WASIRA: UAMUZI WA MKUTANO MKUU UMEZINGATIA KATIBA YA CCM

 Na Mwandishi Wetu

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mainduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amesema uamuzi wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM, uliomchagua Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kugombea kiti cha Urais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, umezingatia takwa la kikatiba na mamlaka ya Mkutano Mkuu.

Amesema baadhi ya watu wanaojiita wanaCCM wanaodai kwamba bado hawajaelewa sababu ya wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM kupitisha uamuzi huo, atawasaidia kuelewesha kwani uwezo wa binadamu kufahamu jambo hauwezi kulingana.

Akizungumza leo Januari 26,2025 jijini Dar es Salaam wakati viongozi, wanachama,  wapenzi wa CCM na wananchi kutoka maeneo mbalimbali walipojitokeza kumpokea,Wasira ametumia nafasi hiyo kueleza uamuzi wa Mkutano Mkuu kupitisha jina la Dk.Samia kuwa mgombea urais katika uchaguzi mkuu mwaka huu,

“Baada ya Mkutano Mkuu kutambua kazi kubwa zilizofanywa na serikali zote mbili, Serikali ya Muungano na Serikali ya Zanzibar, Mkutano Mkuu wa CCM ukasema kama hali ni hii kuna sababu gani kuchelewesha kutangaza mgombea?.

“Sasa wapo watu wanaosema wao ni wanachama wa CCM, hawakuelewa. Hilo nalo siyo jambo la ajabu. Tutawasaidia kuelewa maana siyo watu wote wanaweza kuelewa sawa. lakini tunawaambia Mkutano Mkuu kwa mujibu wa Katiba ya CCM ndiyo kikao kikuu cha mwisho,” amesema.

Wasira ameeleza kuwa Mkutano Mkuu wa Chama una mamlaka ya kubadili, kufuta na kurekebisha uamuzi wowote uliofanywa na kikao cha chini yake, kufuta maamuzi yaliyofanywa na kiongozi yeyote wa CCM.

Amesisitiza: “Sasa aliye na mashaka katika jambo hilo kama wote hawawezi aje kwangu nitamsadia maana katiba ipo kichwani. Uamuzi tulioufanya umezingatia Katiba ya CCM ibara ya 101 inayotutaka tuchague jina moja la kuwa mgombea wa kiti cha Urais, tulitumia ibara hiyo na kwa mamlaka ya Mkutano Mkuu ameteuliwa Dk. Samia.”






Related Posts