Mbwembwe za Rais wa Bukina Faso kuwa kivutio Tanzania

Dar es Salaam. Rais wa mpito wa Bukina Faso, Kapteni Ibrahim Traore ambaye amekuwa kivutio kwa utaratibu wake wa kuvaa kombati za jeshi pamoja na kutembea na bastola kiunoni tofauti na marais wengine, ni miongoni mwa marais 25, watakaohudhuria mkutano wa kimataifa kuhusu nishati Afrika.

Kapteni Traore mwenye umri mdogo wa miaka 34 kuliko marais wote Afrika, amepata umaarufu kwa namna anavyovaa sawa na walinzi wake wanajeshi, lakini kitu cha kipekee ni Rais anayetembea na silaha kiunoni.

Mbwembwe za Kapteni Traore, mtindo wa ulinzi wake zinawakumbusha baadhi ya watu kwa aliyekuwa kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi, aliyepata umaarufu kwa walinzi wake wa kike waliokuwa wakijulikana kwa majina kama ‘walinzi wa Amazon’, au ‘watawa wa kimapinduzi’ au ‘watawa wa kijani.’

Gaddafi mbali na kulindwa na walinzi wanajeshi wa kike takriban 40, pia kila aliposafiri nje ya Libya alibeba hema alilotumia kama makazi yake badala ya kuishi kwenye hoteli kama marais wengine.

Tofauti ni kwamba Gaddafi hakuonekana akibeba silaha, ilhali Kapteni Traore anaonekana akitembea na bastola kiunoni.

Kwenye mitandao ya kijamii, Watanzania wengi wameonyesha shauku ya kumuona Kapteni Traore ambaye umaarufu wake umechangiwa pia na msimamo wa kipekee kuhusu viongozi wenzake wa Afrika.

Mwaka 2024 alipokuwa kwenye mkutano wa Urusi na Afrika kuhusu chakula, aliwakosoa viongozi wa Kiafrika kwa kufuata nyayo za mataifa ya Magharibi bila kujali masilahi ya wananchi wao.

“Tatizo ni kuona wakuu wa nchi za Kiafrika wakiimba wimbo sawa na mabeberu, huku wakitaja sisi ni watu tusioheshimu haki za binadamu,” alisema.

Pia, alionyesha kutokupendezwa na tabia ya baadhi ya viongozi wa Afrika kupenda misaada ya mataifa tajiri badala ya kutengeneza mikakati ya kujitegemea.

Katika mkutano huo, Kapteni Traore alijitokeza akiwa amevaa mavazi ya kijeshi ya kivita, kofia nyekundu, glovu mikononi na bastola kiunoni, tofauti kabisa na marais wenzake waliokuwa wamevalia suti rasmi.

Mwonekano na msimamo wake wa kipekee umemfanya kuwa mmoja wa viongozi wanaovutia zaidi macho ya wengi barani Afrika na duniani kwa jumla. 

Viongozi waungana kuhusu nishati Afrika

Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayeshughulikia masuala ya nishati na mabadiliko ya hali ya hewa, Dk Kevin Kariuki, akizungumzia mkutano huo unaanza kesho Jumatatu Januari 27-28, 2025 amesema utahudhuriwa na marais 25 pamoja na mawaziri wa fedha na nishati 60 kutoka nchi za Afrika.

Kwa mujibu wa Dk Kariuki, mkutano huo wa siku mbili, unalenga kufanikisha hatua ya kusaini Mpango Mahususi wa Nishati wa Afrika.

Awamu ya kwanza ya mpango huo itazihusisha nchi 14 ambazo ni Tanzania, Malawi, Chad, Nigeria, Burkina Faso, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Niger, Liberia, Msumbiji, Madagascar, Zambia, Mali, Ivory Coast, na Mauritania. 

Mpango huo unadhaminiwa na Benki ya Dunia, AfDB, pamoja na washirika wengine wa maendeleo kwa lengo la kuhakikisha watu milioni 300 barani Afrika wanapata huduma ya umeme ifikapo mwaka 2030.

Dk Kariuki ameeleza kuwa, mkutano huu ni wa kipekee unawaleta pamoja wakuu wa nchi na viongozi wengine wakuu wa Afrika kujadili masuala ya nishati.

Mkutano huo utahitimishwa kwa kusainiwa kwa Azimio la Dar es Salaam, litakaloweka msingi wa utekelezaji wa maazimio yaliyojadiliwa.

“Hadi sasa, marais zaidi ya 25 na mawaziri wa fedha na nishati zaidi ya 60 wa Afrika wanakutana hapa.

“Tunatarajia kuona makubaliano na kusainiwa kwa mkataba utakaowezesha lengo la kusambaza umeme kwa watu milioni 300 kabla ya mwaka 2030 kufikiwa,” amesema Dk Kariuki.

Dk Kariuki amebainisha Benki ya Dunia na AfDB walikubaliana Aprili mwaka jana kwamba, hali ya ukosefu wa umeme Afrika haiwezi kuachwa iendelee.

Kufuatia makubaliano hayo, nguzo kuu tano za mpango huu zilizobuniwa ni kuongeza uzalishaji wa nishati, kuwekeza katika miundombinu inayohakikisha uzalishaji wa umeme wa gharama nafuu.

Zingine ni kuimarisha ushindani na kuwezesha mazingira mazuri ya uwekezaji kupitia miundombinu bora.

Nguzo zingine ni miradi ya muunganiko wa mataifa kwa kuanzisha miradi ya ushirikiano kati ya nchi ili kupunguza gharama za usafirishaji wa umeme.

Kuboresha ufikiaji kwa kuimarisha mifumo ya usambazaji kwa kuzingatia maeneo yenye upungufu mkubwa wa nishati.

Pia, kujali maendeleo endelevu kwa kuwekeza katika nishatisafi na salama inayozingatia mabadiliko ya hali ya hewa.

Related Posts