Dar es Salaam. Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, amesema licha ya maendeleo makubwa yaloyofanyika, bado Bara la Afrika linakutana na pengo la kufikia nishati inayohitajika kwa sababu hakuna miundombinu toshelevu.
Kukosekana kwa miundombinu hiyo ndiyo kunakochelewesha upatikanaji wa nishati inayohitajika ili kufikia maendeleo endelevu.
Amesema hayo leo Jumatatu, Januari 27, 2025, wakati akitoa hotuba katika mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika kuhusu nishati unaolenga kutoka na lugha moja itakayowezesha Waafrika milioni 300 kufikishiwa huduma ya umeme ifikapo mwaka 2030.
Dk Nchemba amesema nishati si jambo la anasa, bali ni msingi wa uchumi wa jamii na nchi kwa ujumla, hivyo ni vema kuhakikisha inapatikana ili kuwezesha mabadiliko ya kiuchumi na kupunguza umaskini kwa Bara la Afrika.
“Licha ya maendeleo makubwa ambayo Afrika imefanya, bado bara hili linakutana na pengo la kuwa na nishati inayohitajika kwa sababu hakuna miundombinu toshelevu inayowezesha kuwa na uwezo wa kufikia nishati inayohitajika ili kufikia maendeleo endelevu, ukuaji wa kiuchumi, na ubora wa maisha kwa ajili ya Waafrika,” amesema Nchemba.
Amesema licha ya nishati kuwa msingi wa uchumi wa jamii na nchi, kuna wakati kumekuwa na tabia ya kuridhika kwa kudhani kuwa umeme unatosha ikiwa sehemu ya jamii inaweza kupata nishati hiyo.
“Fikiria maisha ya siku moja bila kuwa na umeme na jaribu kufikiri maisha bila umeme kwa mwezi mmoja, pia fikiria aina ya maisha pasipo umeme kwa mwaka mmoja, pia fikiria maisha bila umeme kwa jamii ambayo haya ndiyo maisha waliyoyazoea,” amesema.
Amesema ni vyema kujua kuwa jamii yenye uwezo wa kufikia nishati safi, nafuu, na inayoaminika inasaidia kutengeneza ajira na kuwezesha jamii.
“Mnaona leo Waafrika takribani milioni 600 hawana uwezo wa kupata nishati, hii ituambie juu ya changamoto tunazokabiliana nazo katika ufikiaji na upatikanaji wa umeme kwa jamii zetu,” amesema Dk Nchemba.
Amesema katika kushughulikia changamoto hizi ni lazima kukutana kwa pamoja na kuleta rasilimali fedha, huku akizitaka taasisi za fedha kuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na suala hilo.
“Pia lazima kuunganisha nguvu ya wabia wa maendeleo, benki za biashara na wawekezaji ili waweze kugharamia miradi ya nishati,” amesema.
Miundombinu pia ni jambo la muhimu ili kuhakikisha nishati inapatikana, jambo litakalowezesha mabadiliko ya kiuchumi na kupunguza umasikini kwa Bara la Afrika.
“Tunatambua muunganiko wa mataifa ili kufikia malengo ya pamoja ya kuhakikisha watu milioni 300 wanapata umeme.
Katika haya yote amesema wadau wa maendeleo ni muhimu katika kuhakikisha kuwa pengo la kukosekana kwa umeme linapungua na kufanikisha malengo ya ajenda 300.
“Ufadhili wa kifedha na uhamasishaji rasilimali na wadau wanaweza kusaidia katika kuwa na miundo ya uwekezaji inayounga mkono ajenda 300 ili kugusa mikakati ya nchi husika.”