Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (World Food Programme -WFP) limesema litaendeleza ushirikiano na Kampuni ya Meli Tanzania (Tashico) katika eneo la usafirisaji wa shehena ya vyakula kutoka Bandari ya Dar es Salaam na Mwanza mpaka Sudan Kusini.
Wawakilishi wa WFP kutoka makao makuu yaliyopo Roma, Italia wametembelea makao makuu ya Tashico jijini Mwanza ili kufanya tathmini ya ushirikano waliouanzisha takribani kwa miaka 10.
Ugeni huo kutoka WFP ulipata fursa ya kutembelea meli ya MV Umoja, ambayo ilikuwa ikitumika kusafirisha shehena ya vyakula kutoka Bandari ya Mwanza nchini Tanzania kwenda Sudani Kusini kupitia Uganda.
Akizungumza baada ya kutembelea meli ya MV Umoja katika Bandari ya Mwanza jana , Ofisa Ufuatiliaji na Tathmini wa WFP , Sala Maharenovic amesema kuwa wamekuja kufanya tathmini ya ushirikiano walioingia na Kampuni ya Meli Tanzania wakati huo ikijulikana kama Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL).
Amesema kuwa ushirikiano walioanzisha umekuwa wenye tija ambapo wamekuja kufanya tathmini ya ushirikiano kati yao na wadau wao ambapo mmoja ya wadau wakubwa akiwa ni Tashico.
“Mazungumzo haya ya pamoja ni muhimu katika kupata tathimini ya kina na kuelewa ni mahitaji gani yanayohitajika sasa ili kuboresha zaidi uhusiano wetu kwa pamoja WFP na Kampuni ya Meli Tanzania,” amesema ofisa huyo mwandamizi wa WFP.
Baada ya kupokea ugeni kutoka makao makuu ya WFP, Mkurugenzi Mtendaji wa Tashico, Eric Hamissi amesema: “Nimefurahi kupokea ujumbe huu wa WFP ambao wamekuja kutembelea katika makao makuu ya kampuni yetu, hii inaendelea kukuza mahusiano mema tuliyoaanzisha. TASHICO imekuwa na uhusiano wa karibu sana wa kikazi na WFP kwa miaka mingi. Nakumbuka wakati huo meli yetu kubwa ya mizigo ya MV. Umoja ilikuwa ikifanya kazi kwa kusuasua lakini tuliweza kupata shehena nyingi za mizigo kutoka kwa wadau wetu hawa kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Mpango wa Chakula Duniani.”
Aliongezea: “Ujio wa timu hii ni mwanzo wa kuona namna ya kurejesha usafirishaji shehena ya mizigo kutoka kwao. Meli ya MV. Umoja ilisimama kufanya kazi mwaka 2019 na Serikali ilitoa Sh19.5 bilioni mwaka 2021 kwa ajili ya ukarabati mkubwa na hatimaye tayari imerejea,”
Mkuu wa Kitengo cha usafirishaji na ugavi wa WFP Tanzania, Mamoud Mabuyu amesema: “Tumekuja hapa na ugeni kutoka makao makuu ya shirika letu yaliyopo Roma, Italia ambapo wamekuja kufanya tathimini kuangalia ni jinsi gani ambavyo tunafanya kazi na washirika wetu kwenye eneo la usafirishaji ambapo Tashico ni mmoja wa washirika wetu wakubwa.”
“Ugeni huu umekuja baada ya miaka 10 ambayo tumefanya kazi pamoja na Tashico hivyo tathimini itaweka wazi ni kiasi gani uhusiano wetu umekuwa na faida kwetu sisi na kwa mashirika ambayo tunafanya nayo kazi na nchi kwa ujumla, na vile vile kupendekeza nini cha kufanya baada ya hapa,” amesema.
Naye Eugenia Punjila, Ofisa Masoko Mkuu wa Tashico, amesema kuwa WFP wamekuwa wakisafirisha shehena ya chakula na mahitaji mengine ya msaada kupitia meli kwenda nchini Sudani Kusini kupitia Uganda.
“Tunaishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza zaidi kwa Tashico kwa wakati huu ambapo tunakabiliana na shehena kubwa,” amesema.
Naye, Nahodha mkongwe wa meli ya MV Umoja, Bembele Samson N’gwita amesema hivi sasa kuna mabadiliko makubwa baada ya ukarabati mkubwa kwenye meli hiyo tofauti na ilivyokuwa miaka 10 iliyopita.
Tashico ni taasisi ya Serikali iliyoanza kazi zake mwaka 1961 chini ya jina la TRC Marine Division, ikiwa na ari kubwa ya kuendeleza sekta ya meli nchini na hadi sasa imetekeleza miradi kadhaa madhubuti.
Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na ukarabati wa meli zilizochakaa, ujenzi wa meli mpya pamoja na kuboresha usafiri wa majini nchini Tanzania, hasa katika maeneo muhimu yenye wakazi wengi wa maziwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa.