Dar es Salaam. Wakati madereva wa bajaji wakitii agizo la Jeshi la Polisi kutoingia katikati ya jiji la Dar es Salaam, hali ni tofauti kwa baadhi ya waendesha pikipiki maarufu bodaboda wameonekana wakikatisha baadhi ya maeneo.
Januari 25, 2025, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu lilitangaza kufungwa kwa barabara tisa sambamba na barabara nyingine tisa kwa muda kupisha misafara ya viongozi mbalimbali wanaokuja kutoka nchi mbalimbali kuhudhuria mkutano wa nishati Afrika. Sambamba na hilo, Polisi iliagiza bajaji na bodaboda kutoingia katikati ya jiji katika kipindi chote ambacho mkutano huo unafanyika.
Mkutano huo unaofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Januari 27 hadi Januari 28, 2025, unatarajiwa kuhudhuriwa na marais 25 na mawaziri 60 kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
Hata hivyo, timu ya Mwananchi iliyopita katika maeneo mbalimbali ilishuhudia bajaji zinazotoka maeneo ya Kimara na Mbezi zikiishia Jangwani, lakini bodaboda zilionekana zikikatiza mitaa kadhaa ya Posta na Kariakoo, ingawa kwa uchache. Baadhi ya bodaboda zilionekana zimebeba abiria waliokuwa wakiwashusha katika mitaa mbalimbali, ikiwemo ya Posta, ambapo baadhi ya barabara zilifungwa ili kupisha misafara ya marais wa mataifa ya Afrika wanaohudhuria mkutano unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JINCC).
Mmoja wa madereva wa bajaji, Aloyce Mapunda, aliiambia Mwananchi kwamba hali ya biashara si nzuri tangu polisi kutoa tangazo hilo, akisema hakuna mishemishe zinazoendelea kama zamani.
“Yaani mji umepoa tofauti na Jumamosi au Jumapili, sasa hivi abiria tunatafuta kwa tochi wale ambao hawaendi katikati ya mji. Hali si nzuri kwetu; hadi mkutano huu ukimalizika, tutakuwa tumenyooka kwa kweli,” amesema Mapunda.
Ameongeza kuwa huduma za teksi mtandao nazo zimepungua, kwani watoa huduma wanadai hakuna kazi.
“Siyo sisi, hata wale huduma za teksi mtandao nao wamezima simu maana wanasema hakuna kazi. Sijui itakuaje maana njia ya mjini ndiyo kuna faida kubwa,” amesema Mapunda.
Baadhi ya maeneo ya kwenda kwenye ukumbi wa mkutano, askari polisi wameonekana kufanya doria maeneo mbalimbali.
Mwananchi imeshuhudia askari wengine wakitembea kwa miguu mitaa ya Posta, wengine wakiwa kwenye magari, ikiwa ni hatua ya kuimarisha ulinzi.
Hata hivyo, magari yaendayo haraka maarufu mwendokasi yameonekana yakiendelea kutoa huduma ya usafiri kama kawaida, hasa kwa kwenda maeneo ya jiji kama ilivyo ada.
Katika hatua nyingine, teksi mtandao hazipatikani kirahisi kutokana na kuwa na idadi kubwa ya abiria.
Mkazi wa Magomeni, wilayani Kinondoni, Hamad Yussuf, amesema amejaribu kuita karibu mara 10, lakini hakufanikiwa hadi alipolazimika kutafuta mbadala wa kwenda eneo anapokwenda, hasa katikati ya mji.
Naye, dereva bodaboda, Daud Michael, amesema hatokwenda mjini katika siku hizi mbili za mkutano, kwani hawezi kupingana na kauli ya polisi.
“Wanaokwenda waache waende, siwezi kujitoa mhanga. Hili nalo litapita tu, nitavumilia tu kuliko kwenda na kuishia mikononi mwa polisi,” amesema Michael.