SIMBA imeanza michuano ya Kombe la Shirikisho kibabe kwa kuifumua Kilimanjaro Wonders kwa mabao 6-0, huku ikiandika rekodi mbili katika hatua ya 64 Bora kwenye Uwanja wa KMC Complex, jijini Dar es Salaam.
Rekodi ya kwanza iliyowekwa na timu hiyo ni kufunga bao la mapema likiwekwa sekunde 18 baada ya filimbi ya kwanza ya kuanzisha mchezo, kisha kufunga mabao 6-0 ikiwa ni idadi kubwa ya mabao katika hatua hiyo ikikamilisha timu ya 32 iliyotinga hatua inayofuata ikizifuata Yanga na Azam zilizotangulia.
Katika mchezo huo uliokuwa wa upande mmoja, Simba ilionyesha mapema kuwa na uchu wa ushindi kuanzia dakika ya kwanza tu ilifunga bao kupitia kwa Valentino Mashaka kabla ya kuongeza mengine na kufanya iende mapumziko ikiwa mbele ya mabao 4-0.
Mashaka aliandika rekodi ya kufunga bao la mapema zaidi katika hatua hiyo kwa msimu huu akitengenezewa krosi safi na beki wa kushoto Valentin Nouma kabla ya mvua ya mabao ikiendelea kuharibu nyumba ya vijana hao wa Kilimanjaro.
Kiungo mshambuliaji Ladack Chasambi alifunga bao la pili dakika ya tatu akimalizia krosi ya beki wa kulia David Kameta ‘Duchu’ baada ya kugongeana vizuri kwenye shambulizi la bao hilo kabla ya dakika sita baadae beki wa Wonders, Patrick Sebastian kujifunga wakati akiongoa shuti la Nouma kabla ya Joshua Mutale kuandika bao la nne dakika ya 21.
Kipindi cha pili Simba bado ikaendelea kuliandama lango la Kilimanjaro ikipata bao la tano kupitia kwa mshambuliaji Steven Mukwala kwa kichwa akimalizia krosi ya Duchu kabla ya Edwin Balua kupiga la sita.
Jana beki mpya wa Yanga ambaye ni beki wa zamani wa Simba Israel Mwenda alianza kwa mara ya kwanza na kutengeneza mabao mawili na Jana Duchu naye amamlipa akitengeneza mabao mawili kwa timu yake.
Dakika ya 54 na 56 Kilimanjaro ilijaribu kufanya mashambulizi makali ambayo almanusura waaadhibu Simba lakini washambuliaji wakakosa umakini huku kipa Ally Salim akisimama vyema na kuokoa shambulizi Moja.
Hadi mwisho wa mchezo Simba ikaondoka. na ushindi huo mkubwa wa mabao 6-0 na kuwa timu ya 15 za Ligi Kuu Bara kutinga hatua ya 32 Bora ya mashindano hayo.
Katika mchezo huo, Simba ilianza na wachezaji wengi wasitumika kikosi cha kwanza.