Mahinyila: Haikuwa sawa kuwapambanisha Mbowe, Lissu wakati huu

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Deogratius Mahinyila amesema japo chama hicho kimepita salama kwenye uchaguzi wa ndani, lakini haikuwa sawa kuwashindanisha aliyekuwa mwenyekiti Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa sasa, Tundu Lissu.

Amesema mvutano huo ulikiweka chama majaribuni hasa wakati huu ambao nchi inaelekea kwenye uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu.

Katika uchaguzi huo uliofanyika usiku wa kuamkia Januari 22, Lissu alipata kura 513 sawa na asilimia 51.5 akimshinda Mbowe aliyepata kura 482 sawa na asilimia 48.3

Akizungumza na katika mahojiano na Mwananchi jana Januari 25, 2025, Mahinyila amesema kutokana na nguvu walizonazo viongozi hao, haikuwa sawa kuwapambanisha hasa wakati huu.

“Nafikiri na huo ulikuwa ni msimamo wangu, pamoja na kwamba tumemaliza uchaguzi na Mbowe amekubali matokeo, lakini mimi sikuwa naamini kama chama kilikuwa ni sahihi kuwashindanisha Mbowe na Lissu.”

“Chadema sio tu chama cha siasa tu, pia ni chama cha ukombozi, sasa kitendo cha kuwashindanisha miamba wawili wakati ambao tunakwenda kwenye uchaguzi mkuu, haikuwa sawa.

“Kama Mbowe angetoa kauli kwamba haridhishwi na matokeo, yangekuwa mambo mengine, kwa hiyo pamoja na kwamba tumemaliza salama kama kauli yetu ya ‘Stronger Together’ (Nguvu pamoja), lakini nafikiri haikuwa sawa,” amesema. 

Amerejea maneno ya Mbowe kuhusu haja a kuanzisha tume ya usuluhishi, akisema suala hilo ni muhimu kwa ajili ya kujenga chama.

“Kikubwa tunachokifanya ni kuhakikisha tunasawazisha hali iliyotokea, kwa sababu tusipowafanya wenye maumivu ya uchaguzi wapone hatutaendelea mbele,” amesema.  Akiwazungumzia Mbowe na Lissu, amesema ni viongozi wenye mitazamo tofauti iliyokijenga chama.

“Ukikaa na mheshimiwa Mbowe unaweza kujifunza mikakati mbalimbali na ukikaa na mheshimiwa Lissu unachoweza kujifunza ni kujituma na ujasiri wa kusimamia misimamo yake bila kujali matokeo yatakuwaje,” amesema.

Mahinyila aliyetembelea ofisi za Mwananchi Tabata Relini jijini Dar es Salaam, ameeleza pia jinsi ushindani wa Mbowe na Lissu ulivyoyumbisha uchaguzi wa baraza hilo.

Uchaguzi huo uliofanyika Januari 13 na 14, 2025 jijini Dar es Salaam, ambapo Mahinyila alipata ushindi  kwa kura 204 akimshinda mpinzani wake, Masoud Mambo aliyepata kura 112.

“Upepo wa Lissu na Mbowe ulikuwa mkali, hata sisi kwenye Bavicha ilikuwa ili uungwe mkono, inategemea unamuunga mkono nani. Kwa hiyo ilikuwa ni changamoto kubwa.”

“Haikuwa na maana kwamba simuungi mkono Lissu, bali sikutaka ionekane kwamba kumuunga mkono Lissu ndio msingi wa kuchaguliwa kwangu,” amesema.

Hata hivyo, amesema kadiri muda ulivyokuwa unazidi kusonga ndiyo joto nalo lilikuwa linazidi kupatanda

“Uhusiano wangu na Lissu ni kwa sababu tunataka mabadiliko ndani ya chama, mbinu za kufanya siasa, namba ya kubadilisha mambo mbalimbali ndani ya taasisi.

“Kwa sababu ndani ya Bavicha tulikuwa wagombea watatu, tukajikuta wawili tunazungumza lugha moja, nikaona dakika za mwisho tumuunge mkono Lissu,” amesema.

Alipoulizwa kama kuna wakati wafuasi wa Mbowe walimfuata wakitaka awaunge mkono, alikiri ni kweli.

“Wapo watu wa upande wa Mbowe walionifuata wakitaka niwaunge mkono, lakini niliwaambia mimi siungi mkono upande wowote, kama wanataka wanipime basi waangalie maono na misimamo yangu.

“Sio kwamba sikuwa na wasiwasi wa kushindwa, sio katika uwezo wangu, bali kutokana na upepo wa kisiasa, kwa sababu nilishasema namuunga mkono Lissu, nikawa na hofu kwamba pengine naweza kushindwa,” amesema.

Akizungumzia Mbowe, Mahinyika amesema ni kiongozi aliyeweka alama kwa kukijengea misingi chama hicho.

“Tutake au tusitake, hakuna namna historia ya Chadema itaandikwa bila kutajwa jina la mwenyekiti wetu Mbowe, kwa sababu ameshiriki katika kuanzisha chama chetu mwaka 1992 na yeye alikuwa kiongozi wa vijana wakati huo.

“Jambo kubwa alilofanya ni kutengeneza misingi ya Chadema tunayoiona sasa. Kwa sasa tupo wengine tulioendeleza hilo gurudumu,” amesema.

Alipoulizwa kama kuondoka kwa Mbowe kwenye uongozi kutakiathiri chama hicho hasa kifedha, Mahinyila amesema, “Mbowe ataendelea kuwa mjumbe wa kamati kuu kwa mujibu wa katiba yetu, sidhani kwamba alikuwa akitoa fedha kwa sababu alikuwa mwenyekiti wa chama, bali ni kwa mapenzi yake kwa chama.”

Amesema chama hicho kina mikakati ya kutafuta vyanzo vya fedha vitakavyoendelezwa na uongozi mpya.

Related Posts