DURU la pili la Ligi Kuu Bara linatarajiwa kurejea wikiendi hii kwa vigogo Simba na Yanga kula viporo walivyonavyo dhidi ya Tabora United na Kagera Sugar, huku kocha wa Wekundu wa Msimbazi, Fadlu David akiwa katikati ya mtego wa Yanga katika mbio za ubingwa za msimu huu.
Simba inayoongoza msimamo wa Ligi hiyo ikiwa na pointi 40 kutokana na kucheza mechi 16 itakuwa ugenini Jumapili kuvaana na Tabora United, wakati watetezi Yanga itakuwa kwenye uwanja wa nyumbani wa KMC Complex kuikaribisha Kagera Sugar.
Kocha wa Simba, Fadlu anapiga hesabu kali sana kuhakikisha duru la pili wa Ligi Kuu anakata kiu ya Wanasimba katika suala zima la kubeba ubingwa.
Simba imeukosa ubingwa wa ligi hiyo kwa misimu mitatu mfululizo ambapo Yanga imekuwa ikitawala. Tangu mara ya mwisho Simba ilipokuwa bingwa msimu wa 2020-2021 wakati ligi ikishirikisha timu 18, hadi leo imekuwa ikipambana lakini haitoboi mbele ya Yanga.
Kumbuka kabla ya hapo, Simba ilibeba ubingwa wa ligi hiyo misimu minne mfululizo wakati ambao Yanga ilikuwa ikiumiza vichwa kupindua utawala huo, ikafanikiwa.
Katika kuweka sawa hesabu za ubingwa, Fadlu ambaye huu ni msimu wa kwanza kuinoa Simba amekamilisha duru la kwanza kwa kukaa kileleni kwa tofauti ya pointi moja dhidi ya Yanga inayoshika nafasi ya pili.
Simba iliyobeba ubingwa wa ligi hiyo mara 22, imekamilisha mzunguko wa kwanza kwa kukusanya pointi 40 baada ya kushinda mechi 13 na sare moja ikipoteza mechi moja pia.
Mtihani alionao Fadlu ambao watangulizi wake walishindwa kupambana na Yanga na kupoteza ubingwa ni katika mzunguko wa pili ambao umekuwa na changamoto nyingi kwani unatajwa kuwa ndiyo wakati wa kila timu kutolea macho ili kufanikisha malengo.
Unaweza kukuta mzunguko wa kwanza timu zinapoteza pointi kirahisi, lakini mzunguko wa pili zinakaza kwani zinafahamu baada ya hapo hakuna tena muda wa kujiuliza.
Katika kuthibitisha hilo, mzunguko wa pili timu pia huimarisha vikosi vyao kwa kufanya usajili kipindi cha dirisha dogo, lengo likiwa ni kuziba mapengo yaliyojitokeza na kutotoka nje ya hesabu.
Sasa basi, Fadlu aliyebeba matumaini ya Wanasimba katika kubeba ubingwa msimu huu, baada ya kufanikiwa kwa kiasi fulani mzunguko wa kwanza, kazi bado haijaisha, ana jukumu la kurekebisha makosa ambayo wenzake waliyafanya mzunguko wa pili katika misimu mitatu nyuma ili kurudisha furaha Msimbazi.
Katika misimu mitatu nyuma, Simba ilikuwa haijawahi kumaliza mzunguko wa kwanza ikiwa na pointi 40, kitendo cha msimu huu kufikisha pointi hizo, imeonekana ni kikwazo cha kwanza ambacho Fadlu amekivuka na kuleta mwanga mpya wa kufikia mafanikio.
Ilionekana Simba kinachowakwamisha zaidi ni matokeo ya mechi za ugenini kitu ambacho msimu huu wamekifanyia kazi mzunguko wa kwanza ikifanikiwa kushinda mechi zote saba ikikusanya pointi 21, hakuna msimu ambao imefanya hivyo jambo ambalo lilichangia kuwakosesha ubingwa.
Msimu wa 2021-2022, katika mechi saba za ugenini, Simba ilikusanya pointi 11 kati ya 21 ambapo ilipoteza pointi 10. Msimu wa 2022-2023 mzunguko wa kwanza ilicheza mechi nane ugenini na kukusanya pointi 15 kati ya 24, ikapoteza pointi 9. Msimu uliopita 2023-2024 ilijitahidi kidogo kwani katika mechi nane za mzunguko wa kwanza ugenini ilikusanya pointi 22 kati ya 24, ilipoteza pointi mbili pekee, kumbuka msimu huo ilimaliza ligi nafasi ya tatu wakati misimu miwili nyuma ilikuwa ya pili.
Ukiweka kando mechi za ugenini, nyumbani Simba msimu huu imeshuka dimbani mara nane ikikusanya pointi 19 kati ya 24 baada ya kupoteza mechi moja dhidi ya Yanga (1-0) na sare ya 2-2 dhidi ya Coastal Union.
Kwa misimu mitatu nyuma ambayo Simba ilipambania ubingwa na kushuhudia Yanga ikiondoka na kicheko, timu hiyo mechi za mzunguko wa kwanza nyumbani nazo zilikuwa na changamoto kwa kiasi fulani ingawa zilikuwa bora kulinganisha na msimu huu.
Rekodi zinaonyesha msimu wa 2021-2022, Simba ilicheza mechi nane za mzunguko wa kwanza nyumbani na kukusanya pointi 20 kati ya 24. Msimu wa 2022-2023 mechi saba zenye pointi 21, Simba ilipata 19 wakati msimu wa 2023-24 katika pointi 21 za nyumbani ikicheza mechi saba, iliambulia 14. Ukiangalia takwimu hizo kulinganisha na msimu huu, utagundua Simba imekuwa bora zaidi ugenini huku nyumbani bado kuna changamoto kidogo.
Kipengele cha kwanza Fadlu amefaulu baada ya kufikisha pointi 40 mzunguko wa kwanza ambazo hazikuwahi kufikiwa na timu hiyo katika misimu mitatu nyuma. Kilichobaki sasa ni hesabu za mzunguko wa pili.
Hesabu hizo za mzunguko wa pili zinaendana sambamba na zile za misimu mitatu nyuma Simba ilifanyaje na nini kiliikamisha katika kubeba ubingwa.
Msimu wa 2021-2022 katika mechi 15 za mzunguko wa pili, Simba ilikusanya pointi 30 kati ya 45 ambapo ilidondosha 15 na kuwafanya kumaliza ligi nafasi ya pili na kupoteza taji lao ililokuwa ikilitetea ikishuhudia Yanga ikiwa bingwa.
Katika mechi 15 za mzunguko wa pili, Simba ilishinda nane, sare sita na kupoteza moja. Ugenini Simba ilicheza mechi nane na kukusanya pointi tisa kati ya 24 wakati nyumbani ikikusanya pointi 21 katika mechi saba ikimaanisha kwamba ilishinda zote. Hapa mechi za ugenini ziliwaangusha.
Msimu wa 2022-2023 Simba ilishinda mechi 12 kati ya 15 za mzunguko wa pili ikitoka sare tatu, haikupoteza ikikusanya pointi 39 kati ya 45. Kumbuka pointi hizo ndizo ambazo Yanga imekusanya msimu huu mzunguko wa kwanza. Kidogo hapa ilionekana kukaza lakini kutofanya vizuri mzunguko wa kwanza kuliwaangusha. Msimu huo mzunguko wa pili mechi nane za nyumbani ilikusanya pointi 22 kati ya 24 wakati za ugenini ikipata 17 kati ya 21.
Lakini msimu wa 2023-2024, Simba katika mzunguko wa pili ilikusanya pointi 33 kati ya 45 katika mechi 15 ikishinda 10, sare 3 na kupoteza 2. Nyumbani ilikusanya pointi 21 katika mechi 8 wakati ugenini ikiambulia pointi 12 katika mechi 7.
Katika msimu wa 2021-22, Yanga mzunguko wa pili ilikusanya pointi 35 zikiwa ni tano zaidi ya zile za Simba. Kumbuka mzunguko wa kwanza msimu huo Yanga ilimaliza na pointi 39 kama ilivyo sasa. Pia msimu wa 2022-23 Yanga ilimaliza mzunguko wa pili kwa kukusanya pointi 40 ambazo Simba imekusanya msimu huu mzunguko wa kwanza. Wakati huo Yanga mzunguko wa kwanza ilimaliza na pointi 38. Msimu wa 2023-2024 Yanga ilimaliza mzunguko wa pili kwa kupata pointi 40 sawa na zile ilizomaliza nazo mzunguko wa kwanza.
Kutokana na takwimu hizo, Fadlu hana budi kupambana pia mzunguko wa pili angalau kufikisha pointi kama ambazo amekusanya mzunguko wa kwanza ili kuwa na uhakika wa ubingwa kwani wapinzani wao wa karibu sana, Yanga wanaweza kuharibu shughuli wakati wowote.
Kama kocha Fadlu anataka kupata ramani nzima ya ubingwa msimu huu ni kupata ushindi katika pambano la Dabi ya Kariakoo litakalopigwa siku ya Wanawake Duniani, Machi 8 mwaka huu baada ya awali kupoteza kwa bao 1-0 la kujifunga la beki Kelvin Kijili.
Katika mchezo huo wa kwanza, uliopigwa Oktoba 19 mwaka jana Fadlu aliivaa Yanga iliyokuwa chini ya kocha Miguel Gamondi aliyetimuliwa baada ya kupoteza mechi mbili mfululizo za ligi hiyo mbele ya Azam iliyowachapa 1-0 na ile ya Tabora United iliyopigwa mabao 3-1.
Fadlu sasa atavaana na Yanga inayonolewa na Sead Ramovic aliyekuja na falsafa ya Gusa Achia Twende Kwao ambayo imekuwa ikiwataabisha wapinzani kwa kupewa dozi za maana katika ligi hiyo, kwani katika mechi tano chini ya kocha huyo, Yanga imeshinda zote na kuvuna jumla ya mabao 18 na yenyewe kufungwa mawili.
Walioanza kuonjeshwa Gusa Achia ilikuwa ni Namungo iliyofungwa mabao 2-0 ikiwa kwao mjini Ruangwa kabla ya Mashujaa kulala 3-2, Tanzania Prisons (4-0), Dodoma Jiji (4-0) na Fountain Gates (5-0), huku katika Kombe la Shirikisho hatua ya 64 Bora, Copco ya Mwanza ilikuwa mabao 5-0.
Hata hivyo, Fadlu anabebwa na rekodi tamu, kwani tangu Simba ilipochapwa bao 1-0 na Yanga, haijapoteza tena mchezo wowote kati ya tisa ya Ligi Kuu, ikishinda yote na kuirejesha kileleni.