Kibaha. Rais Samia Suluhu Hassan ameupandisha Mji wa Kibaha, Mkoa wa Pwani, kutoka Halmashauri na kuwa Manispaa lengo likiwa ni kukuza hadhi ya maeneo ya kiutawala na kuboresha huduma kwa wananchi.
Halmashauri ya Mji wa Kibaha ilianzishwa Septemba 2004, na shughuli za kiuchumi za wananchi waishio humo ni ujasirimali, kilimo, ufugaji, huku baadhi wakiwa ni wafanyakazi wa umma na wengine katika sekta binafsi.
Uamuzi wa kupandishwa hadhi umetangazwa leo, Jumatatu, Januari 27, 2025, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa, kwenye mkutano wa CCM Mkoa wa Pwani. Lengo la mkutano huo lilikuwa ni kuunga mkono azimio la chama hicho la kumpitisha Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea urais wa CCM katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
“Leo Rais Samia ameipandisha Halmashauri ya Mji wa Kibaha kuwa Manispaa na hii inatokana na maendeleo yanayoonekana kufanyika ndani ya eneo hili, hasa ujenzi wa miundombinu muhimu kwa jamii,” amesema Mchengerwa huku akishangiliwa.
Mchengerwa amesema kutokana na kupandishwa hadhi kuwa Manispaa, matarajio ni kwamba bajeti yake itaongezeka, jambo ambalo ni faraja kwa wananchi wa Kibaha.
“Kibaha ni makao makuu ya Mkoa wa Pwani, ni eneo muhimu sana, na ndio maana tumekuwa tukipeleka ombi kwa Rais ili aipandishe iwe Manispaa na hatimaye leo amekubali kuipandisha,” amesema.
Amesema katika kuendelea kuboresha miundombinu ndani ya mwaka huu, Serikali inatarajia kuanza ujenzi wa barabara za njia nane kuanzia Kibaha hadi Chalinze, jambo litalewawezesha kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kibaha Mjini (CCM), Selvestry Koka, amesema kupanda hadhi kwa halmashauri hiyo kumetokana na maendeleo yaliyopo, hasa katika miundombinu ya barabara, majengo ya shule, na huduma za afya, na kwamba wataendelea kuhakikisha wanazifanyia kazi changamoto zilizobaki.
“Ushahidi unaonyesha mazingira hasa kwenye miundombinu iliyojengwa hivi sasa; barabara zimejengwa nyingi na zinaendelea kujengwa, na hata changamoto za maji tunaendelea kuzifanyia kazi ili kuhakikisha wananchi wanaishi kwenye mazingira bora,” amesema.
Awali, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani, Mwinsehe Mlao, amesema kwa sauti moja, wanachama wamekubaliana kuunga mkono maazimio ya mkutano mkuu wa CCM uliofanyika hivi karibuni jijini Dodoma, kwa kupitisha jina la Rais Samia kuwa mgombea pekee wa kiti cha urais kupitia chama hicho.
Wakizungumzia hatua ya Mji huu kupanda hadhi na kuwa Manispaa, baadhi ya wakazi wa Kibaha wamesema ni vema hatua hiyo ikaendana na uboreshwaji wa huduma za kijamii, ikiwemo maji na afya.
“Tunashuhudia ujenzi wa miundombinu ya barabara umefanyika na unaendelea kufanyika kwa baadhi ya maeneo, ushauri ni kwamba waendelee kutekeleza miradi hiyo ili kuendelea kuboresha Mji,” amesema Lucy John.
Allen Mkomwa, amesema anaamini kupanda hadhi halmashauri hiyo kuwa manispaa kutawezesha ongezeko la bajeti kutoka serikalini, jambo litakaloweza kuharakisha ukamilishaji wa miradi ya maendeleo.