Mapya sakata la Rais wa Korea Kusini

Dar es Salaam. Waendesha mashtaka wa Korea Kusini wamemfungulia mashtaka Rais Yoon Suk Yeol aliyeondolewa madarakani kwa tuhuma za kuongoza uasi na kuweka sheria ya kijeshi kwa muda mfupi Desemba 3, mwaka jana.

Mawakili wa Yoon wamekosoa mashtaka hayo wakisema ni uamuzi mbaya zaidi uliotolewa na idara ya mashtaka, huku chama kikuu cha upinzani kikikaribisha hatua hiyo.

Mashtaka hayo, ambayo hayajawahi kushuhudiwa kwa Rais wa Korea Kusini, yanamuweka Yoon kwenye hatari ya kifungo cha maisha ikiwa atapatikana na hatia kwa amri yake ya sheria ya kijeshi. Amri hiyo ilipiga marufuku shughuli za kisiasa, kuvunja bunge, na kudhibiti vyombo vya habari.

Hatua ya Yoon ilichochea msukosuko wa kisiasa katika taifa hilo, ambalo ni la nne kwa ukubwa wa kiuchumi barani Asia na mshirika mkubwa wa Marekani. Waziri mkuu pia alishtakiwa na kusimamishwa mamlaka, huku maofisa wakuu wa kijeshi wakishtakiwa kwa jukumu lao katika madai hayo ya uasi.

“Tamko la Rais la sheria ya kijeshi ya dharura lilikuwa ombi la kukata tamaa kwa umma kutokana na mzozo wa kitaifa uliosababishwa na upinzani uliokuwa nje ya udhibiti,” walisema mawakili wa Yoon.

Ofisi ya waendesha mashtaka haikutoa maoni mara moja juu ya mashtaka hayo, ingawa vyombo vya habari vya Korea Kusini vimeripoti habari hiyo.

Wachunguzi wa kupambana na ufisadi nchini humo walipendekeza kufunguliwa mashtaka kwa Yoon, ambaye alisimamishwa kazi na bunge Desemba 14.

Mwishoni mwa wiki, mahakama ilikataa mara mbili ombi la waendesha mashtaka la kuongeza muda wa kuzuiliwa kwake wakati uchunguzi zaidi ukiendelea. Hata hivyo, licha ya mashtaka hayo, waendesha mashtaka wameomba tena Yoon kuwekwa kizuizini.

Uasi ni mojawapo ya mashtaka machache ya jinai ambayo Rais wa Korea Kusini hana kinga nayo. Adhabu yake ni kifungo cha maisha au kifo, ingawa Korea Kusini haijatekeleza hukumu ya kifo kwa miongo kadhaa.

“Upande wa mashtaka umeamua kumfungulia mashtaka Yoon Suk Yeol, ambaye anakabiliwa na tuhuma za kuwa kiongozi wa uasi,” alisema msemaji wa chama cha Democratic, Han Min-soo, katika mkutano na waandishi wa habari.

Yoon na mawakili wake walijitetea katika kikao cha Mahakama ya Kikatiba wiki iliyopita, wakidai hakuwahi kukusudia kuweka sheria kamili ya kijeshi. Walisisitiza kuwa alikusudia hatua hizo kama onyo la kuvunja mkwamo wa kisiasa.

Sambamba na mchakato wa uhalifu, mahakama kuu itaamua iwapo itamuondoa Yoon ofisini au kurejesha mamlaka yake ya urais. Mahakama hiyo ina siku 180 kutoa uamuzi wake.

Bunge la Korea Kusini linaloongozwa na upinzani lilimshtaki Yoon Desemba 14, na kumfanya kuwa rais wa pili kushtakiwa nchini humo.

Yoon alibatilisha tamko lake la sheria ya kijeshi takriban saa sita baada ya wabunge kukabiliana na wanajeshi bungeni na kukataa amri hiyo.

Iwapo Yoon ataondolewa madarakani, uchaguzi wa urais utafanyika ndani ya siku 60.

Related Posts