Dar es Salaam. Wakati Bara la Afrika likielekea katika utekelezaji wa Agenda 300 Afrika inayolenga kuwafikia Waafrika milioni 300 kwa umeme, baadhi ya mashirika ya fedha na nishati yameahidi kutoa fedha kufadhili miradi ya ajenda hiyo.
Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni 600 Afrika hawana uhakika wa kupata nishati ya umeme, hali inayodidimiza maendeleo ya uchumi barani humo.
Ahadi hizo zimetolewa leo Jumatatu, Januari 27, katika mkutano wa nishati wa Afrika unaofanyika jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika mjadala ambao ni sehemu ya mkutano huo wa siku mbili, Mtendaji Mkuu wa Mpango wa 300 (M300) wa taasisi ya Rockefeller, Andrew Herscowitz, amesema wamekuwa wakishirikiana na Global Energy na Benki ya Maendeleo ya Afrika kutekeleza miradi ya umeme 23.
“Tunaleta wadau wa maendeleo kuhakikisha sekta binafsi inaingia katika mradi huo,” amesema.
Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Rémy Rioux, amesema katika mpango huo wanakusudia kuwekeza Euro bilioni 2 (Sh5.34 trilioni).
“Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, anaunga mkono juhudi hizi. Alikutana na Rockefeller na nafikiri atajitoa zaidi katika mkutano wa kesho wa wakuu wa nchi za Afrika,” amesema.
Ameongeza kuwa watatoa misaada zaidi kuzijengea uwezo sekta za umma na sekta binafsi.
Ahadi nyingine imetolewa na mwakilishi wa Benki ya Uwekezaji wa Miundombinu ya Asia (AIIB), Jin Liqun, akisema wamekuwa wakifadhili nishati duniani kote na sasa wanajikita Afrika.
“Hapa nitoe ahadi kwamba tutachangia Dola bilioni 1.5 (Sh4 trilioni) kwa ajili ya kuunga mkono ajenda hii. Hizi tunaanza nazo, lakini tutaendelea kuchanga fedha zaidi na ninapenda tuzielekeze Afrika na hasa Ajenda 300,” amesema.
Ameeleza sababu ya kufadhili miradi ya Afrika, akisema ni matumaini ya bara hilo kuja kuwa kitovu cha viwanda.
“Kwa karne ya 21, nchi za Afrika zitakua zilizoendelea, zitakuwa ni kitovu cha viwanda na nchi zinazoendelea.
“Kwa sasa kuna operesheni kule Ivory Coast, Rwanda na kuna mradi mkubwa unaoandaliwa kwa nchi hizo. Tunatarajia kuwa na miradi nchini Ethiopia, Kenya, Senegal,” amesema.
Gavana wa Benki ya Maendeleo ya Kiislamu, Muhammad Sulaiman Al Jasser, amesema watachangia Dola bilioni 2.6 (Sh6.94 trilioni).
“Sisi, Benki ya Maendeleo ya Kiislamu, tunaahidi Dola bilioni 2.6, ambapo Dola bilioni moja bilioni itakuwa kwa ajili ya benki, Dola milioni 150 itakuwa kwa sekta binafsi na nyingine zitakuwa kwa ajili ya taasisi ya mikopo na mfumo wa dhamana na bima,” amesema.
Amesema benki hiyo yenye wanachama 57, ambapo wanachama 27 wako Afrika, imewekeza Dola bilioni 7.7 kwenye miradi ya umeme duniani, ambapo nchi za Afrika zimepata Dola milioni 33.
“Kwa Afrika peke yake tumekuwa na miradi 622 ya nishati tukishirikiana na AfDB, sekta binafsi,” amesema.
Amesema tatizo la kukosa umeme lilijidhihirisha zaidi wakati wa janga la Uviko 19, ambapo watoto bilioni 1.5 hadi bilioni mbili walishindwa kupata elimu kwa kukosa intaneti.
Mwakilishi wa Shirika la uzalishaji wa mafuta ya Petrol (Opec), Dk Abderrahman Khene, amesema Opec watatoa Sh2.67 trilioni.
“Tutatathmini hali ilivyo, ambapo kufikia mwaka 2027 kama maendeleo yatakuwepo na kama nchi zitakuja na mpango endelevu tutaongeza nyingine Dola bilioni moja kwa ajili ya Ajenda 300,” amesema.