Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Chadema (Bazecha), Susan Lyimo amesema katika uongozi wake atapigania kutungwa kwa sheria ya wazee ili kulinda maslahi na heshima yao katika jamii.
Lyimo amebainisha hayo leo Januari 27, 2027 jijini Dar es Salaam wakati wa mahojiano maalumu na Mwananchi, zikiwa zimepita wiki mbili tangu alipochaguliwa kuwa mwenyekiti wa baraza hilo, nafasi atakayoitumikia kwa miaka mitano ijayo.
Mbunge huyo wa zamani wa chama hicho, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bazecha Januari 13, 2025 na wajumbe wa mkutano mkuu wa baraza hilo, akimshinda mpinzani wake Hashimu Juma aliyekuwa akitetea nafasi.
Amesema Sera ya Wazee imekuwepo tangu mwaka 2003, sasa miaka 22 imepita sheria hiyo ikiwa bado haijatungwa, ndiyo maana anaona wazee wakiendelea kudhalilika, kuuawa, kutotendewa haki, kukosa pensheni na kutoweza kufanya chochote.
“Imechukua muda mrefu sana kutunga sheria ya wazee, hilo nitalipambania kwa nguvu sana, nataka wazee wazeeke kwa heshima, wafurahie uzee wao na siyo kupata tabu katika umri mrefu waliojaliwa,” amesema.
Ameongeza kuwa wazee ni moja ya makundi yaliyo hatarini katika jamii kama ilivyo kwa watoto na wanawake, lakini makundi mengine yana sheria zinazoangalia ustawi na maslahi yao isipokuwa wazee ambao wameachwa.
Lyimo amebainisha kwamba wazee wengi ni tegemezi na huko vijijini wanatumia kuni kwa ajili ya kupikia, hivyo wanauawa kwa sababu wana macho mekundu kutokana na matumizi ya kuni, jambo linalowaweka kwenye hatari zaidi.
“Sera ya Wazee imetungwa tangu mwaka 2003, namna gani hawa wazee waenende, namna gani tuwashughulikie wazee, ndiyo sababu wazee walioajiriwa wanapata pensheni lakini wenzetu Zanzibar wazee wote wanalipwa pensheni.
“Tunataka tuwe na sheria sasa…tuliipambania sana tulipokuwa bungeni lakini ilishindikana, wakasema wataleta muswada, hawakuleta. Kinachotokea ni kwamba kama hakuna sheria, maana yake ni kwamba hawa wazee wanaodhalilishwa hawana pa kusemea,” amesema.
Ameongeza kuwa wanataka kuwa na sheria ambayo itawatambua wazee, itatambua mahitaji yao na kubainisha namna ya kuwahudumia wazee hao, sambamba na kulinda maslahi yao ili waishi maisha yao yaliyobaki kwa amani, furaha na upendo.
“Kwa mfano, tunazo nyumba za wazee kule Kigamboni, Babati na Moshi, lakini ukienda kuangalia wale wazee, chakula wanachokula, mahali wanapolala, hapafai.
“Wazee hawa wameona mambo mengi, ndiyo kumbukumbu ya historia ya maisha ya jamii, hivyo watunzwe ili jamii ipate kujifunza mambo mengi kutoka kwao,” amebainisha Lyimo ambaye alikuwa makamu mwenyekiti wa Bazecha.
Amesema atafanikisha jambo hilo kwa kupeleka muswada bungeni kwa kuwa kuna nafasi ya kuwasilisha muswada hata kwa watu wasiokuwa wabunge, hivyo anaamini kwamba watatumia fursa hiyo pamoja na kuwatumia wabunge wengine wa upinzani ili wauwasilishe.
Nafasi ya mwanamke Chadema
Akizungumzia nafasi ya mwanamke ndani ya Chadema hasa katika safu ya uongozi wa juu, amesema ni jambo linalomuumiza kwa sababu vyama vingine vyote vina wanawake katika nafasi ya juu.
“Nilitegemea kwenye nafasi za juu, acha nafasi za uchaguzi, basi hata zile za uteuzi za watendaji wakuu kwa maana ya katibu mkuu na manaibu wake.
“Mimi nilikuwa mstari wa mbele kulisemea hili na siku ya uchaguzi wa mwenyekiti wa chama, nilimfuata mwenyekiti Mbowe na Lissu, nikakaa katikati yao, nikawaomba wakati mnasubiri matokeo yenu, ninaomba mnapofanya uteuzi mtuletee mwanamke japo mmoja,” amesema.
Amesema ni dhana potofu kuona kwamba wanawake hawawezi kusimama kwenye majukwaa kwa sababu ni wanawake haohao ndiyo wamekuwa wakisimama kwenye majukwaa kwenye ubunge na nafasi nyingine.
“Hoja hapa ni mfumo dume ambao sijajua ni kwa sababu gani wanauendekeza. Wanawake haohao ndiyo wanatumika. Ukiangalia Baraza la Wanawake limekuwa mstari wa mbele sana kwa ajili kukipaisha chama.
“Hilo ni jambo tutaendelea kulihoji na kuwauliza viongozi wetu, kwa maana hiyo tutamuuliza Mheshimiwa Lissu (mwenyekiti wa Chadema) na Mheshimiwa John Heche (makamu mwenyekiti), kwa sababu gani hawawapi nafasi,” amesema.
Lyimo amesisitiza kwamba wanawake wenye sifa wapo wa kutosha kwani wamekuwa wakikitumikia chama kwenye nafasi nyingine na wameaminiwa na wanachama. Ameongeza kuwa nafasi nyingine kama za naibu katibu mkuu ni za kiutendaji, hivyo wanazimudu.
Lyimo amepongeza namna uchaguzi wa Chadema ulivyofanyika kwa uwazi kila mtu akifuatilia, huku akisema kilichomfurahisha zaidi ni namna aliyekuwa mwenyekiti, Mbowe alivyokubali matokeo mapema, jambo ambalo halijazoeleka.
“Si rahisi kwa mtu aliyekuwa kwenye kiti akaondoka hivi hivi, lakini yeye alikubali, alifanya kitendo cha kiungwana sana. Kwa kweli mwenyekiti mstaafu anastahili maua yake, anastahili heshima kubwa sana, ni mwanadiplomasia wa hali ya juu.
“Ameonyesha mfano mkubwa sana na ameacha alama kubwa sana kwenye uchaguzi huu,” amesema.