Pamba, Fountain zamgombea Sebo | Mwanaspoti

PAMBA Jiji na Fountain Gate zimepelekana Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwa kile kinachodaiwa miamba hiyo yote miwili kudai beki wa kati wa kikosi cha Azam FC, Abdallah Kheri ‘Sebo’, aliyetolewa kwa mkopo zina uhalali wa kumtumia.

Nyota huyo ni miongoni mwa wachezaji watano walioondoka ndani ya kikosi hicho cha matajiri wa Jiji la Dar es Salaam Azam FC dirisha la Januari na kupelekwa kwa mkopo Fountain Gate, ingawa Pamba inadai alisaini kwao kabla ya yote hayo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Pamba, Ezekiel Ntibikeha, alisema ni kweli beki huyo walifikia makubaliano na kusaini mkataba, ingawa wameshangazwa kuona anaenda Fountain Gate tofauti na walivyokubaliana mwanzoni.

“Tulikubaliana kila kitu na mchezaji na akasaini mkataba wa miezi sita, tumeshangaa kusikia ameenda tena Fountain Gate, tumefungua kesi kwenye Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji wa (TFF) na itasikilizwa kesho Jumanne ya Januari 28.”

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Fountain Gate, Kidawawa Tabitha alipotafutwa kuzungumzia hilo, alisema bado hajapata barua rasmi, ingawa Mwanaspoti limepenyezewa taarifa kwamba mchezaji huyo anataka kuichezea ‘TP Lindanda Wana Kawekamo’, Pamba FC.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji wa (TFF), Said Soud alipotafutwa kama kweli shauri hilo liko mikononi mwao na litasikilizwa kesho Jumanne, alisema ikiwa lipo wataliweka wazi na litajulikana pia.

‘Sebo’ aliyetamba pia na timu za JKU, Zimamoto na Ndanda ni miongoni mwa nyota watatu waliotolewa kwa mkopo na Azam FC, akiungana pia na kipa, Ali Ahamada aliyeenda KMC na mshambuliaji, Adam Adam aliyetua kwa Maafande wa Tanzania Prisons.

Related Posts