Dodoma. Mkutano wa 18 wa Bunge la 12 unaanza keshokutwa Jumanne, Januari 28, 2025 huku wachambuzi wa masuala ya siasa na wananchi wakiwashauri wabunge kuutumia muda uliobaki kujifanyia tathmini ya utekelezaji wa majukumu yao kwa miaka mitano.
Kuanza kwa mkutano huo kunalifanya Bunge la 12 lililoanza Novemba 2020, kubakiza mikutano miwili kabla ya kumaliza ili kwenda kwenye Uchaguzi Mkuu Oktoba 2025.
Katika Bunge hilo linaloongozwa na Spika Tulia Ackson, taarifa za utekelezaji wa shughuli za kamati za kudumu za Bunge kwa mwaka 2024 zitawasilishwa kwa mara ya mwisho.
Shughuli kuu ya mkutano wa18 itakuwa ni kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa kamati hizo kisha kufanya uamuzi kwa maazimio watakayotoa kwa Serikali kwa ajili ya utekelezaji.
Kamati hizo ni za Hesabu za Serikali (PAC), Serikali za Mitaa (LAAC), Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC), Afya na Masuala ya Ukimwi, Ardhi, Maliasili na Utalii, Elimu, Utamaduni na Michezo, Maji na Mazingira, Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama pamoja na Bajeti.
Nyingine ni Miundombinu, Nishati na Madini, Sheria Ndogo, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Utawala, Katiba na Sheria, Uwekezaji wa Mitaji ya Umma na Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo.
Wakati kamati hizo zikiwasilisha taarifa zao, pia miswada ya marekebisho ya sheria zilizowasilishwa kwenye mkutano wa 17 wa Bunge na kuchambuliwa kwenye kamati za Kudumu za Bunge, zinatarajiwa kujadiliwa kwenye mkutano wa 18.
Miongoni mwa miswada hiyo ni Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 4, unaolenga kufanyia marekebisho ya Sheria ya Uhamiaji, Sura ya 54, ili kuwapa hadhi maalumu kwa Watanzania wenye uraia wa nchi nyingine.
Muswada huo uliwasilishwa Novemba 8, 2024 baada ya Serikali kuuondoa bungeni Septemba 4, 2024, kwa kile kilichoelezwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Hamza Johari kutoa nafasi ya kuendelea kufanyia kazi zaidi hoja hiyo.
Muswada mwingine ni ule wa Marekebisho ya Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini na miongoni mwa yanayopendekezwa ni kufanyiwa marekebisho ya kifungu cha 33 kinachohusu likizo ya uzazi ili kuongeza likizo ya uzazi kwa mwajiriwa atakayejifungua mtoto njiti.
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) ni miongoni mwa wadau waliofika mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, kutoa maoni yao juu ya muswada huo na kutaka muda wa likizo kuongezwa zaidi ya unaopendekezwa katika muswada huo.
Ilipendekeza iwapo atajifungua mtoto kabla ya muda haujatimia, basi apewe muda wa uangalizi wa mtoto mpaka mtoto akamilishe wiki ya 40 badala ya wiki 36 zilizopendekezwa katika muswada huo, kisha ndio apewe likizo ya uzazi ambayo haitaathiri ule muda wa uangalizi wa mtoto kabla ya kukamilisha wiki 40.
Akizungumza na Mwananchi, Mkazi wa Mailimbili, Rosemary Mwambeja amesema kutokana na taarifa hizo za shughuli za kamati kuwa ni za mwisho kabla ya Bunge kuvunjwa, wabunge wanapaswa kuangalia mambo ambayo yamekuwa yakijirudia mara kwa mara wakati wa kiwasilisha taarifa zake.
“Kwa mfano mradi wa Mchuchuma na Liganga katika kila taarifa kwa kipindi cha miaka mitano tumekuwa tukiusikia lakini utekelezaji bado. Licha ya wabunge kuelezea manufaa, lakini Serikali haijaja hadharani kutueleza kuwa wamefikia wapi,” amesema Mwambeja.
“Sijui watafanyaje, lakini ikiwezekana wafanye kama tulivyoona kwa mabunge mengine hata bajeti zilikuwa zinagomewa kupitishwa hadi Serikali ijieleze vizuri kuwa itafanya lini na kwa fedha gani.”
Alex Ibrania, mkazi wa Nzuguni amesema ni mategemeo ya wananchi waliowengi taarifa za kamati zitakuja kwa mtindo mwingine kwa kueleza mambo waliyokuwa wakishauri na kuazimia katika taarifa zao za miaka minne yamefanyiwa kazi kwa kiwango gani.
“Ni wakati wa kuibana Serikali itekeleze ahadi walizoahidi kupitia Ilani ya uchaguzi maana wanarudi sasa kwa wananchi ambao watawahoji mbona waliwaahidi mambo kadhaa kwa kadhaa yako wapi. Mfano katika maeneo mengi ya vijijini bado shida ni barabara hazipitiki hasa wakati wa mvua,” amesema.
Mkazi wa Mwenge jijini Dar es Salaam, Mariam Juma amesema: “Hiki ni kipindi cha sisi wananchi kuwaona hawa wabunge wetu wamefanya nini. Wao wenyewe wajiulize wamefanya nini na mwisho watakuja kwetu, tena kutuomba kura kwa hiyo wao wenyewe huko wajipime kama wanastahili kurudi tena kutuomba kura.”
Wataka wabunge kujitathmini
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St Augustine (SAUT), Dk Ntuli Ponsian amesema kwa kuwa imebaki mikutano miwili kuvunjwa kwa Bunge, mwaka huu sio wa kupanga kazi za kufanya bali ni wa majumuisho na tathmini ya kile kilichofanyika kwa kipindi cha miaka mitano.
“Waseme wamefanya nini tangu washike nafasi hizo, yaani thamani ya pesa ya wananchi iliyowaweka Dodoma na kuwalipa mishahara nini hasa walichokifanya, wamefanikisha wapi, wameshindwa wapi, kwanini wameshindwa na waseme wabunge wajao wafanye nini, hayo ndiyo wanapaswa kuwaambia wananchi waliowatuma,” amesema Dk Ponsian.
Naye Wakili Elias Machibya amesema katika kipindi kilichobaki wabunge wanatakiwa kuangalia utekelezaji ia Ilani ya uchaguzi umefikiwa kwa kiasi gani ili kukimbizana na maeneo yaliyobaki kabla ya kuingia katika uchaguzi.
“Wajaribu pia, kuangalia mambo ambayo wananchi wanalalamikia hata kama hayako katika Ilani ya Uchaguzi. Inawezekana kuna jambo halipo kwenye Ilani lakini ni kero kwa wananchi,” amesema.
Machbya amesema Serikali imefanya vizuri katika sekta mbalimbali nchini lakini bado zipo kero za wananchi wanazolalamikia, hivyo ni vyema Bunge likaongeza nguvu kwenye maeneo hayo ili zishughulikiwe kabla uchaguzi.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA) Profesa Mohammed Makame amesema katika miaka mitano ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi, Serikali imefanya vizuri chini ya usimamizi wa Bunge.
“Bunge limeonyesha dhamira kufuatilia ahadi za Serikali kupitia mikutano na kamati zake za kudumu, limesimamia bajeti ya Serikali na limetunga sheria ikiwamo zile za uchaguzi,”amesema.
Pia, amesema utunzi wa sheria za uchaguzi ulikuwa na msisimko mkubwa ambao ukitumika ipasavyo ni miongoni mwa sheria zitakazokuwa na nguvu kubwa wakati wa uchaguzi, kwa kuwa kwenye utunzi wake umevishirikisha vyama vya siasa.