Malezi ya wazazi yanavyoharibu kesho ya mtoto      

Dar es Salaam. Kwa baadhi ya wazazi na walezi imekuwa kawaida kwao kuwavalisha na kuwapamba watoto katika mitindo ya aina mbalimbali ambayo wakati mwingine inaonekana kuwa juu ya umri wao.

Hapa tunazungumzia mapambo kama makeup inayohusisha vipodozi kadha wa kadha kwenye ngozi ya uso, kubandika nywele za bandia, kope, kucha na wakati mwingine nywele zao kupakwa dawa zenye kemikali.

Hili linakwenda hadi kwenye mavazi, utandawazi umeendelea kuifanya dunia kuwa kama kijiji, watu wanaiga vitu vya kimagharibi, ikiwa ni pamoja na mavazi. Siku hizi si kitu cha ajabu kuona watoto wamevalishwa nusu utupu.

Sambamba na hayo, matumizi ya simu janja kwa watoto zinazowafanya wanaona mambo yasiyofaa kwao, ikiwemo lugha na mienendo ya kikubwa.

Hii inakuja kipindi ambacho kuna aina nyingine ya ukatili wa mitandaoni, ukatili ambao unatishia usalama wa watoto.

Utafiti uliofanywa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalumu unaonesha kuwa watoto 67 katika 100 wenye umri wa miaka 12 – 17 wanatumia bidhaa za mawasiliano, ikiwa pamoja na simu janja, kompyuta (janja) na runinga (janja) zenye intaneti.

Utafiti huo unaonesha watoto wanne katika 100 waliotumia mitandao walifanyiwa aina mojawapo ya ukatili mtandaoni, ikiwemo kulazimishwa kujihusisha na vitendo vya ngono, kusambaza picha na video zenye maudhui ya kingono bila ridhaa yao, na kurubuniwa kujihusisha na shughuli za kingono kwa kuahidiwa fedha au zawadi nyingine.

Pia, utafiti huo umebainisha kuwa simu na vifaa vingine vya kielektroniki wanavyotumia watoto hupatiwa na wazazi na ndugu wa karibu, bila kujua madhara wanayokumbana nayo watoto bila kusimamiwa matumizi yake.

Muda unaotumika zaidi wa vifaa hivyo ni nyakati za usiku, muda unaoongeza madhara zaidi kwa kuwa watumiaji wengi wanashindwa kumudu majukumu ya shughuli za kuanzia asubuhi na siku nzima, hivyo huathiri maendeleo yao shuleni.

Aidha, matumizi yaliyopitiliza yamesababisha uraibu (ulevi) kwa watumiaji ambapo muda mwingi hutumika kwenye mitandao kuliko kazi zenye tija.

Hayo yote yanaweza kumfanya mtoto kukua katika misingi isiyofaa pamoja na kuathiri afya na ukuaji wake.

Licha ya juhudi mbalimbali zinazofanywa na viongozi na taasisi za kidini, wataalamu wa malezi, wadau na taasisi za Serikali na binafsi, wazazi pia wanapaswa kuwa macho ili kuwaepusha watoto kwenye mienendo isiyofaa.

Mathew Sebastian, ambaye ni mzazi anasema  wazazi waelewe kuwa wanajenga kizazi cha kesho. Wawe makini na wanachofanya au wanachoruhusu kwa watoto wao.

“Mawasiliano mazuri baina ya wazazi na watoto ni muhimu. Waeleze kwa nini maadili na staha ni muhimu. Ni vyema kuwaelimisha watoto kuhusu tofauti kati ya umri wao na majukumu ya watu wazima.”

Anasema kwa jumla malezi mazuri ni hazina kwa kila mtoto, na yanahitaji uvumilivu, maelekezo thabiti na maadili mazuri kutoka kwa wazazi.

Akizungumzia upande wake, anasema ameweka mipaka ya wazi, akitolea mfano katu haruhusu mtoto mavazi yasiyofaa au kutumia vipodozi akiwa bado mdogo, huku akiwaelewesha kuwa kila kitu kina wakati wake.

“Nawaonesha mfano bora kwa kuwa kielelezo cha tabia na mtazamo ninaotaka kuona kwao. Pia najitahidi kupata muda wa kutosha kuzungumza nao, ninaongea nao mara kwa mara kuhusu thamani ya kujiheshimu na jinsi ya kufanya maamuzi mazuri maishani,” anasema Sebastian.

Anasema simu na vifaa vingine vya teknolojia hutolewa kwa uwajibikaji.

“Ninaangalia muda wanaotumia mtandaoni na kuhakikisha wanapata maudhui yanayowafaa.

“Nne, ninaweka sheria kuhusu teknolojia. Pia hapo naangalia tabia za marafiki zao. Kwa kifupi, naamini kuwa jukumu langu ni kuwalea watoto kwa misingi ya staha na heshima, nikizingatia kuwa mimi ni kiongozi wao wa kwanza maishani. Ninapowabana leo, najua ninalinda kesho yao,” anasisitiza.

Mzazi mwingine, Amina Rajabu (si jina lake halisi) anayekaa na binti yake wa pekee mwenye umri wa miaka minne, anasema amemzoesha kumpamba aendane na wakati kama yeye alivyozoea.

“Dunia imebadilika, sasa hivi mambo ya urembo haya mawigi, kuvaa suruali, kaptura ni kawaida kwa mtoto wa kike. Cha msingi namsimamia asije kuharibika akapoteza heshima na maadili, ila suala la mavazi ni kawaida tumezoea,” anasema.

Akizungumza kwa upande wake, Rashid Mansa anasema mtoto akiwa katika umri mdogo mara nyingi anajifunza kwa kutazama anayoyaona, huku akijaribu kuyafanya na yeye.

Anasema mzazi ana wajibu wa kumuwekea ukomo mtoto wake katika matumizi ya mitandao, mavazi hadi pale atakapokuwa na umri wa miaka 18.

“Kwa hatua tuliyofikia, ni ngumu kuwa na malezi ya aina moja kwa watu wote kwa kuwa uhuru wa mitandao na maisha ya kawaida ya nje mtoto anayoyaona inamfanya ajifunze hata nje ya nyumba anayoishi, wazazi wanapaswa kuwa macho katika hili,” anashauri Mansa.

Akizungumza na Mwananchi, Mtaalamu wa Saikolojia, Dk Neema Mwankina anasema watoto wanachokipata ni tabia ambayo inapandwa kutoka kwa wazazi wao.

Anasema mzazi anaipanda tabia kwa mtoto wake, hivyo pale unavyomvalisha mavazi ya namna hiyo anapandikiza mazoea.

“Unavyopandikiza madhara yake unakuja kuyaona, wakati anakuwa mtu mzima atakuwa anavaa mavazi yasiyo na staha, anakuwa kama msanii. Unavyomvalisha tangu mtoto akiwa mkubwa anakuwa hivyohivyo, kuonesha mapaja na vifua kwake kawaida,” anasema.

Anasema mzazi anaweza kuona ni usasa, wakati akiwa mkubwa akitaka kumrekebisha inakuwa ngumu kwa kuwa ameshazoea.

“Wazazi tunachangia maisha ya watoto kuwa na tabia za tofauti, elimu itolewe kwa wazazi na walezi, kwani sasa hivi baadhi yao wanalea kwa kuiga, tofauti na zamani walikuwa wanafuata misingi iliyo bora,” anasema Dk Mwankina.

Anaenda mbali zaidi na kusema siku hizi wazazi wanawalea watoto kwa kuwadekeza kama mayai, jambo ambalo linachangia kumomonyoka kwa maadili, kwa kuwapa watoto uhuru wa kupitiliza.

“Wakati mwingine inafikia mzazi unakuwa mtumwa wa mtoto wako, anaweza akakutuma hata kikombe, akimaliza kunywa chai anataka utoe, mambo ambayo zamani hayakuwepo.

Haya ni matokeo ya watoto kujifunza tamaduni zisizofaa, anachokiangalia kwenye runinga wakati wote ni tamthiliya inayomuonesha mtoto akipambana na wazazi wake, akiwajibu vibaya au hata kuvunja vitu pale anapokasirishwa, unafikiri hapo atajifunza nini,” anasema.

Anasema inashangaza watoto wanawatuma mama zao kwa maana ya kwamba wamekuwa jeuri, akisema kizazi hiki kinalea watoto katika njia isiyokuwa njema

“Tutakuwa na kizazi ambacho hakieleweki, watoto watakuwa hawajielewi kabisa, maisha yatakuwa magumu kuanzia upande wa maadili kuliko tunavyofikiria,” anasema.

Mwanasaikolojia Prisca Sao anasema mtoto abaki kuwa mtoto na mtu mzima abaki kuwa mtu mzima. Kitendo cha kuzoeshwa mtindo wa kikubwa wa mavazi na urembo kinamfanya azoee aone kawaida.

Anasema inamtengenezea akilini mwake awaze namna watu wanavyomuona. Inamtengenezea awaze bila urembo wa kiutu uzima hajakamilika.

“Wazazi na walezi wakumbuke mila na desturi zinapaswa kutunzwa, mtoto avae kwa namna ya kusitiri mwili wake. Mtoto akivaa kwa kuacha viungo vyake nje inasababisha  hata watu wenye nia ovu kumfanyia ukatili.

“Kwanza viungo vyao havijakomaa, wanavyowapaka make up, mawigi, kucha sijui kope inawaharibu watoto. Watoto wanapaswa kuwa watoto,” anasema Sao.

Mkazi wa Dodoma, Annastazia Malecela anasema ilikuwa ni makosa makubwa mtoto kuvaa mavazi yasiyo na heshima katika kipindi ambacho anakua.

Anasema katika karne ya 20 ambayo kizazi chake ndiyo kilikuwa kipo, wazazi wao walikuwa wakiwabana wasije kuacha maadili ya Kiafrika.

“Tulikuwa tukiadhibiwa, mfano usipomsalimia jirani, ukifanya kosa lolote nje ya nyumba akija mtu mzima kuwaambia wazazi unaadhibiwa vikali, sembuse uvae vibaya?

“Hata wanangu niliwakuza katika misingi hiyo, sawa hatukuwa na hayo mambo kama mawigi, kucha na kope za bandia kama sasa, lakini watoto walivaa kiheshima na walikua katika misingi hiyo,” anasema.

Anasema maisha ya sasa kuna utandawazi na watoto mbali na anapoishi, anaona mengi nje ambayo anaweza kuiga. Anachoshauri watoto wanapaswa kubanwa wasipewe uhuru, kwani itawaletea shida katika ukuaji wao.

Anasema kuna mipaka ya malezi mzazi hapaswi kuvuka, kwani mtoto anapaswa kubakia mtoto hadi pale atakapokuwa mkubwa ndipo atayafanya yale ambayo anapaswa kufanya akiwa na mkubwa.

Dk Fabian Maricha anasema kimsingi watoto wanaoweza kupata matatizo ni wale wanaotumia baadhi ya bidhaa zisizoruhusiwa kutumiwa na kundi hilo, ambapo wanatumia pasipo kujua au mwongozo kutoka kwa wazazi au walezi wao kukosa uelewa.

“Kwa wale waliopambwa na wazazi wao na wanafanya hivyo mara kwa mara, mfano kwa baadhi ya mafuta au vipodozi vyenye madhara kwa watoto vinaweza kuwa vimewekewa muda maalumu wa matumizi kama wiki mbili, hivyo ikiwa ni kinyume na hapo inaweza kuleta shida,” anasema Dk Maricha.

Anasema hata hivyo kimsingi hakuna sana madhara kibaolojia, ingawa tatizo linakuja zaidi kwenye upande wa saikolojia na tabia, kwani mtoto anaweza kubadilika na kufanya mambo yasiyo ya umri wake kwa kujihisi ni mtu mzima.

“Ama inawezekana akawa na mzio na hii si mtoto pekee, bali hata watu wazima anaweza akapata changamoto pale anapotumia kipodozi asichoendana nacho,” anasema

Related Posts