Fadlu ashtuka apanga jeshi kuivaa Tabora United

SIMBA jana kilikuwa uwanjani kumalizana na Kilimanjaro Wonders katika mechi ya kiporo ya Kombe la Shirikisho, lakini mapema kocha mkuu wa kikosi hicho, Fadlu Davids ikielezwa ameshtuka mapema na kuanza kulipanga jeshi alilonalo kabla ya kurejea katika mechi za Ligi Kuu Bara.

Simba inatarajiwa kuwa wageni wa Tabora United katika mchezo wa kiporo wa duru la pili utakaopigwa Jumapili ijayo kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini Tabora.

Mechi hiyo iliahirishwa mwishoni mwa mwaka jana ili kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi 2025 na fainali za Chan 2024 ambazo hata hivyo zimeahirishwa kutoka Februari hadi Agosti mwaka huu.

Inaelezwa wakati wa maandalizi ya mechi ya jana ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Kilimanjaro Wonders, Kocha Fadlu alitumia pia nafasi hiyo kuzungumza na wachezaji, kuhusu mchezo huo wa kiporo sambamba na mechi nyingine tano zitakazopigwa na timu hiyo ndani ya mwezi ujao wa Februari.

Inadaiwa, Fadlu ambaye alitua Msimbazi mwanzoni mwa msimu huu akitokea Raja Casablanca ya Morocco alikokuwa kocha msaidizi, amerejea matokeo ya mechi mbili zilizopita wa washindani hao katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu, Yanga na Azam mbele ya Tabora Utd.

Tabora ilianza kwa kuifunga Yanga kwenye uwanja wa nyumbani wa Azam Complex (enzi hizo kabla ya kuhamia KMC) kwa mabao 3-1 kisha kuizima Azam kwa mabao 2-1 mjini Tabora, mbali na kulazimisha sare ya 2-2 na Singida Black Stars timu zinazotengeneza 4 Bora sambamba na Simba katika ligi ya sasa.

Kitendo hicho cha kuzifunga Yanga na Azam na kutoka sare ya Singida inayoonekana kuimarika mno msimu huu, kimemshtua Fadlu ambaye katika mchezo wa kwanza dhidi ya Tabora ilishinda kwa mabao 3-0, huku Nyuki hao wa Tabora wakiwakosa mastaa karibu wote wa kigeni waliokuwa hawajapa vibali.

Habari kutoka ndani ya Simba zinasema kuwa, kocha Fadlu ametumia muda mwingi kuzungumza na wachezaji na kuwaeleza namna wanavyoweza kwenda kukutana na ugumu mjini Tabora katika mechi hiyo ya Jumapili, hivyo kuwataka kujipanga kwa mchezo huo na mingine ya duru la pili la Ligi Kuu.

“Kocha Fadlu anajua Tabora iliyocharazwa mabao 3-0 kwenye Uwanja wa KMC, sio wanayoenda kukutana nayo, ikiwamo aina ya wachezaji hata kocha anayeinoa timu hiyo, hivyo kazungumza na wachezaji na kuwataka kujipanga vizuri na kuhakikisha hawafanyi makosa, kulinda rekodi waliyonayo,” kilisema chanzo hicho kutoka ndani ya Simba na kuongeza;

“Ukiacha mechi hiyo, Simba ina michezo miwili migumu ugenini dhidi ya Fountain Gates na Namungo, mbali na zile za nyumbani dhidi ya Tanzania Prisons, Dodoma Jiji na Azam ambazo zote sio nyepesi na kocha hataki kuona timu inapoteza pointi yoyote, ndiyo maana amewatahadharisha wachezaji mapema.”

Inaelezwa kocha Fadlu aliyeiongoza Simba kutinga robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa imeongoza Kundi A mbele ya CS Constantine ya Algeria, hesabu zake ni kuendelea na moto ule ule aliokuwa nao tangu alipopoteza mchezo wa Dabi ya Kariakoo mbele ya Yanga Oktoba 19 mwaka jana.

Tangu ilipopoteza mchezo huo, Simba haijaonja machungu ya kupoteza wala kutoka sare katika mechi tisa za mwisho za Ligi Kuu, jambo ililoifanya irejee kileleni na kuongoza hadi sasa kwa pointi 40 baada ya kushuka uwanjani mara 15, ikiwazidi watetezi Yanga iliyo na na pointi 39 ikicheza pia idadi ya mechi 15.

Simba ikimaliza mechi hizo sita za Februari, itaifuata Coastal Union jijini Arusha Machi Mosi kabla ya kuvaana na Yanga wiki moja baadae kwenye marudio ya Dabi ya Kariakoo itakayopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza kwa bao 1-0 ikiwa wenyeji Oktoba 19.

Related Posts