Dar es Salaam. Kwa nini Tanzania iuze umeme nje ya nchi, ilhali bado haijatosheleza mahitaji yake ya ndani?
Swali hilo linawakilisha maswali lukuki wanayojiuliza baadhi ya Watanzania, kuhusu uwezekano wa Tanzania kumulika nje wakati ndani mwake kuna giza.
Msingi wa maswali hayo ni ukweli kwamba, upatikanaji wa umeme nchini ni takriban asilimia 75 kwa mujibu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Licha ya kiwango hicho cha usambazaji umeme kwa wananchi wake, Tanzania inauza umeme kwa mataifa ya Kenya, Zambia na Malawi.
Hata hivyo, Tanzania inazalisha Megawati 3,600 za umeme zaidi ya mahitaji yake ambayo ni megawati 1,800.
Tofauti ya mlinganyo wa uzalishaji na usambazaji, unatokana na uhaba wa miundombinu ya usafirishaji, inayohitaji fedha kujengwa.
Katika mazingira hayo, Tanzania inalazimika kuuza ziada ya umeme inaouzalisha, kupata fedha za kusambaza umeme ndani, kama inavyoelezwa na Mhandisi Mwandamizi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Andrew Mugua.
Hatua ya Tanzania kuuza umeme nje, amesema ni mkakati wa kuongeza mapato ya kigeni.
Mathalan, ripoti ya Benki ya Dunia mwaka 2022, inaonyesha Tanzania iliingiza Dola 12 milioni (zaidi ya Sh30.5 bilioni) kutokana na mauzo ya umeme nchi jirani.
Mugua anaeleza hilo, akifungamanisha na mradi wa usambazaji umeme msongo wa kilovoti 400 wa Zuzu jijini Dodoma uliofadhiliwa na AfDB na Shirika la Maendeleo la Japan (Jica).
Kwa mujibu wa Mhandisi huyo, mradi huo ni moja ya vituo vinavyotengeneza miunganiko ya mifumo ya njia za umeme kutoka nchi moja kwenda nyingine.
Miunganiko hiyo, amesema ni katika nchi za Kusini mwa Afrika kupitia Iringa na Mashariki mwa Afrika kupitia Singida.
Amesema uuzaji umeme nje ya nchi pia, unaziunganisha nchi za Afrika na hatimaye zitegemeane katika usambazaji wa umeme.
Hata hivyo, hatua ya Tanzania kuuza umeme kwa baadhi ya mataifa ya Afrika, imetangulia katika mpango wa uwezeshaji wa upatikanaji wa umeme kwa watu milioni 300 Afrika.
Mpango huo, ndio ulioitisha wakuu wa nchi za Afrika wanaokutana kesho, Januari 27 na 28, kujadili kuhusu uwezeshaji wa upatikanaji wa nishati kwa Waafrika hao.
Tanzania ndio nchi mwenyeji wa mkutano huo, ambao pamoja na mambo mengine mataifa 14 ya Afrika yatasaini mkataba wa kutekeleza maazimio ya uwezeshaji wa upatikanaji wa umeme kwa Waafrika milioni 300 ifikapo mwaka 2030.
Meneja wa Mradi wa Usambazaji Umeme wa Zuzu Backbone, David Mrema amesema mradi huo unakuza njia ya kusafirisha umeme.
Amesema mradi huo umewezesha kuhimili ongezeko la wateja wa umeme katika Mkoa wa Dodoma hasa baada ya Serikali kuhamia jijini humo.
Ameeleza njia hiyo ina uwezo wa kubeba Megawati 2,000 na inaweza kukusanya vyanzo vingi vya umeme kuelekea Kaskazini mwa Tanzania.
Amesema dhamira ya mradi huo ni kuhudumia ndani kwa kuongeza mtandao wa usambazaji, lakini kuongeza fursa za kuunganisha na mataifa mengine.