Dar es Salaam. Pengine usipate fursa ya kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati, lakini nawe ni miongoni mwa wanufaika.
Hoja hiyo inajibu mitazamo ya wananchi kadhaa, ambao aghalabu wahoji wananufaikaje na mikutano mikuu ya nchi, ikiwa wao si sehemu ya washiriki.
Kwa mujibu wa wanazuoni wa uchumi, kila huduma itakayotumiwa na wageni watakaowasili nchini, kuna mnyororo wa faida inayomgusa kila mwananchi.
Hatua ya wageni kulala kwenye hoteli za Tanzania, kununua chakula kwa wauzaji wa Tanzania na viburudisho vingine, kutembelea hifadhi, kutumia usafiri na vitu vingine faida yake inawagusa wananchi wote, kwa mujibu wa wachumi hao.
Wamekwenda mbali zaidi na kufafanua, methali ya ujio wa wageni hao, utaitangaza Tanzania na fursa zake, hivyo kurahisisha kupatikana kwa wawekezaji na hatimaye kuzalisha ajira.
Hoja hizo zinakuja ikiwa ni siku moja imesalia kabla ya kufanyika kwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati unaolenga kuongeza uunganishaji nishati kwa Waafrika milioni 300 ifikapo mwaka 2030.
Mkutano huo unatarajia kuwakutanisha zaidi ya wakuu wa nchi 25 kutoka Afrika, utafanyika katika Kituo cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.
Tayari Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameshatoa salamu za ukaribisho kwa Marais wa Mataifa ya Afrika na wageni mbalimbali watakaohudhuria mkutano huo.
Akizungumzia faida kwa wananchi, Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Hamis Mwinyimvua anasema kwa kuwa kuna mnyororo wa matumizi kuna maslahi ya kiuchumi kwa nchi.
Anaeleza maslahi hayo yatatokana na kadri wageni watakavyonunua vitu mbalimbali watakapokuwa nchini.
Kwa mujibu wa Dk Mwinyimvua, wageni hao watakula, watalala na kwenda kupata burudani, huduma ambazo kimsingi hazitapatikana bure.
Anasema kadri wageni watakavyolipia huduma hizo na ndizo watakavyowanufaisha watoa huduma husika.
“Watoa huduma hizo ni watanzania kwa hiyo mwananchi atanufaika moja kwa moja na ugeni huo,” anasema.
Ukiachana na wanaotoa huduma, anasema zinakopatikana huduma hizo wameajiriwa wananchi, hivyo nao watanufaika.
Anakwenda mbali zaidi na kueleza walioajiriwa nao wana ndugu wanaowategemea, hivyo wote watanufaika.
“Manufaa ni mnyororo, inawezekana mwananchi asiwaone wageni, lakini akajikuta ananufaika kwa namna fulani,” anasisitiza.
Dk Mwinyimvua anasema kwa sababu ugeni huo utahitaji huduma ambazo lazima zilipiwe Kodi, Serikali nayo itanufaika na hatimaye manufaa yatakwenda kwa wananchi moja kwa moja.
Mwanazuoni mwingine wa uchumi na masuala ya kodi, Dk Balozi Morwa anasema mapato ya kikodi ndiyo turufu ya mwananchi kawaida kutokana na mkutano huo.
Anaeleza katika mkutano huo, watakutana wakuu wa nchi na taasisi mbalimbali ambazo kwa namna moja au nyingine zitavutiwa kuwekeza nchini.
Kwa mujibu wa Dk Morwa, isingekuwa rahisi kwa wawekezaji hao kuja Tanzania iwapo kusingelikuwa na mkutano huo.
Iwapo wawekezaji watapatikana, anasema watazalisha ajira na kulipa Kodi, yote hayo yana maslahi kwa wananchi wa kawaida.
Lakini, hatua ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo, anasema kunaipa fursa nchi ya kutangaza rasilimali za nishati ilizonazo, yakiwemo madini ya Uranium.
“Ni fursa nzuri kwa Tanzania kutangaza rasilimali ilizonazo katika sekta ya nishati kama kuwepo kwa madini ya Uranium,” anasema.
Anasema mwananchi wa kawaida atanufaika iwapo wawekezaji watapatikana na hatimaye kuanza kulipa kodi itakayowezesha utekelezwaji wa huduma mbalimbali.
Maandalizi ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi kuhusu nishati yakamilika, Marais 25 kuhudhuria-Balozi Kombo.
Akizungumzia maandalizi ya mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Kombo, anasema maandalizi ya mkutano huo yamekamilika.
Anasema zaidi ya marais 25, Mawaziri