Japo dhima, lengo na maana kubwa vya ndoa ni kwa wawili kuishi pamoja kwa upendo, usawa na matarajio ya kuishi pamoja, nyingine ni kutengeneza au kuzaa watoto kwa lengo la kuendeleza kizazi.
Hata hivyo, siku hizi ndoa inabadilika, hasa kwenye nchi za magharibi ambako hitajio la watoto si shuruti tena, bali chaguo na uamuzi wa wanandoa. Kwa Afrika, bado hitajio hili siyo chaguo wala utashi, bali shuruti. Hivyo, watoto wanapokosekana, ndoa huyumba hata kuvunjika.
Leo tutadurusu changamoto, ulazima na umuhimu wa watoto. Kabla ya kuzama, tunagusia aina za ndoa za kisasa. Si ajabu kuona wanandoa walioamua na kuishi bila kuwa na watoto si kwa sababu hawawezi, bali hawataki kutokana na sababu wanazojua. Ndoa inaweza kutotoa watoto kwa sababu mbalimbali, zikiwemo kutotaka au kuwa tayari kuwa na watoto, matatizo ya kiafya, n.k. Pia, zipo ndoa zinazopata watoto lakini wakafariki au wakaharibika kitabia kutokana na sababu mbalimbali.
Kuna ndoa za kuasili watoto ambazo ni nyingi siku hizi kwenye nchi za magharibi. Katika ndoa hizi, wahusika ima kutokana na kutojaliwa kuweza kuzaa au kutotaka kuwa na watoto, huamua kuasili watoto na kuwalea kama watoto wao wa kuzaa.
Kadhalika, wapo wanandoa wasiopenda watoto kabisa. Hawa, badala ya kuasili watoto, huamua kufuga wanyama almaarufu pets au wanyama kipenzi ambao, licha ya kuwaliwaza wahusika, huwapenda na kuwagharimia kwa kila jambo. Pamoja na changamoto na gharama za kuwa nao, watoto ni zao la upendo wa wazazi lilengalo kuwa mbegu ya kuzalisha wengine ili maisha yawe endelevu. Hata hivyo, wana changamoto zake kuanzia kuwagharimu wazazi kifedha na kulhali. Si jambo rahisi kuzaa au kulea watoto. Kwani, wanahitaji muda, matunzo, na zaidi upendo pamoja na malezi kwa jumla. Kuzaa, kwa lugha rahisi ni kujitoa mhanga kwa mtu mwingine bila kukubaliana au kutegemea malipo.
Ndiyo maana, tunasema kuwa watoto ni zao la upendo ambao hatuna nguvu nao. Ulishawahi kujiuliza ni kwa nini wazazi wanawapenda watoto kuliko hata wanavyojipenda wao wenyewe?
Hata kwa wasio na watoto, ni kwa nini watoto wanapendwa na kuthaminiwa sana. Mtoto akilia, hata kama ni kwenye mkutano wa mtu au watu wenye madaraka, husikilizwa na kuvuta hisia za kila mtu. Kwa nini?
Je, ni kweli tunawapenda watoto au kuna kitu tumeumbwa nacho chenye kutushurutisha kuwapenda watoto? Je, ni kwa nini kuku ambaye akimuona binadamu au mwewe hukimbia, lakini akawa tayari kupambana anapokuwa na vifaranga?
Ukitafakari hili, utajua tunachomaanisha tunaposema kuna kitu tumeumbwa nacho kinachotushurutisha kuwapenda watoto hata kuliko tunavyojipenda.
Hata hivyo, hii haiondoi uhalisia kuwa, kwa upande wa pili kinzani, wapo wazazi wanaoua watoto wao. Pamoja kuwa sisi si madaktari wa akili, kuna tafiti nyingi zinazoonyesha kuwa wanaofanya hivi, huwa na changamoto au matatizo ya kiakili.
Maana, kuua mtoto, ni sawa na kuchoma au kuteketeza mali kwa makusudi. Lazima kuwapo sababu au tatizo kiakili kwa mhusika. Kuweka kirahisi, mbwa akimng’ata binadamu, ni jambo la kawaida. Je, inakuwaje binadamu akimng’ata mbwa? Pamoja na kuwa baraka na tunda la upendo, wanaweza kudumisha au kuvunja ndoa. Katika baadhi ya mila, kuna namna watoto wanavyoweza kuvunja au kudumisha ndoa. Mfano, wapo wanaowaacha wenza wao kwa sababu hawana uwezo wa kuzaa au tuseme ni tasa au wana ugonjwa unaowanyima uwezo wa kuzaa. Kwa kina mama, tatizo hili huleta mateso, sonona, usumbufu hata madhara yasiyoelezeka.
Utasikia ‘anajaza choo’ na mengine mengi. Je, inapotokea mume hawezi kubebesha mimba, hali inakuwaje? Kuna baadhi ya makabila, muathirika kama huyu husaidiwa na ndugu zake kupata watoto.
Pili, wapo wanaoweza kuvunjikiwa ndoa, hasa akina mama wanaozaa watoto wa jinsia moja. Wengi ni wale wanaozaa mabinti tu. Nafasi yetu ni fupi.
Tumalizie kwa maswali. Je, zinapotokea hali hizo juu, wewe ungekuwa muathirika ungetaka utendewe vipi? Je, kuna mtu anayechagua mapungufu kama haya? Je, wajua kuwa anayesababisha jinsia za watoto ni baba na si mama? Kwa ujinga tu, mwanamke ndiye hulaumiwa! Tujifunze