Kipenseli ajitafuta mapemaa Bara | Mwanaspoti

KIUNGO mshambuliaji wa Mashujaa, Balama Mapinduzi ‘Kipenseli’ amesema ameanza kujitafuta mapema kikosini kabla ya kurejea kwa Ligi Kuu Bara, akipania kutumua duru hilo la pili kuondoa gundu kwa kutofunga wala kuasisti ili amalize msimu kwa heshima.

Nyota huyo wa zamani wa Alliance FC, Yanga na Coastal Union, aliliambia Mwanaspoti, kitendo cha kufunga wala kuwa na asisti hadi sasa kunamkata stimu na hataki msimu uishe bila kuambulia kitu, kitu kinachomfanya akomae mazoezini kwa bidii kipindi cha mapumziko ya ligi ili kumweka fiti.

“Nina kazi kubwa ya kufanya duru la pili, kwani kitu cha kunipa heshima katika nafasi ninayocheza ni kufunga ama kutoa pasi za mwisho ya mabao, ndiyo maana sitaki kutoka kapa msimu huu,” alisema Kipenseli na kuongeza;

“Kuna wachezaji wapya wameongezeka ambao watahitaji kuonyesha kitu kipya, hivyo lazima ushindani utakuwa mkubwa ambao ni faida kwa timu.”

Alisema anatamani mwisho wa msimu jina lake litajwe miongoni mwa wachezaji, ambao huduma zao zilikuwa msaada mkubwa kwa timu.

“Kila mchezaji anatamani atajwe kwa kufanya vitu vikubwa, ila naamini lazima nitafanya kitu cha jina langu kuheshimika, nitapambana kwa kadri niwezavyo,” alisema.

Related Posts