazwa kuwa amefariki dunia mara tatu mfululizo, huku akitafsiri kuwa ni kipindi ambacho Mungu aliamua kumficha na hapo ndipo watu waliokuwa wanamdai hawamdai na anao wadai hawamlipi.
Amesema Mungu anayemtumikia ana wivu na hataki utukufu wake uchukuliwe na mtu yeyote, asije kumuinua halafu mtu mwingine aje kusema alitabiri kuwa atainuka.
“Asije mtu mwingine yeyote akasema wamempa nguvu za giza ndiyo maana ameinuka, hapana anataka utukufu wake peke yake, kuwa mimi Mungu ndiye niliyekuinua, kukupa uzima, kuponya na acha kuendesha hii gari kwa sababu waliokuwa wanaitafuta roho yako ni huyu na huyu na akanifunulia,”amedai Gozbert.
Amesema watu hao walizika jina na lengo lao ilikuwa ni kutoa uhai bila kujua kuwa amebeba kusudi la Mungu.
Akiwa katika ibada za kila siku katika kanisa lake la Ngurumo ya Upako, mchungaji huyo amesema awali hakuwa anajua kilichotokea lakini wingi wa ujumbe aliokuwa akitumiwa na watu mbalimbali ndiyo ulimshtua.
Amesema jambo hilo limetokea ili ajue upendo ambao watu wako nao juu yake kwani baada ya tukio hilo alipigiwa simu na kutumiwa jumbe na watu mbalimbali hadi kutoka kwa ambao hakuwafikiria kabisa.
“Kiukweli nimeona upendo kupitia jumbe mbalimbali. Binafsi niwashukuru Watanzania wote wa ngazi mbalimbali na viongozi kwa upendo mlionionyesha, au nitumie neno ambalo alilowahi kusema Lowassa (Hayati Edward Lowassa) ni mahaba makubwa sana ambayo yameonekana,” amesema.
Amesema jambo hilo limemfanya kugundua kuwa pamoja na tofauti zilizopo watu ni wamoja na likitokea tatizo wote wanasimama pamoja huku akitaka mshikamo huo na umoja udumu Tanzania, kanisa na raia wote.
Akizungumzia sakata la kuchomwa moto gari kisheria, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga na mwanasheria, Julius Mtatiro amesema Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (The Penal Code) Kifungu cha 319 kinakataza uchomaji wa mali kwa makusudi, ambapo mtu yeyote ambaye kwa kunuwia na isivyokuwa halali anatia moto katika jengo lolote au chombo chochote kikiwa kimekamilika au lah ataadhibiwa.
Pia kifungu hicho kinazungumzia adhabu ambayo mtu atapewa ikiwa atachoma kiwanda cha machimbo au matengenezo au zana za machimbo ya madini atakuwa anatenda kosa na atawajibika kwa adhabu ya kifungo cha maisha.
“Pia kifungu cha 320, kinasema kujaribu kuchoma mali. Mtu yeyote ambaye anajaribu isivyokuwa halali kuwasha moto kitu chochote kilichorejewa katika kifungu cha 319, au kunuwia na isivyokuwa halali anatia moto kwenye kitu chochote ambacho kipo karibu na kitu chochote ambacho kimerejewa katika kifungu cha 319 na kuna uwezekano wa kushika moto kutoka hapo, atakuwa anatenda kosa na atawajibika kwa adhabu ya kifungo cha miaka 14,” amesema Mtatiro.
Mbali na mali pia Kifungu cha 321 kinakataza mtu kutia moto katika mazao na mimea iotayo ikiwemo mazao ya mavuno ya ukulima yawe mitini, yamechumwa au yamekatwa au mazao ya nyasi za kulisha wanyama zilizolimwa ziwe za kuota zenyewe.
Pia kifungu hicho kinakataza kutia moto mazao ya asili ya ardhi hiyo au sivyo, ziwe zimesimama au zimekatwa na kufanya hivyo itakuwa ni kutenda kosa na atawajibika kwa adhabu ya kifungo cha miaka 14.
Lakini mbali na uharibifu wa mali, Wakili Dominic Ndunguru amesema kitendo cha kuchoma moto gari pia ni kinyume na sheria za mazingira ambayo inatoa miongozo juu ya uteketezaji wa vitu mbalimbali ikiwemo taka ngumu, plastiki na betri.
“Hili linafanyika ili kulinda mazingira ili kuendelea kupunguza athari zinazoweza kuchochea mabadiliko ya tabianchi.”
“Unapochoma ile gari ina mafuta, matairi yakiungua moshi unaongeza hewa ya ukaa, kama ni betri inatengenezwa kwa kemikali mbalimbali vipi ikichuruzika kwenda kwenye vyanzo vya maji kama vipo karibu inaleta athari gani kwa viumbe hai, kama baharini itaua samaki,” amesema Ndunguru.
Amesema ili kulinda mazingira, ni vyema watu kuzingatia njia mbalimbali za uteketezaji taka ngumu zilizowekwa. “Kuna viwanda vya kusaga chuma msanii huyo angeweza kutumia njia hiyo kuteketeza hilo gari,”amesema.