Simulizi ya wazazi waliotupwa shimo la choo, kuporwa mtoto (2)

Kibaha. Jana Jumamosi, Januari 25, 2025, tulianza simulizi ya wanandoa ambao mtoto wao wa miezi saba alichukuliwa na watu wasiojulikana walipovamia nyumbani kwao asubuhi ya Januari 15 na kupatikana Januari 24. Tukio hilo lilitokea katika kijiji cha Kumba, eneo la Kibaha kwa Mfipa, Mkoa wa Pwani.

Katika sehemu ya kwanza iliyoanza jana, Johana, mama wa mtoto huyo, Merysiana Melkizedeck, alisimulia maisha aliyopitia katika siku tisa za kumtafuta mtoto wao hadi walipopewa taarifa za kupatikana kwake na kukabidhiwa na polisi.

Katika mahojiano aliyofanya na Mwananchi nyumbani kwake, kijiji cha Kumba, umbali wa kilomita sita kutoka Kibaha kwa Mfipa, Melkizedeck Mrema, baba wa mtoto huyo, anasema hakutegemea kama watu hao ambao walionyesha nia ya kumuua wangeenda mbali na kumchukua mtoto.

Melkizedeck Mrema (kushoto) na mkewe Johana Bung’ombe wakiwa na mtoto wao aliyetekwa,Mesiana Mrema nyumbani kwao Kibaha Mkoa wa Pwani baada ya kufanikiwa kumpata. Picha na Michael Matemanga

“Hadi sasa nashindwa kuelewa lengo ni nini; sina uadui na mtu yeyote na huku sisi ni wageni, tumehamia miezi minne iliyopita. Wale watu hawakuwa na nia ya kuiba pekee, walitaka kuniua pia, lakini sikufikiria kama wangekuwa na uthubutu wa kumdhuru mtoto,” anasema Mrema.

Yeye ndiye aliyekuwa wa kwanza kuwaona watu hao waliofika nyumbani kwake asubuhi ya Januari 15 na kutekeleza uhalifu huo, ikiwa ni pamoja na kumuiba mtoto wao.

Anasema asubuhi ya siku hiyo, kama ilivyo ada, aliamka kufanya shughuli za nyumbani kabla ya kujiandaa kwenda kwenye majukumu yake, ndipo alipovamiwa na watu hao wanne na kupigwa na nondo.

“Ilikuwa kumeshakucha kabisa, inaelekea saa moja kasoro asubuhi. Nilipotoka nje na kuzunguka kwenye banda la kuku kuwafungulia, nilipofungua mlango nikakutana na vijana wanne wakaniwahi na kuanza kunishambulia.

Mmoja alikuwa na nondo akanipiga nayo kichwani, mwingine akatoa panga, na wakati nazuia asinipige kichwani, likanikata mikononi. Hapo nikaona hawa watu hawatanii. Ikabidi nitii maelekezo ili wasitudhuru.

Anasema watu hao walimuamuru aingie ndani, akatii, na wakafunga milango yote kuzuia mtu kuingia kisha wakaendelea kumshambulia huku wengine wakibeba vitu vya ndani.

“Wakati wananishambulia huku wakiongea kwamba wanataka kunimaliza, mke wangu alitoka na kuanza kubishana nao. Mmoja wao alimrudisha chumbani na kumwambia atulie huko.

“Pale sebuleni walichukua kila walichoona kinafaa, wakaingia vyumbani wakachukua walivyohitaji, ikiwemo simu, na kunitaka niwape namba za siri. Nilifikiri nikiendelea kutoa ushirikiano wataondoka watuache, haikuwa hivyo. Niliwapa namba za siri, lakini bado waliendelea kunishambulia,” anasema na kuongeza:

“Baada ya kuridhika na walichokifanya, walinitoa nje na kuzunguka kwenye banda la kuku, ambako kuna shimo la choo lenye urefu wa futi 12. Wakati tunakwenda nje walikuwa wamenifunga kamba mikononi. Tulipofika, walifunua mfuniko wa shimo hilo lenye kinyesi na majitaka na kunitaka nitumbukie,” anasema.

Kila kitu kina hasara na faida zake. Kwa Mrema, ukubwa wa umbo lake ulikuwa kikwazo kwake kuingia kwenye shimo hilo. Licha ya watu hao kumuweka kwenye mdomo wa shimo na kumtaka ajisukume kuelekea chini, haikuwa rahisi kwake kupita.

“Mimi ni mnene, kwa hiyo haikuwa rahisi kupita kwenye mdomo wa shimo nikiwa nimefungwa mikono. Hivyo nikawaambia kama mnataka nitumbukie humu, nifungueni. Wakawa wanabisha na kunilazimisha kunisukuma. Hivyo nikawa naning’inia, miguu ikiwa ndani na mwili ukiwa nje.

“Baada ya wao wenyewe kuona haiwezekani, mmoja wao alikata ile kamba mikononi mwangu. Hapo lilifanikiwa zoezi la mimi kutumbukizwa kwenye shimo. Wakati hayo yanaendelea, mke wangu na mtoto walikuwa ndani.

Mrema anasema baada ya dakika kadhaa, akahisi kuna utulivu. Akaanza kugonga kwenye bomba linalopokea maji taka ndani ya shimo hilo huku akiita jina la mkewe, lakini hakupata majibu.

Alikaa ndani ya shimo hilo kwa dakika zisizopungua 45 ndipo aliposikia kishindo cha mtu aliyefika nyumbani hapo na kubisha hodi.

“Aliyekuja ni mzee aliyeagizwa aje kunifuata nikafungue duka maana kulikuwa na mzigo wa saruji nilipaswa kupeleka kwa mteja. Baada ya kuona duka halijafunguliwa hadi muda ule, alikuja, na anasema alipofika pale alisikia sauti za mtu anayegonga. Hivyo, akajua kuna fundi ndipo akazunguka nyuma.

“Alipofika kwenye shimo, nikaongeza sauti zaidi na akanisikia. Alifungua ule mfuniko ambao wale watu walikuwa wameufunika. Alijaribu kuweka ngazi lakini ikashindikana, hivyo akaenda kutafuta kamba na kutoa taarifa kwa mwenyekiti aliyefika eneo la tukio.

Punde baada ya kutoka, akili ya Mrema ilielekea kwa mke na mtoto wake. Majirani walijaribu kuita lakini hakukuwa na majibu.

Kwa kuwa milango ilikuwa imefungwa, ilibidi Mrema kutumia dirisha alilotengeneza kama mlango wa dharura kuingia ndani ya nyumba hiyo kwa ajili ya kumsaka mke na mtoto wake. Hata hivyo, alipigwa na butwaa kwa kuwa hakuwakuta.

“Nilizunguka kila kona ya nyumba, sikuwaona. Nilichanganyikiwa. Akili yangu ikaniambia kuwa hawa watu wameondoka nao, maana miongoni mwa vitu walivyochukua ni gari ambalo walilikuta nje.

“Pale pale, nikaomba ‘smartphone’ ya jirani ili nifuatilia (track) walikokuwa. Nilibaini kuwa walikuwa eneo la Msangani.

“Nikawaambia majirani twende tuwafuatilie, lakini wakasema ni hatari kwa usalama. Badala yake walishauri tuende polisi tukatoe taarifa. Tulifanya hivyo, na polisi wakaja pale nyumbani kwa ajili ya mahojiano na kukusanya taarifa walizohitaji.”

Mrema aendelea kutafuta familia yake

Bado akili ya Mrema ilikuwa inazunguka kutaka kujua ilipo familia yake. Kwa kuwa eneo walipoishi limezungukwa na vichaka, alianza kuzunguka huku na kule akiamini huenda watu hao wamewatupa huko au kuwaacha kwenye nyumba ambazo ujenzi wake haujakamilika.

“Kutwa nzima nilikuwa kama nimechanganyikiwa, nazunguka tu kwenye mapori. Hakuna nilichokipata. Ilipofika saa kumi jioni, akili ikaniambia niende upande wa pili kuna nyumba ambayo haikaliwi na watu na yenyewe kuna shimo kama lile la nyumbani kwetu.

“Nilipofika pale, nikasikia sauti ya mke wangu, akipiga kelele kuomba msaada. Kwa kuwa tayari nilishachanganyikiwa, hata sikusikia sauti inatoka upande gani. Pale kwenye shimo walifunika na kuweka nyasi, hivyo sikuhisi kama anaweza kuwa mule. Nilirudi nyumbani na kuwaambia waliokuwa wamenizunguka. Wote tukarudi pale, ndipo tulipobaini sauti inatoka shimoni.

Baada ya mfuniko wa shimo kufunuliwa na kuhakikisha aliye mule ndani ni mke wake, alimuuliza kama yupo na mtoto. Jibu alilopewa lilimkata maini na kujikuta anaondoka katika eneo hilo akiwaacha watu wakimtoa mkewe.

“Nilipomuuliza, ‘upo na mtoto?’ na akajibu ‘Hapana,’ hapo nilichanganyikiwa zaidi. Nikawa najiuliza hawa watu walikuwa na nia gani? Kwanini walidhamiria kutuua familia nzima? Je, mtoto wamemtupia kwenye shimo lipi? Maana wazazi wake walitupwa kwenye mashimo ya vyoo. Nikaanza kuzunguka kwenye vichaka kumsaka,” anasimulia.

Hayo ndiyo yalikuwa maisha yake katika siku zote tisa, akiamini huenda angeweza kumkuta mtoto wake ametupwa kwenye shimo kama ilivyofanyika kwao au kwenye vichaka, lakini haikuwa hivyo.

“Kuna wakati yalinijia mawazo ya kukata tamaa. Nikajisemea, ni heri tuupate hata mwili wake. Lakini kila nilipokuwa nasali, nilipata imani kwamba mtoto yuko salama na atarudi. Mtoto wangu anapenda nanasi. Juzi nilienda sehemu kuchukua mananasi, nikaliweka moja chumbani na kuwaambia, ‘Hili atakuja kula mwanangu akirudi.’

“Sijui kwanini nilikuwa na imani hiyo, lakini niliagiza lile nanasi lisiguswe na mtu kwa kuwa tutalila mimi na mtoto wangu. Na hivyo ndivyo inavyokwenda kuwa; leo tutalimenya, tulile na mwanangu,” anasema Mrema akitabasamu.

Mtoto alichukuliwa katika mazingira gani?

Johana anasema baada ya mumewe kupelekwa nje, watu hao walirudi ndani na kumchukua yeye. Mmoja wao alimchukua mtoto na kumuweka pembeni.

“Walitoka na mimi nje. Mtoto alibaki ndani na walifunga mlango. Walinipeleka hadi kwenye shimo na kunitumbukiza humo kisha wao kuondoka. Bahati iliyoje kwangu, shimo lile halikuwa limetumika kwa muda mrefu. Wenye nyumba walihama, hivyo uchafu ulikuwa umekauka.

“Nikiwa mule, nilihisi ni mimi peke yangu ndiye nimeondolewa. Niliamini kuwa watakuwa wameshamalizana na mume wangu, wamemuacha salama, na mtoto yuko ndani. Kumbe haikuwa hivyo. Waliondoka na mtoto wangu,” anasema Johana.

Hata hivyo, jitihada zilizofanywa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani ziliwezesha kukamatwa kwa watu watatu wakiwa na mtoto huyo katika pori la Kimara Misare lililopo Mlandizi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, alisema baada ya kufanyika msako, Januari 24 saa tisa usiku, walifanikiwa kuwakamata watu hao na mtoto huyo. Mtoto alipelekwa hospitali ya Tumbi kwa ajili ya uchunguzi, uliobaini kuwa ni mzima wa afya.

Related Posts