Towana Looney, mwanamama kutoka Alabama nchini Marekani ameingia kwenye rekodi baada ya kupandikizwa figo ya nguruwe ambapo mpaka sasa, zikiwa zimepita siku 61 tangu afanyiwe upandikizaji huo, anaendelea vizuri kabisa.
Mwanamama huyo alipandikizwa figo ya nguruwe baada ya kupata matatizo ya figo zake ambapo maendeleo yake ya kiafya, yamezua gumzo kubwa duniani kote.
“Mimi ni superwoman,” alisema Towana wakati akizungumza na Shirika la Habari la Associated Press jijini New York.
Kabla ya Towana kufanyiwa upasuaji huo wa kupandikiza figo, Wamarekani wengine wanne walishafanyiwa upasuaji wa kupandikiza viungo kutoka kwa wanyama, wawili wakiwa wamefanyiwa upasuaji wa kupandikiza moyo wanguruwe na wawili wakiwa wamefanyiwa upandikizaji wa figo za nguruwe lakini kati yao, hakuna aliyeishi zaidi ya siku 60.
“Ukimuona mitaani, hauwezi kabisa kufikiria kwamba yeye ndiye binadamu pekee duniani ambaye anatembea akiwa na figo ya nguruwe ndani ya mwili wake, tena inayofanya kazi vizuri,” alikaririwa Dokta Robert Montgomery kutoka NYU Langone Health ambaye ndiye aliyeongoza upasuaji huo.