Arusha. Mahakama ya Rufani imebariki adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela, aliyohukumiwa aliyekuwa mfanyakazi wa ndani wa kiume (house boy) Emmanuel Mdio, kwa kosa la kumlawiti mtoto wa kiume wa mwajiri wake, aliyekuwa na umri wa miaka minane.
Hii ni rufaa yake ya pili kukwaa kisiki awali alihukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Moshi, baada ya kutiwa hatiani na mahakama hiyo ambapo alikata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, iliyogonga mwamba na kuridhia hukumu ya awali.
Mahakama ya rufani ilitupilia mbali rufaa hiyo baada ya kuona haina mashiko na adhabu iliyotolewa ilikuwa sahihi hivyo kujiridhisha upande wa mashitaka umethibitisha kosa hilo bila kuacha shaka yoyote.
Rufaa hiyo ya jinai namba 31 ya mwaka 2022, ilisikilizwa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani ambao ni Barke Sehel, Patricia Fikirini na Lameck Mlacha walitoa hukumu hiyo Januari 20,2025 katika kikao chake kilichoketi Moshi.
Katika kesi ya msingi, Emmanuel alishtakiwa kwa kosa la ulawiti kinyume na kifungu cha 154 (1) cha Kanuni ya Adhabu.
Ilidaiwa katika tarehe na mwezi usiojulikana mwaka 2018,eneo la Shirimatunda Bonite ndani ya Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, mrufani alikuwa akimlawiti mtoto huyo ambaye katika kesi hiyo alijulikana kama shahidi wa pili.
Shahidi wa tatu ambaye ni Mwalimu wa afya katika Shule ya Msingi Shirimatunda, aliyokuwa akisoma mwanafunzi huyo, alibaini mwanafunzi huyo hatembei sawasawa.
Shahidi huyo alidai baada ya kumuhoji, mwanafunzi huyo aliyekuwa akisoma darasa la pili alimweleza kuwa msaidizi huyo wa nyumbani alikuwa akimlawiti na walikuwa wakiishi nyumba moja (kwa bibi wa mwathirika huyo), ndipo akaripoti suala hilo kituo cha polisi.
Shahidi huyo wa pili, katika ushahidi wake alidai Jumapili moja asubuhi, Emmanuel aliingia chumbani kwake akiwa ameshika keki na kinywaji, ambapo alienda moja kwa moja kwake (akiwa amelala kwenye godoro lililokuwa sakafuni).
Alidai mahakamani hapo kuwa Emmanuel alimvua nguo na kumlawiti na alipomaliza alimpa keki na kinywaji hicho, huku akimuonya asimueleze mtu yoyote la sivyo atamuua kwa nyundo.
Shahidi wa nne ambaye ni daktari katika Hospitali ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi ambaye ndiye alimchungunza mtoto huyo, Dk Victor Adolf, alieleza kuwa aliona michubuko kwenye sehemu ya haja kubwa ya mwathirika huyo, michubuko iliyosababishwa na kupenya kwa kitu butu.
Katika utetezi wake, Emmanuel alikana kuhusika na tukio hilo na kudai kesi hiyo ilitengenezwa dhidi yake na babu wa mwathirika huyo, baada ya kudai mshahara wake ambao alikuwa hajalipwa kwa miezi sita.
Katika kesi hiyo Mahakama ilimuhukumu Emmanuel baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili na kubaini kuwa upande wa mashitaka umethibitisha kosa hilo bila kuacha shaka.
Katika rufaa ya kwanza, Mahakama Kuu Kanda ya Moshi iliitupilia mbali rufaa na katika rufaa ya pili iliyokuwa ikisikilizwa na Mahakama ya rufani, Emmanuel alikuwa na sababu tatu za rufaa.
Sababu hizo ni Mahakama mbili za chini zilikosea sheria na ukweli kwa kumtia hatiani mrufani huku shitaka likiwa na dosari, sababu ya pili ilikuwa Mahakama hizo zimekosea kisheria kumtia hatiani kwa kutegemea ushahidi wa mashtaka usioaminika na sabbau ya tatu akidai kuwa kesi dhidi yake haikuthibitishwa bila kuacha shaka yoyote.
Wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo, Emmanuel aliomba kuongeza sababu nyingine tano ikiwemo Jaji wa Mahakama Kuu aliyesikiliza rufaa ya kwanza alikosea kisheria katika kushikilia hukumu dhidi yake kutokana na ushahidi wa mwathirika licha ya ushahidi huo kuchukuliwa kinyume na kifungu cha 127 (2) cha Sheria ya Ushahidi.
Katika rufaa hiyo Emmanuel hakuwa na uwakilishi wa wakili huku upande wa jamhuri ukiwa na mawakili wawili wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Janeth Sekule.
Jaji Sehel amesema baada ya kupitia mwenendo wa rufaa hiyo na kusikiliza hoja za pande zote mbili, Mahakama mbili za chini zilijiridhisha na kuamini ushahidi wa upande wa mashtaka.
Amesema ushahidi wa mwathirika mwenyewe (shahidi wa pili), alimtaja Emmanuel kama mtu ambaye alikuwa akimlawiti.
Jaji Sehel amesema ushahidi wa mwathirika huyo ulithibitishwa na ushahidi wa daktari (shahidi wa nne) ambaye aliieleza Mahakama kuwa alimchunguza mtoto huyo na kukuta michubuko katika sehemu yake ya haja kubwa iliyosababishwa na kitu butu.
“Kwa kuzingatia kwamba, katika kesi za makosa ya kujamiiana, ushahidi bora unatoka kwa mwathirika, tunaona rufaa haina mashiko na kuitupilia mbali,”alihitimisha Jaji Sehel katika hukumu hiyo ambayo nakala yake inapatikana katika mtandao wa Mahakama.