Dar es Salaam. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imezindua Mfumo Jumuishi wa Forodha Tanzania (Tancis) ulioboreshwa, ambao unatajwa kuwa tiba ya matatizo yote ya kiforodha kwenye uondoshaji shehena bandarini, mipakani na kwenye viwanja vya ndege
Mfumo huo ambao umeboreshwa unaziunganisha taasisi 36 ukilenga kuboresha ufanisi, kuhakikisha usahihi wa data na kupunguza ucheleweshaji wa shughuli za forodha.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya siku ya kimataifa ya forodha, leo Januari 26, 2025, iliyoongozwa na kaulimbiu isemayo: “Forodha itatekeleza dhamira yake ya usalama na ustawi”, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda amesema maboresho hayo yanakwenda kuongeza ufanisi wa shughuli za forodha.
Amesema, mfumo huo unapunguza muda wa kuondosha mizigo bandarini, jambo ambalo litasababisha biashara kufanyika kwa haraka na kuimarisha uchumi wa mtu mmojammoja.
“Mfumo huu mpya pia unafanya kazi kwa kutumia akili bandia, una usahihi wa data na unafanya kazi kwa uwazi zaidi, huku ukiendelea kuboreshwa,” amesema.
Mwenda amesema mfumo huo ulioboreshwa ulianza kufanya kazi Januari 20, 2025.
“Ulikabiliwa na changamoto ndogondogo wakati tunaanza kutokana na kuwa mpya, hata hivyo hadi kufikia Februari Mosi changamoto zote zitakuwa zimetatuliwa.”
Amesisitiza mfumo huo mpya utapunguza kwa kiasi kikubwa muda wa uingizaji na utoaji bidhaa sanjari na gharama zisizo za lazima.
Akiuzungumzia mfumo huo, Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania, (Taffa), Edward Urio amesema matumaini yao kuhusu kuimarishwa kwa Tancis, na kusifu uwezo wake wa kuboresha ufanisi na uwazi katika ukusanyaji wa mapato.
“Tunaamini mfumo huo utaongeza uwazi na ufanisi unakwenda kuwa tiba ya matatizo yote ya kiforodha kwenye uondoshaji shehena bandarini, mipakani na kwenye viwanja vya ndege,” amesema
Hata hivyo, alikiri kuwa baadhi ya wanachama wamekumbana na changamoto, kama vile gharama za ziada kutokana na uhifadhi na ucheleweshaji wa usafirishaji wakati wa awamu ya kupitishwa kwa mfumo, jambo ambalo anaamini TRA italishughulikia.
“Tunatumai kamishna mkuu wa TRA ataingilia kati kutafuta suluhu za kirafiki ili kupunguza changamoto hizi huku maboresho yakiendelea,” ameongeza.
Kamishna wa Forodha, Juma Bakari amesema mfumo mpya wa kusafisha bidhaa umeimarika zaidi ya ule wa awali ulioanzishwa mwaka 2014.
“Huu mpya unajumuisha mahitaji mapya ya biashara na kuendana na teknolojia.”
“Unarahisisha uendeshaji wa biashara hasa katika uingizaji na utoaji wa bidhaa,” amesema.
Amebainisha kuwa inaunganisha taasisi 36 zinazoweza kuutumia, na hivyo kuimarisha mawasiliano kati yao.