TIMU ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, itajua wapinzani wake itakaokutana nao wakati droo ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), itakapofanyika kesho kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mohammed V uliopo Rabat jijini Morocco.
Stars ni kati ya timu 24 zitakazoshiriki michuano hiyo itakayoanza kutimua vumbi Morocco kuanzia Desemba 21, mwaka huu hadi Januari 18 mwakani, ikiwa ni AFCON ya 35, kufanyika katika historia tangu michuano hiyo ilipoanzishwa mwaka 1957.
Timu 24 zilizofuzu zitapangwa katika vyungu vinne vyenye timu sita kulingana na ubora wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), ambapo Stars iko chungu cha nne na wawakilishi wengine wakiwamo, Msumbiji, Comoro, Zimbabwe, Sudan na Botswana.
Chungu cha kwanza kitakuwa na wenyeji Morocco, Senegal, Misri, Algeria, Nigeria na mabingwa watetezi wa michuano hiyo Ivory Coast, huku kile cha pili kikiwa na timu za Cameroon, Mali, Tunisia, Afrika Kusini, DR Congo na Burkina Faso.
Chungu cha tatu kinaundwa na Gabon, Angola, Zambia, Uganda, Equatorial Guinea na Benin ambapo katika droo hiyo kutakuwa na makundi sita yenye timu nne, huku zitakazomaliza katika nafasi mbili za juu kwa kila kundi zitafuzu moja kwa moja hatua ya 16.
Timu hizo zitaungana na nne zitakazomaliza katika nafasi ya tatu zikiwa na matokeo bora zaidi ili kukamilisha idadi ya timu 16, ambazo zitaanza kushindania taji hilo kubwa Barani Afrika, ambalo litachezwa kwenye viwanja sita vilivyopo katika majiji sita.
Stars ilikata tiketi ya kushiriki michuano hiyo baada ya kumaliza katika nafasi ya pili ya Kundi H ikiwa na pointi 10, nyuma ya DR Congo iliyomaliza na pointi 12, huku Guinea ikishika ya tatu na pointi tisa, wakati Ethiopia ilimaliza na pointi nne.
AFCON ya mwaka huu ni ya nne kwa Stars katika historia yake ambapo mara ya kwanza ilikuwa ya Nigeria mwaka 1980, kisha ikashiriki tena baada ya miaka 39, ilipofanya hivyo mwaka 2019, Misri chini ya kocha mkuu, Mnigeria Emmanuel Amuneke.
Mara ya tatu ilikuwa mwaka 2024 kule Ivory Coast ikiwa na kocha, Adel Amrouche mwenye uraia pacha wa Algeria na Ubelgiji ambapo ilipangwa Kundi F na timu za Morocco, Zambia na DR Congo na kuishia hatua ya makundi na pointi zake mbili tu.
Mwaka huu imefuzu kwa mara ya nne tena ikijiwekea rekodi ya kipekee baada ya kufuzu ikiwa chini ya kocha mzawa, Hemed Suleiman ‘Morocco’, kwani kabla ya hapo haikuwahi kutokea jambo lililomfanya kujitengenezea wasifu mkubwa nchini.
Mastaa watakaohudhuria sherehe za droo hiyo ni Essam El Hadary (Misri), Patrick Mboma (Cameroon), Mohamed Sissoko ‘Momo’ (Mali), Christopher Katongo (Zambia), Aymen Mathlouthi (Tunisia) na Gervais Yao Kouassi ‘Gervinho’ kutokea Ivory Coast, wakati pia ofisa habari wa Yanga, Ali Kamwe atahudhuria.
Michuano hii inarejea tena Morocco kwa mara ya kwanza tangu ilipofanyika mwaka 1988, ambapo Cameroon ndio iliyotwaa taji hilo, huku mwaka 2027, mashindano hayo yatafanyika nchi tatu za Afrika ya Mashariki ambazo ni Tanzania, Kenya na Uganda.