KOCHA mpya wa Stand United ‘Chama la Wana’, Juma Masoud amesema licha ya kukabidhiwa timu hiyo wakati huu wa michezo ya mwisho wa msimu hana presha, huku malengo yake makubwa ni kuweka rekodi ya kuipandisha Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao.
Kocha huyo wa zamani wa FGA Talents kwa sasa Fountain Gate, amejiunga na kikosi hicho akisaidiana na Feisal Hau, ambapo amejiunga nayo kwa mkataba wa miezi sita, akichukua nafasi ya Meja Mstaafu, Abdul Mingange aliyejiunga na Songea United.
“Nimekuwa mzoefu kwa muda mrefu na hata nilipopewa hii nafasi sikuona tatizo, lengo letu ni kupambana sana ili tutimize malengo hayo, nataka kuandika rekodi yangu mpya binafsi kwa sababu sijawahi kuipandisha timu yoyote kucheza Ligi Kuu Bara,” alisema.
Masoud alisema licha ya wachezaji wengi kusajiliwa bila ya mapendekezo yake ameridhishwa kwa kiasi kikubwa na uwezo wao, huku akiweka wazi uzoefu na ushirikiano anaoupata kutoka kwa wachezaji na viongozi utatimiza malengo waliyojiwekea.
Kabla ya mchezo wa jana dhidi ya Kiluvya United, timu hiyo imecheza michezo 15, ikishinda tisa, sare miwili na kupoteza minne, ikiwa katika nafasi ya nne na pointi zake 29, huku Masoud akiipambania kuirejesha kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kushuka msimu wa 2018-2019.