DC Mvomero aagiza Tawa kuwasaka mamba wanaoua watu, wadai kusababisha vifo 17

Mvomero. Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Judith Nguli, ameagiza Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa) kushughulikia haraka mamba wakorofi waliopo Mto Mkindo na mito mingine wilayani humo ili kudhibiti athari zaidi zinazoweza kujitokeza, ikiwemo vifo.

Ametoa agizo hilo ikiwa ni wiki moja tangu mwananchi wa kijiji cha Lukenge, kata ya Mtibwa wilayani humo, Anselem John (60), kufariki dunia baada ya kushambuliwa na mamba wakati akinawa kwenye mto huo uliopo kando mwa shamba lake baada ya kumaliza kulima.

“Taarifa za usalama wa wananchi kule kwenye mto zimekuwa ndogo kwa sababu mamba wamekuwa wakijeruhi na kuua kwa kipindi kirefu. Tayari karibu vifo vipatavyo 17 vimetokea, lakini havikuwahi kuripotiwa kwa sababu moja au nyingine, ikiwa ni pamoja na wananchi kutokujua wapi pa kwenda kutolea taarifa,” amesema Nguli.

Amesema, pamoja na changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kijijini hapo, wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari wanapokwenda kwenye mito kuchota maji, kuoga au kufanya shughuli nyingine.

Amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua za haraka, ikiwemo kurekebisha pampu ya kisima cha maji kilichokuwa kikitumika awali ili wananchi waache kwenda mtoni.

Naye Ofisa Wanyamapori kutoka Tawa, Paul Mbeya, amewaomba wakazi wa eneo hilo kutoa ushirikiano kufanikisha kubaini maeneo yenye mamba wakali kwenye mto huo ili hatua za kuwavuna zichukuliwe.

“Hili zoezi la uvunaji wa mamba tumeanza tangu mwaka jana. Lakini nafikiri kwa kutopata taarifa kutoka kijiji hiki ndiyo maana hatukufika kwa wakati. Kilosa tumevuna zaidi ya mamba nane, Ruaha, Mvuha ambayo ni Morogoro Vijijini, tumevuna mamba wengi,” amesema Mbeya.

Akizungumza na Mwananchi, Hashimu Luwinzo, shuhuda na mkazi wa kijiji hicho, amesema mtu huyo alizamishwa kwenye mto huo Januari 21, 2025, mwili wake ulipatikana alfajiri ya Januari 22, 2025, kwenye kingo za mto huo ukiwa na majeraha makubwa.

Aidha, amesema matukio ya watu kushambuliwa na mamba kwenye kijiji hicho ni ya muda mrefu bila msaada wowote, na kwamba mpaka sasa zaidi ya watu 17 wamekufa kwa kushambuliwa na mamba huku wengine wakipata ulemavu wa kudumu.

Luwinzo ameiomba Serikali kupitia Tawa kuchukua hatua stahiki, ikiwemo kuwavuna mamba wakorofi.

“Kijiji cha Lukenge kimezungukwa na mito mingi ikiwemo Mkindo, Diwale, Divule, na mto Wami. Yote hiyo imeungana katika kijiji cha Lukenge, hii mito ina tabia ya kuwa na maji kipindi cha mwaka mzima, kwa hiyo ni sehemu salama kwa mazalia na makazi ya mamba kwa muda mrefu,” amesema Luwinzo.

Amesema: “Kipindi cha mvua, mamba huwa wanatawanyika kutoka kwenye mto Wami, ambao ni mkubwa, kwenda kwenye mito midogo yenye maji mengi kama huu mto Mkindo.”

Ameongeza kuwa kuna changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwenye kijiji hicho, ambapo maji ya mto huo ndiyo tegemeo kwa matumizi ya nyumbani, kilimo, na pia shughuli za uvuvi kwa kutumia mitumbwi.

Related Posts