Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Deogratius Mahinyila amesema kauli mbiu ya ‘No reforms, no election’ (Hakuna mabadiliko, hakuna uchaguzi) ni amri ya wananchi walioiweka Serikali madarakani.
Kauli hiyo imekosolewa hivi karibuni na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Stephen Wasira akisema chama hicho kiko tayari kwa mazungumzo ya maridhiano, lakini hakitaki kupewa amri.
Akizungumza na Mwananchi leo Januari 25, 2025 jijini Dar es Salaam, Mahinyila amesema chaguzi za mwaka 2019, 2020 na 2024 zimewapa fundisho kuhusu mfumo wa uchaguzi.
“Nafikiri anayesema ni amri asome ibara ya 8 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayosema msingi wa mamlaka ya nchi hii ni wananchi, kama No reforms no election imekubalika kwa wananchi, hata CCM wanapaswa kuikubali,” amesema.
Amesema kifungu hicho cha katiba kinawapa mamlaka wananchi kusema wanalotaka kwa Serikali waliyoiweka madarakani.
Amesema japo miaka ya nyuma chama hicho kimekuwa kikipata wawakilishi wakiwamo wabunge, madiwani na viongozi wa serikali za mitaa, hiyo haimaanishi kuwa hakukuwa na sheria kandamizi.
“Suala sio kususia uchaguzi je, ukishiriki uchaguzi hao wawakilishi utawapata? Mwaka 2019 uchaguzi wa serikali za mitaa zaidi ya asilimia 98 ya wagombea wetu walikatwa.
“Juzi hapa (Novemba 2024) uchaguzi wa serikali za mitaa, mimi nilikwenda kugombea uenyekiti wa kijiji, nilikatwa wakisema mimi sio mkazi wa kijiji hicho, wakati jina langu lipo kwenye orodha ya wapigakura.
“Kwa hiyo hata tukienda kwenye uchaguzi na kugombea, watatukata tu. Mwaka 2019 na 2020 tumeona, watu ambao hawajui kujaza fomu walikuwa ni Chadema tu. Hayo tuyaingize kwenye maajabu ya dunia,” amesema.
Ameendelea kusema hata kama sheria zilizotumika wakati wakipata wabunge na madiwani, haikumaanisha kuwa zilikuwa nzuri.
“Katika sheria kuna haki zinazoweza kutolewa kwa mkono huu zikachukuliwa kwa mkono wa pili. Kusema tu kwa kuwa tuliwahi kuwa na wabunge wengi miaka ya nyuma haimaanishi kwamba ndio sheria zilikuwa nzuri, tuzichambue sheria zenyewe.
“Hizo nyakati ambazo Chadema ilikuwa inapata wabunge, nchi ilikuwa inaongozwa na nani, upepo wa siasa ulikuwaje?”
Alipoulizwa kama muda uliobaki utatosha kufanya mabadiliko ya sheria wanayoyahitaji kufikia kwenye uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu, Mahinyika amesema kinachotakiwa ni nia.
“Kwanza kwenye mabadiliko yoyote ya siasa ni kutokana na nia tu. Zipo sheria zilizopitishwa kwa muda mfupi, sasa kama ipo nia hakuna linaloshindikana, lakini kama nia haipo hata tukikaa miaka 30 hatutafika huko,” amesema.
Akiwa mwenyekiti mpya, Mahinyila amesema anataka kulifanya baraza hilo kuwa sauti ya Watanzania.
“Awali, Bavicha ilikuwa sauti kuu ya vijana na hata Taifa lilikuwa linasikia, hivyo jambo la kwanza tutakalolifanya na wenzangu ni kuhakikisha vijana wa Chadema tunakuwa sauti ya Watanzania, kuelezea changamoto zinazowakabili,” amesema.
Mbali na kuwaunganisha vijana katika chama hicho, Mahinyila amesema wanataka kuwaunganisha vijana katika vyama vingine kwa ujumla.
“Tatizo la ajira kwa vijana halichagui kijana wa CCM au wa Chadema, ugumu wa maisha hauchagui kijana wa chama fulani ukaacha chama fulani. Chochote tunachoona ni kibaya ni kibaya kote.”
“Kama leo tunakemea uchawa, ni tatizo ukiwa CCM au ukiwa chama kingine, kwa hiyo nafikiri ni sisi kujua changamoto zinatukumba bila kujali tofauti zetu,” amesema.
Akifafanua zaidi changamoto ya ajira, Mahinyila amesema inasababishwa na mfumo mbovu wa elimu usioendana na mahitaji ya soko la ajira.
“Kwa mfano, katika mfumo wa elimu tunapowapeleka vijana shule anasoma fizikia, unampa mkopo, halafu akitoka hapo hana ajira.
“Lakini mataifa mengine wakikupa hela ya Serikali uende shule maana yake wanajua watakupa kazi.”
Amegusia pia suala mitaji na kodi kwa vijana wanaozisha biashara, akisema ni kikwazo.
“Leo kijana kufungua kampuni, angalau uwe na Sh1.5 milioni ili. Halafu akifungua biashara mamlaka za kodi nazo zinataka kodi,” amesema.
Ameendelea kueleza kuwa, anataka baraza hilo liwe la kutoa changamoto ndani ya chama hicho kwa lengo la kukijenga.
“Sitamani tuwe na baraza ambalo tutakaa tu makao makuu, halafu tunaandaa programu ya kwenda kuitekeleza Tandahimba (Mtwara) wakati hatujui vijana wa huko wanawaza nini,” amesema.
Kuhusu uchumi, amesema ameweka mikakati ya kuuimarisha ili kuwapa uhuru.
“Tukiweza kujiamulia mambo yetu, tutakuwa na mawazo huru. Hilo tutalifanya na tumefurahi kusikia mwenyekiti wetu amehamasisha kuwepo kwa mabadiliko ya katiba ya chama.
“Kwa maana kwamba mapato ya chama kuwe na fungu la vijana,” amesema.
Mahinyila alizaliwa Agosti 5, 1995 katika Kijiji cha Berege wilayani Mpwapwa Mkoa wa Dodoma.
Amesoma shule za msingi tofauti wilayani humo kabla ya kujiunga na Shule ya Sekondari Meliwa aliyosoma kidato cha kwanza hadi cha sita.
Anasema alijiunga na shule hiyo ili kuendeleza kipaji cha kucheza mpira wa miguu, lakini hakuendelea tena na ndoto hiyo.
Mwaka 2015 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akichukua shahada ya kwanza ya sheria aliyomaliza mwaka 2019 na kisha akajiunga na Shule ya Sheria (LST) akichukua stashahada ya uzamili ya ya sheria aliyohitimu mwaka 2021.
Alianza kujihusisha na siasa tangu mwaka 2011 alipojiunga na Chadema. Hata hivyo, aliongeza nguvu mwaka 2015 alipokuwa Jeshi la Kujenga Taifa kambi la Mafinga, ambapo aliahirisha mafunzo kwa muda na kwenda kusimamia uchaguzi kabla ya kurudi na kumalizia.
Akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alijiunga na Jumuiya ya Wanafunzi wa Chadema (Chaso) na kugombea na kuwa Makamu Mwenyekiti wa tawi.
Akiwa chuoni hapo, alikuwa pia spika wa bunge la wanafunzi (Daruso).
Mwaka 2020 aligombea udiwani Kata ya Berege, lakini uchaguzi huo ulivurugika, akakamatwa na kushtakiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi, ambapo alikaa rumande magereza ya Mpwampwa na baadaye Isanga mkoani Dodoma.
Hata hivyo, kesi hiyo ilifutwa akiwa ameshapewa dhamana na hata aliporudi uraiani alikuta tayari mgombea wa CCM ameshaapishwa.