Wasira amtumia ujumbe Lissu, agusa udiwani na ubunge CCM

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, amesema mabadiliko ya Katiba ya chama hicho yaliyofanyika yatawawezesha kupata wagombea wa udiwani na ubunge wazuri na si mzigo, huku akivionya vyama vya upinzani akisema: “Ikulu wataendelea kuishuhudia kwenye runinga tu.”

Mbali na hilo, Wasira amelitaka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kushughulikia tatizo la kukatikakatika kwa umeme. Pia amesema mabasi ya mwendo haraka njia ya Mbagala yataanza kabla ya Machi 30, 2025, na njia ya Gongo la Mboto yataanza Juni.

Wasira ameeleza hayo leo, Jumapili, Januari 26, 2025, katika hafla ya kumpokea iliyoandaliwa na CCM Mkoa wa Dar es Salaam, iliyofanyika katika uwanja wa Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam

Ametoa kauli hiyo ikiwa ni i takribani wiki moja imepita tangu mkutano mkuu maalumu wa chama hicho uliofanyika Januari 18 na 19, 2025, jijini Dodoma ulipomchagua kushika wadhifa huo, akichukua nafasi ya Abdulrahman Kinana aliyejiuzulu Julai 29, 2024.

Katika mkutano mkuu huo maalumu chini ya Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan, pamoja na mambo mengine ulifanya mabadiliko ya Katiba ya CCM ikilenga kuongeza ushiriki wa wanachama wa chama hicho kwenye vyombo vya uamuzi.

Mabadiliko hayo yanayohusu Ibara ya 47(1), 60(1), na 73(1) ya Katiba ya chama hicho, yameongeza wajumbe 10 kwenye Kamati Kuu wanaochaguliwa kutoka Bara na Zanzibar, kila upande watano.

“Tumebadilisha Katiba ya CCM kuongeza ushiriki mkubwa. Kwa mfano, Jimbo la Kawe ninakoishi, mwaka 2020 kulikuwa na wagombea 100 wa ubunge. Halafu wakikaa pale, asilimia kubwa wanakuwa wapigakura. Sasa unajikuta wanasahau wagombea wanaomba kura kwa wagombea wenzao,” amesema Wasira.

Wasira amesema jambo hilo lilikuwa linasababisha vurugu mechi, hivyo, waliona ni busara kuongeza wapigakura, na sasa mabalozi wa nyumba 10 na wajumbe wao wote watakuwa wapigakura.

“Pamoja na mabadiliko haya mazuri, ombi langu kwenu kwa vikao vya chama: tulete watu wanaoweza kukubalika. Si mnasema huyu mwenzetu nani? Ambaye si mwenzetu? Wote ni wenzetu. Basi mleteni mwenye uwezo ambaye ni mwenzetu,” amesema.

Wasira amesema chama hicho hakiwezi kukubali kuletewa mtu ili mradi na wao kazi yao iwe kusukuma tu kama mzigo, huku akisema hata muasisi wa chama hicho, Mwalimu Julius Nyerere, alisema chama lazima kiwasikilize watu.

“Alisema chama ambacho hakitawasikiliza watu kitalia kilio ambacho kitakosa mtu wa kuwafuta machozi. Leteni watu wanaokubalika, ndiyo maana tunataka vikao vilivyokaliwa na watu vituambie kwa watu tunaowaongoza fulani anatufaa,” amesema.

Wasira amesema bila kuwasikiliza wananchi wataishi maisha magumu, na wasiowatakia mema watapata sababu za kusema CCM haikuleta mtu anayekubalika.

“Migogoro yetu ndani ya CCM ndiyo inawafanya upinzani kupata ushindi. Kwa hiyo, tumebadili mfumo wa uchaguzi ili tupate watu wanaotufaa. Na mabalozi wetu wa nyumba 10 watakuwa wanashiriki moja kwa moja,” amesema.

CCM kupitia mkutano wake mkuu uliofanyika jijini Dodoma na kuongozwa na Mwenyekiti wake, Rais Samia, ilitangaza mabadiliko hayo yanayogusa nafasi ya ujumbe wa Kamati Kuu, na ongezeko la idadi kwa wajumbe wapigakura za maoni kwa madiwani na wabunge.

Sasa itakuwa na kiongozi wa nyumba zisizozidi 20 zenye wanachama wasiopungua 50 na wasiozidi 80 kwa mijini, huku wanachama 30 na wasiozidi 80 kwa vijijini, kutoka 10 za awali.

Katika hotuba yake hiyo, Wasira, mwanasiasa huyo mkongwe amesema kazi ya CCM ni kuendelea kushikilia dola kwa sababu bado wana kazi ya msingi ya kufanya ambayo haiwezi kutekelezwa bila kuwa na dola.

“Tunapowaambia bado tunahitaji kuendelea kushika dola, maana yake ni kwamba kazi tuliyoomba na tukadai uhuru wa nchi hii bado inaendelea. Maendeleo hayana mwisho. Tena niwaambie, kwani yana tabia ya kuzaa matatizo mapya,” amesema.

Katika maelezo yake amesema: “Kuna wenzetu wanaohitaji dola; tunawashtaki kwa wananchi kwamba watavuruga nchi yetu na amani yetu, na wataturudisha nyuma. Lakini sitaki kusema ni kina nani.”

Wasira amesema kuna watu wanajipambanua kwamba Nyerere alisema chama chao ndiyo bora, lakini hakumaanisha hivyo. Alichokuwa anasema ni kiwe chama cha upinzani kweli kweli.

“CCM tunasema binadamu wote ni sawa, lakini wao wanakataa. Halafu wanataka mashindano. Unawezaje kushindanisha vijana wa Temeke maskini na tajiri? Hakuna mashindano hapo. Tunachohitaji ni kuwasaidia wote, ikiwemo wa chini, wapate maisha safi,” amesema Wasira.

Wasira amesema, bahati nzuri Mungu amesikia na amekataa: “Hawawezi kushika dola, wataendelea kuiona Ikulu kwenye runinga.”

Wakati Wasira akieleza hayo, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla, akiwa visiwani Zanzibar amewajibu Chadema wanaosisitiza “hakuna uchaguzi kama hakutakuwa na mabadiliko ya kimfumo (‘No reform, no election’)” kwamba hawana fedha.

Mkutano mkuu wa Chadema uliofanyika Januari 21, 2025, ulipitisha pendekezo la Kamati Kuu ya chama hicho la “No reform, no election.” Mwenyekiti mpya wa chama hicho, Tundu Lissu, amesisitiza akisema kwa sasa wameelekeza nguvu kwenye suala hilo na si kuangalia maandalizi ya uchaguzi.

“Mazingira ya kiuchaguzi ya nchi hii ni mabaya na sheria za uchaguzi ni mbovu. Hazirekebishiki. Zinahitajika kuandikwa upya. Kama kweli tunataka kushinda, lazima turekebishe sheria. Hatutashiriki na tutajitahidi kutumia umma usifanyike,” alisema Lissu.

Lissu amesema lengo ni kuhakikisha kunakuwa na uchaguzi huru na haki ili waiondoe CCM madarakani.

Hata hivyo, Makalla kwenye maelezo yake amesema: “Mabadiliko yanafanywa na vyombo vya sheria. Kuna Bunge. CCM tunajiandaa na uchaguzi, na hatuwezi kuelekezwa au kutokee mmoja aseme hakuna mageuzi, hakuna uchaguzi. Mimi naamini wana ajenda ya siri; hawana fedha ya uchaguzi na hawajajipanga.”

Makalla amesema kinachofanywa na watu hao ni kwa sababu hawajajipanga na wanatafuta visingizio. Mabadiliko yapo na kutakuwa na Tume Huru ya Uchaguzi safari hii.

“Hakuna watu kupita bila kupingwa. Hayo ni mabadiliko makubwa hayakuwepo, na kama hayo maelekezo hayawezi kuelekezwa kama matamko, tuna vyama 18 vimesajiliwa. Hatuwezi kusema chama kimoja kina uwezo wa kuelekeza au kulazimisha,” amesema.

Katika hotuba yake, Wasira amelitaka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuongeza jitihada katika kuboresha miundombinu ya kusafirisha umeme ili wananchi wapate umeme wa uhakika wakati wote, kwa kuwa Serikali imeshajenga Bwawa la Mwalimu Nyerere.

“Matatizo madogomadogo yanayosababisha umeme kukatika mara moja moja ni tatizo la miundombinu tu, si matatizo ya uzalishaji umeme. Tunaomba Tanesco waweke kasi katika kurekebisha mitandao yao ili watu wapate umeme wa uhakika,” amesema.

Wasira amesema ujenzi wa bwawa hilo umefikia asilimia 99. Kukamilika kwake, utazalisha umeme megawati 2,215, na kilichobakia ni kufunga mashine tatu na kuanza uzalishaji huo.

“Kilichobakia ni kufunga mashine tatu na kuanza kuzalisha umeme megawati 2,215. Najua Dar es Salaam tulikuwa tunapata matatizo ya mgao, lakini wengi walikuwa hawaelewi. Kulaumu ni kazi nyepesi kuliko kufanya,” amesema.

Msingi wa hoja hiyo ni malalamiko ya wananchi wa maeneo mbalimbali nchini kuhusu kukatika kwa umeme mara kwa mara na kuwasababishia adha.

Akielezea utekelezaji wa Ilani ya CCM, Wasira amesema mradi wa mabasi ya mwendo haraka njia ya Mbagala utaanza kabla ya Machi 30, 2025, huku akisema lengo ni kuwaondolea adha wananchi wa mkoa huo.

“Hakuna sehemu yenye watu wengi kama Mbagala. Kila ukifika, unaweza kusema kuna mkutano, kumbe wako kazini kwao. Kila siku wanakuja Kariakoo na kurudi. Kazi ya kuwajengea miundombinu imekamilika, na Machi 30, 2025, tutaanza kuona mabasi yakienda na kuondoa tatizo,” amesema Wasira.

“Tunajenga miundombinu ya usafiri kwenda Gongo la Mboto. Ikifika Juni mwaka huu, mabasi yataanza kwenda Gongo la Mboto. Ni eneo la pili kwa uwingi wa watu ikitoka Mbagala,” amesema.

Licha ya Wasira kutoa ahadi hiyo, barabara hiyo ya Mbagala yenye urefu wa kilomita 20.3 inayotoka katikati ya Mji hadi Rangitatu imekuwa ikipigwa danadana nyingi kuhusu siku rasmi ya kuanza mabasi kazi. Viongozi wa Serikali na CCM wamekuwa wakitoa ahadi ambazo mpaka sasa hazijatekelezwa.

Vilevile, Serikali ilitoa tangazo kwa umma Desemba 2024 ikizialika kampuni za usambazaji gesi asilia kuomba zabuni ya usambazaji wa nishati hiyo kwa mabasi 755 yanayotoa huduma hiyo kwa mradi wa awamu ya pili.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mwisho wa kuwasilisha maombi ya zabuni hizo ni kabla ya Januari 29, mwaka huu.

Awali, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, John Mongella amesema kama wasaidizi wake watahakikisha Wasira anatekeleza majukumu yake ipasavyo, huku akieleza wengi ni vijana.

“Niseme tu, Mwenyekiti alitupanga vijana (Rais Samia Suluhu Hassan), na alituelekeza. Aliona uje wewe (Wasira) ili usimamie na kutuelekeza. La sivyo, moto ambao wangeuona ingekuwa balaa,” amesema Mongella.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kutoka Dar es Salaam, Juma Simba Gadafi, amesema mkoa huo utaendelea kuwa ngome ya chama hicho, na kazi wanayoiona mbele yao ni kuhakikisha wanatoka na mtaji wa kura za kutosha.

Related Posts