SIMBA inaianza safari ya michuano ya Kombe la Shirikisho ikiwa nyumbani kuikaribisha Kilimanjaro Wonders, huku kocha msaidizi wa timu hiyo, Seleman Matola akisema hawatawadharau wapinzani wao hao kwa vile msimu huu, Wekundu wa Msimbazi hawaachi kitu katika mbio za kurejesha mataji klabuni.
Wekundu hao wenye mzuka baada ya kutinga robo fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, ikiongoza kundini mbele ya CS Constantine ya Algeria, Bravos do Maquis ya Angola na CS Sfaxien ya Tunisia itaikaribisha timu hiyo ya Kilimanjaro katika mechi ya 64 Bora leo Jumapili kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge, Dar es Salaam.
Mchezo wa leo unatazamiwa kwa umakini zaidi na timu zote mbili huku kila moja ikiwa na hesabu, Simba ikiuchukulia mpambano huo kwa umakini mkubwa ili kuepuka kurudia makosa ya nyuma kwani imewahi kuondolewa mapema na timu za madaraja ya chini katika misimu miwili tofauti nyuma.
Msimu wa 2017/18, Simba ilitolewa hatua ya pili na Green Warriors ya Ligi Daraja la Pili kwa mikwaju ya penalti 4-3 baada ya sare ya bao 1-1 katika dakika 90. Wakati huo ilikuwa bingwa mtetezi.
Baada ya hapo, msimu uliofuatia wa 2018-2019, pia ilitolewa na Mashujaa enzi hizo ikiwa Ligi Daraja la Kwanza kwa kufungwa mabao 3-2 ndani ya dakika 90.
Kwa upande wa Kilimanjaro Wonders inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Mkoani wa Kilimanjaro, inahitaji kuendelea kuonyesha ubora wake licha ya kwamba inafahamu inakutana na timu ya levo kubwa zaidi yao.
Akizungumzia mchezo huo, Kocha Msaidizi wa Simba, Seleman Matola amesema wanafahamu ni mchezo muhimu kwao, hivyo hawawezi kuidharau timu wanayokutana nayo.
“Tumejipanga kwa sababu ni mechi ya mtoano, tunafahamu mechi za mtoano siku zote hazina mwenyewe kwa maana ukikosea tu unajikuta nje kwa hiyo tunauchukulia kwa umuhimu mkubwa sana.
“Tunakwenda kuucheza kama fainali kwa sababu tuna uzoefu na mashindano haya na timu kama hizi kwani si mara moja zimewahi kututoa, hivyo tunauchukulia kwa umuhimu mkubwa sana ili kufuzu hatua inayofuata,” alisema Matola na kuongeza.
“Tunakutana na timu ambayo hatuifahamu ila wao wanatufahamu, imetupa ugumu katika maandalizi yetu, tumejaribu kutafuta namna ya kuwafahamu imekuwa ngumu, lakini tuna uzoefu na timu hizi, tunajua tutacheza nayo vipi.
“Ifahamike tu hakuna timu ndogo wala kubwa, siku hizi kila timu inaweza kucheza mpira na kufanya vizuri popote, tutapanga kikosi kuendana na mchezo wenyewe.”
Ikumbukwe, tangu kuanzishwa kwa michuano hiyo mwaka 1967 Simba imebeba ubingwa wa michuano hiyo mara nne mwaka 1995, 2016/17, 2019/20 na 2020/21. Vinara wa kubeba kombe hilo ni Yanga waliochukua mara nane 1967, 1974, 1999, 2001, 2015/16, 2021/22, 2022/23 na 2023/2024 ambao kwa sasa ni wa watetezi, huku Azam imebeba mara moja msimu wa 2018/19.
Kocha wa Kilimanjaro Wonders, Daud Macha amesema kikosi chake kipo katika hali nzuri kwa ajili ya mchezo huo huku jambo kubwa ni hawana majeruhi yeyote.
“Tunaiheshimu Simba kwa sababu ni timu kubwa na wachezaji wetu ni wachanga, tumekuja kwa ajili ya mchezo huu ambao tunahitaji kufanya vizuri, kikosi changu nashukuru kipo tayari na hakuna majeruhi.
“Huu ni mchezo wa mpira wa miguu hivyo hatuwezi kusema tumekuja kupoteza, bali tumekuja kushindana.
“Aina ya uwanja tunaokwenda kuchezea kwetu sio mgeni kwani takribani miezi mitatu nyuma tulikuwa Ujerumani pia kucheza kwenye umati wa watu sio wageni ila tu tunaweza kusema tunakutana na wachezaji wazoefu kitu ambacho kinaweza kuwa shida lakini kwenye suala la mazingira na uwanja ni kitu cha kawaida.
“Ukiangalia timu yetu na wao ni vitu viwili tofauti, tumezungumza na wachezaji wetu na kuwaambia tunakwenda kukutana na timu ya aina gani, tutawaheshimu, tutacheza kama vile tupo mazoezini tunavyofanya siku zote.
“Hadi kufikia hapa tulipofika tunajua sisi tumefikaje, hii ndiyo nafasi kwa vijana kuonekana zaidi, sidhani kama vijana wangu wana hofu ya kukutana na mchezaji mwingine kama yeye. Tumewajenga kisaikolojia, mtaona kesho nini wanakifanya uwanjani licha ya kwamba ni vijana wadogo,” alisema kocha huyo.
Kilimanjaro Wonders Soccer Center ni kituo cha kulea na kukuza vipaji vya soka kutoka Moshi, mkoani Kilimanjaro ikiwa inashiriki Ligi ya Mkoa wa Kilimanjaro.
Ilianzishwa Julai 2022 na inaundwa na wachezaji wavulana na wasichana wenye umri kuanzia miaka 11 hadi 20.