MFUMO ULIOBORESHWA WA TANCIS KUBORESHA TARATIBU ZA FORODHA NCHINI.

Na Karama Kenyunko Michuzi Tv

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema mfumo mpya wa Tanzania Customs Integrated System (TANCIS) utarahisisha uingizwaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi na kuingia ndani kwa haraka, jambo litakalosaidia kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na watafanyakazi mchana na usiku.

Mfumo huo uliozinduliwa hivi karibuni umebuniwa kuboresha ufanisi, kuhakikisha usahihi, na kupunguza ucheleweshaji katika shughuli za forodha.

Akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Forodha Januari 26, 2025, yenye kaulimbiu “Forodha itatimiza ahadi yake ya usalama na ustawi”, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda alieleza maboresho makubwa yaliyofanywa kwenye mfumo huo.

“Mfumo mpya wa TANCIS unatumia teknolojia ya akili bandia kwa ajili ya uchakataji wa data kwa usahihi, uwazi zaidi, na urahisi wa operesheni,” alisema. “TRA tumejipanga kuboresha mifumo yetu na taratibu kwa kutumia teknolojia ya kisasa kuboresha shughuli za forodha.”

Amesema mfumo ulioboreshwa, ambao ulianza kufanya kazi rasmi Januari 20, 2025, umekumbana na changamoto ndogo wakati wa uzinduzi wake wa awali. Hata hivyo, Kamishna Mkuu General alihakikishia wadau kuwa mafundi wanashughulikia changamoto hizo kwa bidii.

“Tunatambua umuhimu wa ufanisi, usalama, na ustawi kwa taifa letu, na tunashirikiana na wadau muhimu kuhakikisha mafanikio,” alisema.

Alisisitiza kuwa mfumo mpya utapunguza kwa kiasi kikubwa ucheleweshaji wa ukaguzi wa mizigo na gharama zisizo za lazima, hivyo kuboresha ufanisi kwa ujumla.

“Ahadi yangu, pamoja na timu yangu, ni kuwa kuanzia Februari, mfumo huu ulioboreshwa utaanza kufanya kazi kikamilifu na kuwafaidisha watumiaji wote,” alisema, akibainisha kuwa maboresho hayo pia yatahakikisha thamani ya bidhaa inakokotolewa kwa haki na usahihi zaidi.

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA), Edward Urio, ameonyesha matumaini kuhusu mfumo mpya wa TANCIS, akipongeza uwezo wake wa kuboresha ufanisi na uwazi katika ukusanyaji wa mapato.

“Tunaamini mfumo huu utaongeza uwazi na ufanisi,” amesema Urio. Hata hivyo, amekiri kuwa baadhi ya wanachama wamekumbana na changamoto kama vile gharama za ziada kutokana na ucheleweshaji wa kuhifadhi na kusafirisha mizigo wakati wa awamu ya awali ya utekelezaji wa mfumo huo.

“Tunaomba Kamishna Mkuu wa TRA aingilie kati ili kupata suluhisho la kirafiki kupunguza changamoto hizi wakati maboresho yakiendelea,” aliongeza.

Mfumo mpya wa TANCIS ni hatua muhimu katika kuboresha taratibu za forodha nchini Tanzania, kuhakikisha taifa linaendelea kufanikisha malengo yake ya usalama na ustawi.

Kwa upande mwingine, Kamishna wa Forodha, Juma Bakari, amesema kuwa mfumo mpya wa ukaguzi wa bidhaa umeboreshwa zaidi ukilinganisha na ule wa awali uliotumika tangu 2014. Sasa umejumuisha mahitaji mapya ya kibiashara na kuendana na maendeleo ya kiteknolojia.

“Unarahisisha shughuli za kibiashara, hasa katika uagizaji na usafirishaji wa bidhaa,” amesema.

Amebainisha kuwa mfumo huo unaziunganisha taasisi 36 zinazoweza kuutumia, hivyo kuboresha mawasiliano kati yao.

Aidha, amesema kutakuwa na matumizi bora ya taarifa, kwani data zitasimamiwa vizuri, hivyo kusaidia maafisa wa forodha na taasisi nyingine kufanya maamuzi sahihi.







Related Posts