KOCHA Msaidizi wa Singida Black Stars, David Ouma ametamba timu hiyo imekamilika kila idara na ipo tayari kwa ajili ya mzunguko wa pili huku akitamba licha ya ugeni wa benchi la ufundi, wanajivunia wachezaji wao kuingia kwenye mfumo kwa uharaka.
Singida Black Stars iliingia kambini mapema kwa ajili ya kujiweka sawa chini ya benchi lao jipya wakijichimbia Jijini Arusha na inaelezwa kambi hiyo ipo katika mchakato wa kuvunjwa hivi karibuni, ili kurudi Singida kujiandaa na ngwe ya lala salama ya Ligi Kuu Bara.
“Tulikuwa na mapungufu kwenye maeneo machache, sasa yamefanyiwa maboresho dirisha lililofungwa hivi karibuni na wachezaji tuliowaongeza watatibu mapungufu tuliyoyaona na wapo kwenye hali nzuri ya ushindani,” alisema Ouma na kuongeza;
“Singida Black Stars ipo tayari kwa mapambano kwa kasi ile ile tuliyoanza nayo bila kujali mabadiliko ya benchi la ufundi, hii ni kutokana na timu kuingia kwenye mfumo wa benchi jipya la ufundi ambalo lilianza majukumu siku chache baada ya kutambulishwa.”
Ouma alisema kijumla timu yao ipo kwenye hali nzuri ya utimamu na wachezaji wote kwa asilimia 90 wapo tayari kwa kuipambania kuhakikisha inafikia malengo ya kumaliza tano bora msimu huu na kupata nafasi ya kuiwakilisha nchi kimataifa.
“Timu yote ipo vizuri, pia ukiangalia mchezaji mmoja mmoja kila nafasi, tumetengeneza kikosi cha ushindani ukiangalia na ratiba ngumu iliyo mbele yetu tunakuwa na imani ya kufanya vizuri,” alisema na kuongeza;
“Baada ya marekebisho ya ratiba tulikuwa na mpango wa kukaa jijini Arusha kwa mwezi mzima lakini sasa tunatarajia kurejea Singida tayari kwa mapambano ya kupambania nafasi ya uwakilishi wa michuano ya kimataifa, nafasi hiyo inawezekana na tupo tayari.”
Akizungumzia ratiba kwa jumla alisema sio rahisi kwao lakini wapo tayari kupambana kuhakikisha wanakusanya pointi zote za Februari katika mechi sita walizopangiwa tatu nyumbani tatu ugenini.
Mwezi ujao wakati Ligi Kuu ikirudi, Singida iliyopo nafasi ya nne kwa sasa inatarajiwa kukutana na Kagera Sugar nyumbani, KMC, JKT Tanzania, Yanga zote ugenini na kumalizana na Pamba Jiji na Mashujaa nyumbani.